Wednesday, September 3, 2014

NMB YAIPA SHAVU MKATABA WA KUIDHAMINI AZAM FC MIAKA MIWILI

BENKI ya NMB imejitia kitanzi mkataba wa udhamini wa miaka miwili na mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara, Azam fc, utaohusisha gharama za usafiri na baadhi ya nyingine za uendeshaji wa timu.
Mwenyekiti wa Azam fc, Said Muhammad Said amewaambia waandishi wa habari leo makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo, Azam Complex, Mbande, Chamazi, nje ya jiji la Dar es salaam kuwa mkataba huo utaanza utekelezaji mara moja.
“Tumeupokea kwa furaha mkataba huu na tunapenda kuwashukuru NMB kwa kuungana nasi”. Alisema Said.
Naye katibu mkuu wa Azam fc, Nassor Iddrisa ‘Father’ alifafanua kuwa NMB watanufaika na mkataba huo kwa kutangaza nembo yao katika jezi za Azam fc, mabasi ya Azam fc na kuweka mabango katika uwanja wa Azam Complex.
Pia Azam watavaa jezi zenye nembo ya NMB kuanzia mazoezini na katika mechi za ligi kuu na mashindano ya kimataifa.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa NMB, Mark Weissing amesema mafanikio ya Azam fc ndio chachu ya kuingia ushirikiano na timu hiyo.
Azam fc inakuwa timu ya pili kuingia mkataba na taasisi ya kifedha nchini ambapo timu ya kwanza ni Simba ambayo iliingia mkataba na NMB mwaka 2004, lakini 2004 walitemana.
Pia NMB iliwahi kuidhamini timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa stars kati ya mwaka 2007 na 2010 ikiwa chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo ambaye kwasasa ni kocha mkuu wa Yanga sc.
Wakati wa utiaji saini wa mkataba baina ya Azam fc na NMB, watu wengi walikuwa na hamu ya kujua una thamani gani.

Hata hivyo viongozi wa Azam fc waligoma kutaja thamani ya mkataba huo, lakini taarifa za uhakika zinasema mkataba huo unakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi za Kitanzania Bilioni 1.
Imeelezwa kuwa kwa kila mwaka Azam fc watanufaika na shilingi milioni 500 za Kitanzania kutoka NMB.
Tangu imeanzishwa mwaka 2004 ba kupanda ligi kuu 2008, Azam fc inapata mdhamini kwa mara ya kwanza .
Azam fc inakuwa miongoni mwa timu chache za Tanzania zinazonufaika na udhamini.
Simba na Yanga ndio timu pekee zilizokuwa zinanufaika na udhamini, kwa miaka mingi, lakini siku za karibuni Mbeya City walivuna milioni 360 kutoka kwa Binslum.
Udhamini ni moja ya vyanzo vya mapato kwa klabu za mpira wa miguu, lakini imekuwa changamoto kwa timu mbalimbali kufikia mafanikio ya kupata wadhamini.
Siku zote mdhamini anawekeza sehemu anayoweza kunufaika, hivyo sio rahisi kuweka fedha kwenye timu yenye kiwango kibovu.
Kilio cha kukosa udhamini kwa timu za ligi kuu kinasikika kila kukicha, lakini zimeshindwa kutegua mtego huo tofauti na Azam fc na Mbeya City.
Hakuna haja ya kulia kwa kukosa udhamini, ukiucheza mpira kwa nafasi uliyopata na kufanikiwa kama Mbeya City, Azam fc, Yanga, na Simba, mabilioni na mamilioni yatakuja yenyewe.
Mafanikio ya Azam fc yamewafanya walambe mabilioni kutoka NMB, na timu nyingine zinatakiwa kujipanga kwa kutafuta mafanikio uwanjani zaidi ya kulia kila wakati.

GOR MAHIA WATUA KESHO KUMPIMA PATRICK PHIRI NA SIMBA YAKE

WEKUNDU wa Msimbazi wanatarajia kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa ligi kuu nchini Kenya, Gor Mahia siku ya jumamosi katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Geofrey Nyange ‘Kaburu’, makamu wa Rais wa Simba sc, amewaambia waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuwa kikosi cha Gor Mahia kitawasili kesho uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam kikitokea Nairobi kwa kutumia ndege ya shirika la Kenya.
Kaburu aliongeza kuwa nacho kikosi cha Simba kitawasili siku hiyo hiyo kikitokea Zanzibar kilipoweka kambi ya kujiwinda na ligi kuu.
Licha ya kukipiga na Simba, Gor Mahia imeomba kucheza mechi mbili, hivyo siku ya jumapili watakuwa na mechi nyingine ya kirariki wakati kikosi cha Patrick Phiri kitarejea Zanzibar kuendelea kumalizia program zake za maandalizi kabla ya ligi kuanza septemba 20 mwaka huu.
Awali Simba walipanga kuchuana na Mtibwa Sugar, lakini kocha Phiri akapendekeza kutafutiwa mechi ngumu ya kimataifa ili kuangalia namna kikosi chake kilivyoimarika.
Mechi ya jumamosi itakuwa fursa nzuri kwa mashabiki wa Simba kuwaona wachezaji wao akiwemo mshambuliaji hatari aliyerejea Msimbazi, Mganda Emmanuel Anord Okwi ambaye atavalia jezi yake namba 25 aliyokuwa anaitumia kabla ya kutimkia Etoile Du Sahel ya Tunisia.
Kaburu alisema viingilio katika mechi hiyo ni shilingi elfu 5 (5,000) kwa viti vya kijana, viti vya rangi ya chungwa ni shilingi 10,000, VIP C na B itakuwa shilingi 2,000 wakati VIP A itakuwa shilingi elfu 30,000.
Tiketi kwa ajili ya mchezo huo zitaanza kuuzwa siku ya mechi kuanzia majira ya saa 4:00 asubuhi.
Simba wataanza kampeni za kusaka ubingwa wa ligi kuu bara septemba 21 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam dhidi ya Coastal Union

MECHI YA NGAO YA JAMII BAINA YA YANGA NA AZAM FC WASOGEZWA MBELE

MECHI ya Ngao ya Jamii kuashiria kufunguliwa kwa pazia la ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2013/2014 baina ya mabingwa Azam fc na makamu bingwa, Dar Young Africans sasa utapigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam septemba 14 badala ya septemba 13 mwaka huu kama ilivyopanga.

Shirikisho la soka Tanzania limeamua kuusogeza kwa siku moja mchezo huo uliotakiwa kupigwa jumamosi na sasa kupigwa jumapili kwa lengo la kuwapa fursa mashabiki wengi kuuona.
TFF  imesema jumapili ni siku tulivu kuliko jumamosi na mchezo wa mwaka huu utaambatana na shughuli za kijamii ikiwemo uchangiaji wa damu.
Pia sehemu ya mapato ya mchezo huo yatapelekwa katika shughuli ya kijamii iliyochaguliwa.
Mechi hiyo itapigwa ikiwa ni wiki moja kabla ya kuanza kwa ligi kuu septemba 20 mwaka huu ambapo Yanga wataanzia ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar katika dimba la Jamhuri mkoani Morogoro.
Mnyama Simba atakuwa uwanja wa Taifa siku moja baada ya kufunguliwa kwa ligi kuu (septemba 21 mwaka huuu) dhidi ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union.
Azam fc watakuwa nyumbani Azam Conmplex kuchuana na Polisi Morogoro

Thursday, August 28, 2014

USAJIL LIGI KUU VODACOM TZ BARA BADO WADUNDADUNDA WAPINGWA KALENDA TENA.

Baada ya tarehe 17 baada ya hapo ukaja tarehe 27 na sasa usajili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa wachezaji wa ndani umesogezwa mbele kwa masaa 48 kuanzia jana, kutokana na timu kushindwa kukamilisha usajili katika muda husika jana. Hayo ni kwa mujibu wa Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Selestine Mwesigwa ambapo amesema sababu za kusogeza mbele ni klabu zote za Ligi Kuu kushindwa kukamilisha usajili jana.
Mwesingwa amesema kilichopelekea vilabu vimeshindwa kuutumia huu mfumo wetu mpya wa elektroniki, sasa tumewapa Saa 48 zaidi warekebishe, zikiisha hizo, hapo hakuna nafasi tena, tunasonga mbele. Amesema kwamba hadi muda wa kufunga usajili jana Saa 6:00 usiku, ni timu moja ya Kimondo FC ya Daraja la Kwanza ndiyo iliyokuwa imefanikiwa kukamilisha usajili wake katika mfumo huo.
Mwesingwa amesema tff inapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza Kimondo kwa kumudu kuutumia mfumo huu na kuwasilisha usajili wao ndani ya muda. Hata hiyo Mwesigwa amesema kwamba dirisha la usajili kwa wachezaji wa kigeni litafungwa Septemba 6, mwaka huu. “Hili dirisha la wachezaji wa kigeni likifungwa, hakuna nyongeza ya muda tena, kwa kuwa hili lipo katika mfumo wa kimataifa chini ya FIFA, likifungwa, limefungwa dunia nzima, hivyo nawasihi viongozi wa klabu wahakikishe hawafanyi makoasa.

TWIGA STARS KUELEKEA AFRIKA KUSINI IJUMAA AGOSTI 29 MWAKA HUU.

TIMU ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) inatarajia kuondoka nchini Ijumaa (Agosti 29 mwaka huu) kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya mechi ya kirafiki na timu ya Taifa ya nchi hiyo (Banyana Banyana). Twiga Stars inakwenda huko kwa mwaliko wa Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA) kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa Jumapili (Agosti 31 mwaka huu) katika mji wa Polokwane.
Msafara wa timu hiyo utaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Saloum ambapo utajumuisha wachezaji 18 na benchi la ufundi lenye watu watano.
Wachezaji kwenye msafara huo ni Amina Bilali, Anastaz Katunzi, Asha Rashid, Donisia Minja, Esther Chabruma, Etoe Mlenzi, Fatuma Jawadu, Fatuma Makusanya, Fatuma Maonya, Fatuma Swaleh, Happiness Mwaipaja, Maimuna Said, Mwajuma Abdillahi,
Mwanahamis Shurua, Shelda Mafuru, Sophia Mwasikili, Therese Yona na Zena Rashid.
Benchi la Ufundi linaongozwa na Kocha Rogasian Kaijage, na msaidizi wake Nasra Mohamed. Wengine ni Christine Luambano (daktari), Furaha Mnele (Meneja) na Mwanahamisi Nyomi (mtunza vifaa). Timu hiyo inatarajia kurejea nchini Septemba 2 mwaka huu kwa ndege ya Fastjet.

TANZANIA YAPIGWA CHINI KUANDAA UENYEJI AFCON 2017.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeliandikia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuhusiana na kipengele cha kutaka kwanza nchi iandae Fainali za Afrika kwa Vijana ndiyo iwe na sifa ya kuandaa Fainali za Afrika (AFCON) kiondolewe.
TFF ilishapeleka barua CAF kutaka kipengele hicho kiondolewe, na kutaka kijadiliwe katika Congress (Mkutano Mkuu) ujayo wa CAF.
Tanzania imeshaiandikia CAF barua kuomba uenyeji wa Fainali za AFCON za 2017 baada ya Libya iliyokuwa imepewe uenyeji huo kujitoa. Uamuzi wa Tanzania kuomba kuandaa fainali hizo ulifanywa na Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana Agosti 24 mwaka huu.

MTIHANI WA WAAMUZI, MAKAMISHNA KUFANYIKA SEPTEMBA 5

MTIHANI wa utimamu wa mwili (physical fitness test) kwa waamuzi wanaotaka kuchezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu huu utafanyika katika vituo viwili kuanzia Septemba 5-6 mwaka huu.
Waamuzi watakaoshiriki mtihani huo ni wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na wale wa class one. Pia kutakuwa na semina wa makamishna wanaotaka kusimamia mechi za VPL na FDL ambayo itafanyika Septemba 7 mwaka huu.
 

Vituo vya mtihani huo ni Dar es Salaam na Shinyanga. Kituo cha Dar es Salaam ni kwa waamuzi na makamishna kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Lindi, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Njombe, Pwani, Ruvuma na Tanga.
Kituo cha Shinyanga ni kwa waamuzi na makamishna kutoka mikoa ya Arusha, Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Manyara, Mara, Mwanza, Rukwa, Shinyanga, Simiyu, Singida na Tabora.
Waamuzi wote ambao wamechezesha VPL na FDL msimu wa 2013/2014 na kupata matatizo au kuondolewa kwenye ligi hawahusiki na mtihani huo. Washiriki wanatakiwa kufika kituoni siku moja kabla.
Wasimamizi ni Charles Ndagala, Israel Mujuni, Issarow Chacha, Joan Minja, Pascal Chiganga, Riziki Majala, Said Nassoro, Salum Chama, Soud Abdi,Victor
wandike na Zahara Mohamed.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) wameandaa kozi ya ukufunzi wa utawala itakayofanyika Desemba mwaka huu.
Kozi hiyo itakayoendeshwa na wakufunzi kutoka FIFA itafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Desemba 1 hadi 5 mwaka huu, ambapo sifa ya chini ya elimu kwa wanaotaka kushiriki ni kidato cha nne.
Kwa wanaotaka kushiriki kozi hiyo wanatakiwa kutuma maombi yao kwa Katibu Mkuu wa TFF. Mwisho wa kupokea maombi hayo ni Septemba 5 mwaka huu ambapo wanatakiwa pia kuwasilisha nakala za vyeti vyao vya kitaaluma.