Monday, September 8, 2014

YANGA YASEMA KUFA NA KUPOMA KUHUSU SAKATA LA OKWI KUKATAA RUFAA FIFA YASEMA MPAKA KIELEKE

Uongozi wa klabu ya Yanga umesema utapinga maamuzi ya kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji  kuhusiana na maamuzi yake ya kumtangaza mchezaji wake, Emmanuel Okwi kuwa huru.
Mwenyekiti wa Kamati  ya Sheria ya Yanga, Sam Mapande amesema kuwa hawajaridhishwa na maamuzi hayo ambayo yanakinzana na shitaka zima la mchezaji huyo.
Mapande amesema kuwa kamati ya TFF imeamua sakata la Okwi kinyume na malalamiko yao kwani hakukuwa na lalamiko la mchezaji huyo wa Uganda kuhusiana na malipo ya fedha zake za usajili.
Alisema kuwa cha kushangaza, kamati hiyo ya TFF iliamua kusikiliza kesi ambayo haikuwa mbele yao na kutoa maamuzi ambayo hata wao wameshangazwa nayo.
“Kwanza kesi yenyewe ilikuwa haijamalizika, walituambia tuwasilishe vielelezo kuhusiana na kitendo cha mchezaji huyo kufanya mazungumzo na klabu ya Misri, lakini cha kushangaza maamuzi yametolewa, hili limetushangaza sana,” alisema Mapande.
Alisema kuwa mazingira yalikuwa yameandaliwa kuibeba Simba na Okwi kwani hata malalamiko yao kwa Simba hayakusikilizwa. “Malalamiko yetu yalikuwa wazi kabisa, yapo kimaandishi, hatukuwai kulalamikiwa, suala la fedha za usajili la Okwi limetoka wapi, kama lilikuwepo, mbona hatujajulishwa kimaandishi kama utaratibu ulivyo,” alisema.
Alisema kuwa Kamati hiyo kumruhusu mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo Zacharia Hans Pope ambaye pia ni mwenyekiti wakamati ya usajili ya Simba kuwemo katika kikao hicho kinyume na taratibu za Fifa kupitia kifungu namba 19 kinachoeleza mgongano wa kimaslah.

                                              MAAMUZI YA KIKAO CHA JANA
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekutana leo (Septemba 7
mwaka huu) na kupitia masuala mbalimbali ikiwemo mgogoro wa kimkataba kati ya klabu ya Yanga na mchezaji Emmanuel Okwi.

Mkataba huo ulipitiwa na Kamati ikiwemo kumsikiliza mchezaji mwenyewe pamoja na upande wa Yanga, na kuridhika kuwa mkataba kati ya pande hizo umevunjika.

Ukiwa ni mkataba wa pande mbili, Yanga ilikiuka kipengele namba 8 kuhusu malipo ya ada ya usajili.

Yanga ikiwa mwajiri, haikutekeleza kipengele hicho cha kimkataba hadi kufikia Juni 27 mwaka huu ilipoandika barua TFF kuomba mkataba huo uvunjwe. Kwa maana hiyo Okwi ni mchezaji huru, hivyo yuko huru kujiunga na timu yoyote.
Mkataba ni uhusiano kati ya mwajiri (Yanga) na mwajiriwa (Okwi), ambapo Kamati imebaini kuwa uhusiano huo haupo,hivyo hakuna mazingira ya pande hizo mbili kuendelea kufanya kazi pamoja.

Pamoja na Yanga kuwasilisha pingamizi la kuwepo mmoja wa wajumbe katika kikao kwa sababu za kimaslahi (conflict of interests), walifahamishwa kuwa kilichopo mbele ya kamati ni mgogoro wa kimkataba kati ya Yanga na Okwi, na si usajili.

Pia lilijitokeza suala la Okwi kutakiwa na klabu ya Wadi Degla ya Misri. Kamati imeiagiza Sekretarieti ya TFF kulifanyia uchunguzi suala hilo na kulitolea taarifa katika kikao kijacho.

Hata hivyo mjumbe huyo hakushiriki katika kuchangia hoja na kutoa maamuzi. Uamuzi wa kamati ulifanyika baada ya majadiliano, hivyo hakukuwa na suala la kupiga kura.

Kuhusu pingamizi la Coastal Union kwa Abdi Banda, Kamati imebaini kuwa klabu hiyo imevunja mkataba kati ya pande hizo mbili kwa kushindwa kumlipa mchezaji huyo mshahara wa miezi mitatu mfululizo kama takwa la mkataba.
Klabu ya Coastal Union iliwakilishwa na mmoja wa viongozi wake, wakati Banda aliwakilishwa na mwanasheria wake.

Vilevile Kamati imekubaliana na pingamizi la Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA) kuhusu wachezaji waliofanyiwa uhamisho kutoka katika mkoa wake bila kulipiwa ada za usajili, hivyo klabu husika zinatakiwa kulipa ada hizo.

Pia Kamati imeagiza klabu zote zilizosajili wachezaji bila kuwafanyia uhamisho, kulipa ada za uhamisho kwa pande husika kabla ya kuanza ligi, vinginevyo leseni zao zitazuiwa hadi watakapolipa.

Mashauri mengine ya pingamizi yatasikilizwa baadaye kwa vile klabu husika hazikupata fursa ya kufika mbele ya kamati.

TFF YATUMA RAMBIRAMBI MSIBA WA MWAMUZI LUGENGE

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mwamuzi wa daraja la kwanza (class one), Luteni  David Lugenge kilichotokea jana (Septemba 7 mwaka huu) kwa ajali ya gari katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Luteni Lugenge ambaye mwishoni mwa wiki alishiriki mitihani ya utimamu wa mwili kwa waamuzi wa Ligi Kuu alikuwa na ndugu yake Christopher Alexander Lunyungu katika gari dogo wakienda mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Handeni, Peter Juma, Luteni Lugenge alikuwa akimsindikiza mwenzake aliyekuwa anakwenda kujitambulisha kwa wakwe zake watarajiwa.
Msiba huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu kwani Luteni Lugenge alikuwa ni mmoja wa waamuzi wanaoinukia nchini, hivyo mchango wake ulikuwa bado unahitajika. Hivyo tutamkumbuka daima.
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Luteni Lugenge, Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu nchini (FRAT) na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
 BONIFACE WAMBURA
KNY KATIBU MKUU
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

BRATTER ASEMA BADO NATAKA UONGOZI WA FIFA-URAIS


Sepp Blatter ambae ni raisi wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA  amethiboitisha kuwa atatetea kiti chake hicho katika uchaguzi ujao wa shirikisho hilo. Akihojiwa jijini Manchester Blatter mwenye umri wa miaka 78 alithibitisha uamuzi wake huo kuhu akidai atatoa taarifa rasmi katika mkutano mkuu wa kamati ya utendaji ya FIFA utakaofanyika Septemba 25 na 26. Tayari rais wa Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA Michel Platini ameshatangaza kutogombea nafasi hiyo ya Blatter. Blatter ambaye amekuwa katika kiti hicho cha FIFA toka mwaka 1998 amesema amechukua uamuzi huo kwasababu kazi alioianza anaona bado haijamalizika.

Wednesday, September 3, 2014

AZAM FC KIBOKO, AISHI MANULA AITWA TAIFA STARS AZAM KUWA NA WACHEZAJI 10 TAIFA

Mlinda mlango Chipukizi wa Azam FC AISHI MANULA ameongezwa katika kikosi cha wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' inayojiandaa kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Burundi tarehe 7 September 2014. Sasa Azam FC ina jumla ya wachezaji 10 katika kikosi cha Stars ambao ni

1.MWADINI ALI
2. SHOMARI KAPOMBE 
3. ERASTO NYONI 
4. SAID MORAD 
5. AGGREY MORIS 
6. HAMIS MCHA 
7. HIMIDI MAO 
8. SALUM ABUBAKAR 
9. JOHN BOCCO 
10. AISHI MANULA 


NMB YAIPA SHAVU MKATABA WA KUIDHAMINI AZAM FC MIAKA MIWILI

BENKI ya NMB imejitia kitanzi mkataba wa udhamini wa miaka miwili na mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara, Azam fc, utaohusisha gharama za usafiri na baadhi ya nyingine za uendeshaji wa timu.
Mwenyekiti wa Azam fc, Said Muhammad Said amewaambia waandishi wa habari leo makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo, Azam Complex, Mbande, Chamazi, nje ya jiji la Dar es salaam kuwa mkataba huo utaanza utekelezaji mara moja.
“Tumeupokea kwa furaha mkataba huu na tunapenda kuwashukuru NMB kwa kuungana nasi”. Alisema Said.
Naye katibu mkuu wa Azam fc, Nassor Iddrisa ‘Father’ alifafanua kuwa NMB watanufaika na mkataba huo kwa kutangaza nembo yao katika jezi za Azam fc, mabasi ya Azam fc na kuweka mabango katika uwanja wa Azam Complex.
Pia Azam watavaa jezi zenye nembo ya NMB kuanzia mazoezini na katika mechi za ligi kuu na mashindano ya kimataifa.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa NMB, Mark Weissing amesema mafanikio ya Azam fc ndio chachu ya kuingia ushirikiano na timu hiyo.
Azam fc inakuwa timu ya pili kuingia mkataba na taasisi ya kifedha nchini ambapo timu ya kwanza ni Simba ambayo iliingia mkataba na NMB mwaka 2004, lakini 2004 walitemana.
Pia NMB iliwahi kuidhamini timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa stars kati ya mwaka 2007 na 2010 ikiwa chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo ambaye kwasasa ni kocha mkuu wa Yanga sc.
Wakati wa utiaji saini wa mkataba baina ya Azam fc na NMB, watu wengi walikuwa na hamu ya kujua una thamani gani.

Hata hivyo viongozi wa Azam fc waligoma kutaja thamani ya mkataba huo, lakini taarifa za uhakika zinasema mkataba huo unakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi za Kitanzania Bilioni 1.
Imeelezwa kuwa kwa kila mwaka Azam fc watanufaika na shilingi milioni 500 za Kitanzania kutoka NMB.
Tangu imeanzishwa mwaka 2004 ba kupanda ligi kuu 2008, Azam fc inapata mdhamini kwa mara ya kwanza .
Azam fc inakuwa miongoni mwa timu chache za Tanzania zinazonufaika na udhamini.
Simba na Yanga ndio timu pekee zilizokuwa zinanufaika na udhamini, kwa miaka mingi, lakini siku za karibuni Mbeya City walivuna milioni 360 kutoka kwa Binslum.
Udhamini ni moja ya vyanzo vya mapato kwa klabu za mpira wa miguu, lakini imekuwa changamoto kwa timu mbalimbali kufikia mafanikio ya kupata wadhamini.
Siku zote mdhamini anawekeza sehemu anayoweza kunufaika, hivyo sio rahisi kuweka fedha kwenye timu yenye kiwango kibovu.
Kilio cha kukosa udhamini kwa timu za ligi kuu kinasikika kila kukicha, lakini zimeshindwa kutegua mtego huo tofauti na Azam fc na Mbeya City.
Hakuna haja ya kulia kwa kukosa udhamini, ukiucheza mpira kwa nafasi uliyopata na kufanikiwa kama Mbeya City, Azam fc, Yanga, na Simba, mabilioni na mamilioni yatakuja yenyewe.
Mafanikio ya Azam fc yamewafanya walambe mabilioni kutoka NMB, na timu nyingine zinatakiwa kujipanga kwa kutafuta mafanikio uwanjani zaidi ya kulia kila wakati.

GOR MAHIA WATUA KESHO KUMPIMA PATRICK PHIRI NA SIMBA YAKE

WEKUNDU wa Msimbazi wanatarajia kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa ligi kuu nchini Kenya, Gor Mahia siku ya jumamosi katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Geofrey Nyange ‘Kaburu’, makamu wa Rais wa Simba sc, amewaambia waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuwa kikosi cha Gor Mahia kitawasili kesho uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam kikitokea Nairobi kwa kutumia ndege ya shirika la Kenya.
Kaburu aliongeza kuwa nacho kikosi cha Simba kitawasili siku hiyo hiyo kikitokea Zanzibar kilipoweka kambi ya kujiwinda na ligi kuu.
Licha ya kukipiga na Simba, Gor Mahia imeomba kucheza mechi mbili, hivyo siku ya jumapili watakuwa na mechi nyingine ya kirariki wakati kikosi cha Patrick Phiri kitarejea Zanzibar kuendelea kumalizia program zake za maandalizi kabla ya ligi kuanza septemba 20 mwaka huu.
Awali Simba walipanga kuchuana na Mtibwa Sugar, lakini kocha Phiri akapendekeza kutafutiwa mechi ngumu ya kimataifa ili kuangalia namna kikosi chake kilivyoimarika.
Mechi ya jumamosi itakuwa fursa nzuri kwa mashabiki wa Simba kuwaona wachezaji wao akiwemo mshambuliaji hatari aliyerejea Msimbazi, Mganda Emmanuel Anord Okwi ambaye atavalia jezi yake namba 25 aliyokuwa anaitumia kabla ya kutimkia Etoile Du Sahel ya Tunisia.
Kaburu alisema viingilio katika mechi hiyo ni shilingi elfu 5 (5,000) kwa viti vya kijana, viti vya rangi ya chungwa ni shilingi 10,000, VIP C na B itakuwa shilingi 2,000 wakati VIP A itakuwa shilingi elfu 30,000.
Tiketi kwa ajili ya mchezo huo zitaanza kuuzwa siku ya mechi kuanzia majira ya saa 4:00 asubuhi.
Simba wataanza kampeni za kusaka ubingwa wa ligi kuu bara septemba 21 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam dhidi ya Coastal Union

MECHI YA NGAO YA JAMII BAINA YA YANGA NA AZAM FC WASOGEZWA MBELE

MECHI ya Ngao ya Jamii kuashiria kufunguliwa kwa pazia la ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2013/2014 baina ya mabingwa Azam fc na makamu bingwa, Dar Young Africans sasa utapigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam septemba 14 badala ya septemba 13 mwaka huu kama ilivyopanga.

Shirikisho la soka Tanzania limeamua kuusogeza kwa siku moja mchezo huo uliotakiwa kupigwa jumamosi na sasa kupigwa jumapili kwa lengo la kuwapa fursa mashabiki wengi kuuona.
TFF  imesema jumapili ni siku tulivu kuliko jumamosi na mchezo wa mwaka huu utaambatana na shughuli za kijamii ikiwemo uchangiaji wa damu.
Pia sehemu ya mapato ya mchezo huo yatapelekwa katika shughuli ya kijamii iliyochaguliwa.
Mechi hiyo itapigwa ikiwa ni wiki moja kabla ya kuanza kwa ligi kuu septemba 20 mwaka huu ambapo Yanga wataanzia ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar katika dimba la Jamhuri mkoani Morogoro.
Mnyama Simba atakuwa uwanja wa Taifa siku moja baada ya kufunguliwa kwa ligi kuu (septemba 21 mwaka huuu) dhidi ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union.
Azam fc watakuwa nyumbani Azam Conmplex kuchuana na Polisi Morogoro