Wednesday, May 28, 2014

TAIFA STARS KWENDA HARARE ALHAMISI KUIKABILI ZIMBAMWE

TFF_LOGO12Msafara wa watu 30 wa Taifa Stars unaojumuisha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi unaondoka kesho alfajiri (Mei 29 mwaka huu) kwenda Harare, Zimbabwe kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika.
Mechi hiyo itachezwa Juni Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Harare, Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itatua jijini humo saa 5 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways.
Msafara wa Taifa Stars ambayo ambayo jana (Mei 27 mwaka huu) ilicheza mechi ya kujipima nguvu na Malawi na kushinda bao 1-0, na utarejea nchini Juni 2 mwaka huu unaongozwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi.
Wakati huo huo, mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars na Malawi (Flames) iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 8,380,000 kutokana na watazamaji 1,504 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo.
Mgawo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 1,278,305.08, gharama za kuchapa tiketi sh. 225,600, gharama za uwanja sh. 1,031,414.24, gharama za mechi sh. 1,375,218.98 na TFF/Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 4,469,461.69.
MWAMBUSI KOCHA BORA VPL 2013/2014
Kocha Mkuu wa timu ya Mbeya City, Juma Mwambusi ameshinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa msimu wa 2013/2014.
Hafla ya kukabidhi tuzo kwa washindi mbalimbali ilifanyika jana (Mei 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Mbali ya tuzo hiyo, Kocha Mwambusi ambaye hivi sasa yuko nchini Sudan na timu yake kwenye michuano ya Nile Basin alipata pia zawadi ya kitita cha sh. milioni 7.8.
Aliyeshinda tuzo ya kipa bora ni Hussein Shariff wa Mtibwa Sugar aliyepata sh. milioni 5.2 wakati Amisi Tambwe wa Simba aliibuka na tuzo ya mfungaji bora. Tambwe naye alipata sh. milioni 5.2.
Mchezaji bora wa VPL kwa msimu wa 2013/2014 ni Kipre Tchetche wa Azam FC aliyejipatia sh. milioni 5.2. Tuzo ya refa bora imetwaliwa na Israel Mujuni aliyezawadiwa sh. milioni 7.8.
Yanga iliyoshika nafasi ya pili kwenye ligi na kupata sh. milioni 37, pia ilipata sh. milioni 16 baada ya kushinda tuzo ya timu yenye nidhamu ya hali ya juu. Sh. milioni 21 za mshindi wa nne zilikwenda kwa timu ya Simba.
Mabingwa wapya wa VPL, Azam FC walipata sh. milioni 75 wakati Mbeya City ilipata sh. milioni 26 kwa kushika nafasi ya tatu.
RAIS MALINZI ATUMA RAMBIRAMBI MSIBA WA KOCHA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zambia (FAZ), Kalusha Bwalya kutokana kifo cha Kocha wa timu ya Nkana FC, Masauso Mwale.
Amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha ghafla cha Kocha Mwale, na kuongeza kuwa msiba huo si pigo kwa Zambia pekee bali Afrika kwa ujumla kwa vile ni mfano wa kuigwa kwa makocha wazalendo waliozipatia mafanikio makubwa klabu za Afrika.
Rais Malinzi amemuomba Rais Bwalya kutuma salamu zake za rambirambi kwa familia ya Mwale, na kuitaka kuwa na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito kwao.
Mwale (51) alifariki mwishoni mwa wiki kwa ajali ya gari aliyokuwa akiendesha katika barabara ya Kitwe- Ndola akienda kambini kujiunga na timu yake kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Sewe San Pedro ya Ivory Coast.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

KUELEKEA MSIMU MPYA WA LIGI VP TIMU ZILIZO KAMILISHA USAJILI MPAKA SASA.


Katika harakati za kuelekea msimu mpya wa ligi kuu Vodacom Tanzania bara timu mbalimbali tayari zimekwisha anza kufanya usajili wa hapa na pale
Tukianza na Wagomga Nyundo wa jiji la mbeya Timu ya Mbeya City kutoka Mkoani Mbeya, tayari imekamilisha usajili wa
Mshambuliaji kutoka Timu ya Kagera Sugar Themi Felix na Kiungo Peter Mwalianzi kutoka timu ya JKT Mgambo.
Safu ya Ushambuliaji ya Timu hiyo iliyofanikiwa kushika Nafasi ya Tatu kwenye Ligi Kuu Vodacom, VPL, Msimu huu, itakuwa sasa na Paul Nonga, Mwagane Yeya, Saad Kipanga na Themi Felix kuanzia msimu ujao na huku Peter Mwalianzi akiongeza nguvu kwenye safu ya Kiungo inayoongozwa na Steven Mazanda.

Tuwatazame Mabingwa wapya wa VPL, Azam FC, tayari walishakamilisha usajili wa Frank Domayo na Didier Kavumbagu kutoka Yanga na kumuongeza Beki Abdallah Heri kutoka Klabu ya Zimamoto ya kule Zanzibar.
Hivyo basi kwa sasa safu ya Kiungo ya Mabingwa hao itaundwa na Hi
mid Mao, Kipre Balou, Salumu Abubakary na Domayo Frank huku Brian Umony, Gaudence Mwaikimba, John Bocco, Kipre TcheTche na Kavumbagu wakikamilisha Safu ya Ushambuliaji.

Nao Timu ya Ruvu Shooting iliyomaliza Msimu kwenye Nafasi ya Tano baada ya kupata Alama 38, tayari imekamilisha usajili wa Zuberi Dabi kutoka Klabu ya Kagera Sugar. Timu hiyo pia imefanikiwa kumsajili Chagu Chagula mshambuliaji Raia wa Tanzania ambaye amecheza sana Nchini Burundi.
Kwa upande wa Wagosi wa Kaya Baada ya kuandaa mkakati na kuachana na Wachezaji wanaotemwa na Timu za Simba na Yanga, Klabu ya Coastal Union ya Tanga tayari imekamilisha usajili wa Bright Obina ambaye aliwahi kuzichezea African Lyon na Ashanti United zote za Dar es Salaam.
Timu hiyo pia imefanikiwa kumnasa Hussein Swed ambaye Msimu uliopita alikuwa na Timu iliyoshuka Daraja ya Ashanti United na sasa wote wametua kwa Wagosi wa Kaya.
Kwa upande wa Simba wekundu msimbazi mpaka sasa bado hawaja weka hadharani majina wachezaji waliowasajili licha ya kuwa na taarifa za kuwa bado wapo katika harakati za kufanya usajili na upo uwezakoano kutwaa wachezaji kutoka kadhaa kutoka nje ya boda Uganda au Kenya ili kuweza kuimarisha kikosi hicho ambacho kwa sasa kipo katika harakati za uchaguziwa viongozi unaotaraji kufanyika Juni 29 mwaka huu.
Yanga nao washindi wa pili wa ligi kuu msimu uliopita tayari wamefanikisha kumnasa Kiungo Omega Seme aliyekuwa kwa Mkopo kwa Wajelajela Tanzania Prison pamoja na kafinikisha kumbakisha Beki Kisiki Mbuyu Twite Baada ya Kuondoka kwa aliye kuwa kiungo chumvi Frank Domayo pamoja na Mshambuliaji Didier Kavumbagu.
Kwa mujibu wa TFF, Usajili wa Wachezaji kwa hatua ya kwanza Msimu mpya wa 2014/2015 unaanza Juni 15 hadi Agosti 3 Mwaka huu wakati Kipindi cha kutangaza Wachezaji walioachwa au kusitishiwa Mikataba ni kuanzia Juni 15 hadi 30.
Kipindi cha kwanza cha Uhamisho wa Wachezaji ni kuanzia Juni 15 hadi Julai 30.
Kupitia Majina na kutangaza pingamizi ni kati ya Agosti 4 na 11 na kuthibitisha Usajili hatua ya awali ni Agosti 12 hadi 14.
Usajili hatua ya pili utakuwa kati ya Agosti 14 na 29 wakati kupitia na kutangaza Majina ya pingamizi hatua ya pili ya usajili ni kuanzia Agosti 30 hadi Septemba 4. Uthibitisho wa Usajili hatua ya pili ni Septemba 5 na 6.
Ligi Kuu ya Vodacom, VPL, inatarajiwa kuanza Agosti 24 na Ratiba inatarajiwa kutoka Mwezi mmoja kabla hapo Julai 24.

Monday, May 26, 2014

TIMU YA U15 YA TANZANIA YAENDELEZA WIMBI MICHEZO YA VIJANA AYG

Tanzania imeendelea kung’ang’ara kwenye Michezo ya Afrika kwa Vijana (AYG) kwa upande wa mpira wa miguu kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 baada ya jana (Mei 25 mwaka huu) kuichapa Swaziland mabao 3-0.
3201Tanzania-flagMabao ya Tanzania katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Gaborone, Botswana yalifungwa na Amani Ally dakika ya sita, Nasson Chanuka dakika ya 32 wakati Amos Kennedy alikamilisha ushindi huo kwa bao la dakika ya 53.
Katika mechi yake ya kwanza, Tanzania ilitoka sare ya bao 1-1 na Mali na baadaye kuwafunga wenyeji Botswana mabao 2-0. Mechi za michuano hiyo zinaoneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini.
Tanzania itacheza mechi yake ya nne kesho (Mei 27 mwaka huu) dhidi ya Nigeria wakati mechi ya mwisho itafanyika Mei 29 mwaka huu dhidi ya Afrika Kusini.

TAIFA STARS, MALAWI KUONESHANA SHUGHULI DAR, KIINGILIO BUKU 5 TU!

10357474_634079413340945_8148690486284095511_nTaifa Stars na Malawi (Flames) zinapambana kesho (Mei 27 mwaka huu) katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 kamili jioni.
Malawi tayari ipo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi hiyo wakati Taifa Stars iliyopiga kambi yake Tukuyu mkoani Mbeya inawasili jijini Dar es Salaam kesho (Mei 27 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwa ndege ya Air Tanzania.

Saturday, May 24, 2014

MBEYA CITY YAANZA VYEMA YAITANDIKA ACADEMI YA BURUNDI 3-MTUNGI

IMG_1150
WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano mipya ya CECAFA Nile Basin Cup inayoendelea nchini Sudan , Mbeya City fc  wameanza kutupa karata yao ya kwanza vyema hii leo majira ya 11:30 jioni kwa saa za Sudan dhidi ya Academie Tchite ya Burundi.

Ambapo katika mchezo huo mbeya city imefanikiwa kuibuka na ushindi mnono wa bao 3-2 mabao hayo yakiwekwa kimiani na  Paul nonga,kaptein Mwagane yeya pamoja Themi felix katika mechi hiiyo iliopigwa uwanja wa Al-Merreikh mjini Khartoum
.

TP MAZEMBE SAMATA, ULIMWENGU DHIDI YA AS VITA MJINI LUBUMBASHI

1WASHAMBULIAJI  wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samata na Thomas Emmanuel Ulimwengu kesho jumapili wanatarajia kuiongoza TP Mazembe katika mchezo wa hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya wapinzani wao wakubwa, AS Vita mjini Lubumbashi.
Timu hizi hasimu zitakutana katika mchezo wa kesho zikiwa na kumbukumbu ya kusababisha maafa ya vifo vya watu zaidi ya 15 katika mchezo wao wa ligi kuu ya DR Congo wiki za karibuni.
Tukio hilo baya lilitokea mjini Kinshasa baada ya mashabiki wa AS Vita kutoridhishwa na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa wapinzania wao TP Mazembe.
Mchezo wa kesho umevuta hisia za mashabiki wengi wa soka, kwani timu hizi zinapokutana, upinzani unakuwabmkubwa mno nje ya uwanja na ndani ya uwanja.

FAINALI BEACH SOCCER KUTIMUA VUMBI KESSHO JUMAPILI

Fainali ya michuano ya mpira wa miguu ya ufukweni (beach soccer) kati ya timu za Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) inachezwa kesho (Mei 25 mwaka huu) kwenye ufukwe wa Escape One uliopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.
beach-soccer-finalTimu hizo zimepata nafasi ya kucheza fainali baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali dhidi Chuo Kikuu cha Ardhi (AU) na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) zilizochezwa wikiendi iliyopita.
Mgeni rasmi katika fainali hiyo itakayooneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Azam Tv atakuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na itaanza saa 4.15 asubuhi. Fainali hiyo itatanguliwa na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya AU na TIA kuanzia saa 3 kamili asubuhi.
Michuano hiyo ambayo ni ya kwanza kufanyika nchini ilishirikisha vyuo 13 vya Dar es Salaam, na ilianza Aprili 20 mwaka huu katika fukwe za Escape One na Gorilla iliyopo Kigamboni.
Vyuo vingine vilivyoshiriki ni Chuo Kikuu cha St. Joseph Tanzania (SJUIT), Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO), Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW) na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Vingine ni Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Utawala wa Kodi (ITA), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ).
Tanzania itashiriki katika michuano ya Afrika ya mpira wa miguu wa ufukweni itakayofanyika mwakani nchini Shelisheli                                                                        
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)