Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes)
imewasili Dar es Salaam leo tayari kwa mechi ya kwanza ya mchujo kusaka
tiketi ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya Ndani (CHAN) kati
yake na Tanzania (Taifa Stars) itak
ayochezwa Jumamosi Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
The Cranes inayofundishwa na Mserbia
Sredojvic Micho imetua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA) saa 5.30 asubuhi kwa ndege ya Air Uganda, na imefikia hoteli ya
Sapphire.
Timu hiyo leo (Julai 11 mwaka huu)
itafanya mazoezi saa 9 alasiri kwenye Uwanja wa Karume, wakati kesho saa
9 alasiri itafanya mazoezi Uwanja wa Taifa, kabla ya kuipisha Taifa
Stars itakayoanza mazoezi saa 10 kamili jioni.
Taifa Stars inayofundishwa na Mdenmark
Kim Poulsen, na kudhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, leo kwa mujibu
wa program yake haitakuwa na mazoezi.
Wachezaji wanaounda The Cranes ni makipa
Ismail Watenga, Kimera Ali na Muwonge Hamza. Mabeki ni Guma Dennis,
Kasaaga Richard, Kawooya Fahad, Kisalita Ayub, Magombe Hakim, Malinga
Richard, Mukisa Yusuf, Savio Kabugo na Wadada Nicholas.
Viungo ni Ali Feni, Birungi Michael,
Frank Kalanda, Hassan Wasswa, Kyeyune Said, Majwega Brian, Mpande
Joseph, Muganga Ronald, Ntege Ivan, Owen Kasule, wakati washambuliaji ni
Edema Patrick, Herman Wasswa na Tonny Odur.
TENGA KUZUNGUMZA NA WAANDISHI KESHO
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Leodegar Tenga atakuwa na mkutano na waandishi wa
habari. Mkutano huo utafanyika kesho (Julai 12 mwaka huu) saa 4 asubuhi
kwenye hoteli ya Tansoma.
Kutokana na mkutano huo, sasa mkutano
kati ya makocha wa Taifa Stars na The Cranes uliokuwa ufanyike saa 5
asubuhi ofisi za TFF nao umehamishiwa hoteli ya Tansoma. Mkutano huo pia
utahusisha manahodha wa timu zote mbili.
WAJUMBE MKUTANO MKUU MAALUMU KUWASILI KESHO
Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) utakaofanyika Jumamosi
(Julai 13 mwaka huu) wanawasili jijini Dar es Salaam kesho (Julai 12
mwaka huu).
Mkutano huo wa marekebisho ya Katiba
utakuwa chini ya uenyekiti wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga na utafanyika
ukumbi wa NSSF Waterfront kuanzia saa 3 kamili asubuhi. Wajumbe wote wa
mkutano huo watafikia hoteli ya Travertine.
Pia mkutano huo utahudhuriwa na wageni
mbalimbali waalikwa wakiwemo kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA) na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA).
MECHI YA STAND, KIMONDO NAYO KUPIGWA JUMAPILI
Mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa
wa Mikoa (RCL) kati ya Stand United FC ya Shinyanga na Kimondo SC ya
Mbeya iliyokuwa ichezwe Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) imesogezwa mbele
kwa siku moja.
Timu hizo sasa zitacheza Jumapili (Julai
14 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Kimondo
ilishinda bao 1-0 mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 6 mwaka huu Uwanja
wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi nyingine ya ligi hiyo itakuwa kati
ya Friends Rangers ya Dar es Salaam na Polisi Jamii ya Mara, na
itafanyika kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi nje kidogo ya Jiji la
Dar es Salaam. Mwamuzi wa mechi hiyo ni Hans Mabena kutoka Tanga.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)