Thursday, July 25, 2013

RODGERS ADAI OFA WALITOA ARSENAL HAILINGANI NA THAMANI YA MCHEZAJI HUYO

KOCHA wa Club ya Liverpool Brendan Rodgers amedai kuwa ofa waliyotoa Arsenal hailingani na thamani aliyonayo mshambuliaji wake Luis Suarez. Liverpool imekataa ofa iliyovunja rekodi ya klabu hiyo ya paundi milioni 40 lakini Suarez anaonekana anataka kuzungumza na timu hiyo yenye maskani yake jijini London. Rodgers amesema kama Arsenal wanamtaka mchezaji huyo wanatakiwa watoe dau ambalo litalingana na thamani yake.  
Kwa maana hiyo Arsenal itatakiwa kuongeza dau zaidi baada ya ofa zake mbili kukataliwa na klabu hiyo. Suarez alionekana kwa mara ya kwanza uwanjani toka alipomng’ata mkono beki wa Chelsea Branislav Ivanovic msimu uliopita wakati alipotokea benchi katika mchezo wa kirafiki walioshinda kwa mabao 2-0 dhidi ya timu ya Melbourne. Suarez alijiunga na Liverpool akitokea klabu ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi mwaka 2011 kwa ada ya paundi milioni 22.7.

JAVU ASAINI JANGWANI KUIMARISHA SAFU YA USHAMBULIAJI YA YANGA

Mshambuliaji nyota wa Club ya  Mtibwa Sugar ya Morogoro, Hussein Javu amesaini Mkataba wa miaka miwili kujiunga na Mabi
ngwa hao wa ligi kuu msimu uliopita Yanga SC ambapo hii leo asubuhi ameanza mazoezi kwenye Uwanja wa Sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga SC, Abdallah Bin Kleb amesema kwamba wamemalizana na Javu pamoja na klabu yake, Mtibwa na sasa huyo ni mchezaji mpya wa Jangwani.

Katika habari ambazo tumezinasa mchezaji huyo ameigharimu Yanga SC zaidi ya Sh. Milioni 60 kwa pamoja fedha alizopewa za usajili na ambazo klabu yake ya Mtibwa imelipwa.
Yanga SC imeamua kumsajili Javu kuimarisha safu yake ya ushambuliaji baada ya kuona kocha Mholanzi, Ernie Brandts hajaridhishwa na mshambuliaji kutoka Nigeria, Ogbu Brendan Chukwudi na wakati huo huo, Hamisi Kiiza anataka dau kubwa aendelee kuichezea timu hiyo.
Kiiza amemaliza Mkataba wake Yanga SC na ili kuongeza Mkataba mwingine, viongozi wanashindwa kufika dau lake na sasa wanaamua kumsajili Javu.
Javu ni kati ya washambuliaji wazuri Tanzania kwa sasa, ambaye kwa misimu mitatu amekuwa mwiba dhidi ya vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga zinapokutana na timu hiyo ya Manungu. 
Kocha Brandts amevutiwa mno na uwezo wa Javu na kwa ujumla amefurahia ujio wake kwenye mazoezi ya Yanga SC leo.Javu ni mchezaji mwenye uzoefu ambaye amekuwa akiitwa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars tangu enzi za Mbrazil, Marcio Maximo ingawa mbele ya Mdenmark, Kim Poulsen hajawahi kupata nafasi.  
Kusajiliwa kwa Javu, kunaongeza ushindani katika safu ya ushambuliaji ya Yanga SC, kwani sasa inakuwa na watu wanne, wengine ni Jerry Tegete, Didier Kavumbangu, Shaaban Kondo, wakati huo huo hatima ya Mnigeria Chukwudi na Kiiza haijajulikana kama wataachwa au watasajiliwa.
Kwa majira haya ya joto, huyo anakuwa mchezaji wa pili wa Mtibwa kusajiliwa Yanga baada ya beki, Rajab Zahir.
Kwa Mtibwa Sugar ni pigo, kwani katika kikosi chao cha kwanza, huyo anakuwa mchezaji wa tatu kuondoka baada ya Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ aliyesajiliwa Simba SC na Shaaban Kisiga aliyejiondoa kwenye timu, baada ya kutofautiana na kocha Mecky Mexime.  
Wakati huo huo, kiungo Rashid Gumbo anaonekana kutikisa kiberiti baada ya kung’ara akiichezea kwa mkopo timu hiyo akitokea Yanga SC. Gumbo amemaliza Mkataba wake Yanga na sasa ili kuendelea kuichezea Mtibwa, lazima wakae naye mezani.Kama ilivyo kawaida kwa Mtibwa ni si jambo la kushangaza kuuza nyota wake kama Arsenal ya England, hali ambayo imepunguza makali yake katika Ligi Kuu miaka ya karibuni, kwani kila nyota anayeibuka anauzwa. Mtibwa iliibuka vizuri katika soka ya Tanzania ikitwaa ubingwa wa Bara mara mbili mfululizo, 1999 na 2000, miaka mitatu tu tangu ianze kucheza Ligi Kuu.










TAIFA STARS YATUA UGANDA KUIVAA THE CRANES

TAIFA_STARS-BORA1Taifa Stars imewasili salama hapa Kampala tayari kwa mechi ya marudiano ya mchujo dhidi ya Uganda (The Cranes) kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Tatu za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Stars ambayo iliwasili ikitokea jijini Mwanza ilipokuwa imepiga kambi ya siku kumi kujiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itakwenda Afrika Kusini mwakani imefikia hoteli ya Mt. Zion iliyoko eneo la Kisseka katikati ya Jiji la Kampala.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, Kim Poulsen ameridhishwa na kiwango cha hoteli hiyo, kwani ndiyo ambayo timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) ilifikia Novemba mwaka jana ilipokuja Kampala kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Stars ambayo ilitiwa chachu na Rais Jakaya Kikwete alipokutana nayo Uwanja wa Ndege wa Mwanza wakati ikiondoka kuja Kampala, na kuitakia kila la kheri itafanya mazoezi yake ya mwisho kesho (Julai 26 mwaka huu) Uwanja wa Mandela kujiandaa kwa mechi ya Jumamosi.
Kocha Kim amesema ingawa mechi hiyo ni ngumu, lakini kikosi chake kimejiandaa kuikabili Uganda kwani wachezaji wako wako vizuri na ari kwa ajili ya mechi iko juu.
Wachezaji wote wako katika hali nzuri, isipokuwa Khamis Mcha aliyekuwa na maumivu ya goti, lakini kwa mujibu wa madaktari wa timu anaendelea vizuri kwani tayari wanampa mazoezi mepesi.
Kikosi cha kamili cha Stars ilichoko hapa kinaundwa na makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas.
Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa.
Wakati huo huo, Kocha Kim Poulsen atakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari siku ya Jumatatu (Julai 29 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)