Thursday, May 2, 2013

KUTOKUWEPO KWA MESSI NI BAHATI KWETU-JUPP


Bosi wa THE BAVARIANI klabu ya Bayern Munich, Jupp Heynckes anaamini kuwa kikosi chake kilipata bahati kwakuwa mshambuliaji nyota wa Barcelona Lionel Messi hakuwemo katika kikosi hicho kitendo ambacho kilipelekea timu hiyo kushinda kwa mabao 3-0 kwenye mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Camp Nou. Mshambuliaji huyo wa kimataifa alikuwa katika benchi akitizama mabao ya Arjen Robben, bao la kujifungala Gerard Pique na Thomas Muller yakiididimiza timu hiyo kwa jumla ya mabao 7-0 katika mechi mbili za nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya walizokutana. Wakati Heynckes akisifu umakini wa kikosi chake katika mechi hiyo ya marudiano lakini amekiri kuwa wapinzani wao walikuwa tofauti bila ya kuwepo nyota wao Messi. Kocha huyo amesema hakuna mtu aliyetegemea kuwa kikosi chake kingeibuka na ushindi wa mabao 7-0 katika mechi mbili walizokutana lakini pamoja na hivyo huwezi kusema zama za Barcelona zimekwisha kwasababu waliwakosa nyota wao wengi ambao ni majeruhi.
na kwa upande wake meneja wa klabu ya FC Barcelona, Tito Vilanova ametanabaisha kwamba majeruhi sio sababu ya kukosekana kwa mshambuliaji nyota wa klabu hiyo Lionel Messi katika mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina aliwashangaza mashabiki wa timu hiyo baada ya kuondolewa katika kikosi kilichoanza dhidi ya Bayern huku wengi wakidhani majeruhi ya msuli wa paja ndio chanzo kikubwa cha kukosekana kwake. Hata hivyo kwa mujibu wa Vilanova majeruhi halikuwa tatizo la kumuacha Messi na kudai kuwa angeweza kumpa nafasi nyota huyo kuingia katika kipindi cha pili kama angedhani kikosi chake kilikuwa na nafasi ya kufika fainali. Vilanova amesema Messi hakuwa mgonjwa kama watu wanavyofikiri lakini alikuwa hajisikii vyema hivyo alifikiri kwamba kwa hali aliyokuwa nayo asingeweza kuisaidia timu hiyo kwa muda ule.

BIN KHALIFA AMETEULIWA KUWA MJUMBE WA FIFA
SHIRIKISHO la Soka barani Asia limemchagua Sheikh Salman Bin Ebrahim Al Khalifa kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA katika uchaguzi uliofanyika Malaysia. Al Khalifa ambaye ni raia wa Bahrain alifanikiwa kupata kura 28 katika kura 46 zilizopigwa ambapo alimshinda Hassan Al Thawadi wa Qatar aliyepata kura 18. Al Khalifa amewahi kuikosa nafasi hiyo ya juu kabisa ya maamuzi ya FIFA kwa kura chache baada ya kuzidiwa na aliyekuwa rais wa AFC Mohamed Bin Hammam kwa kura 23 kwa 21 mwaka 2009. AFC pia imemteua Al Khalifa kugombea nafasi ya urais wa shirikisho kwa kipindi kingine cha miaka miwili.