Wanandinga wa kimataifa wa Ivory Coast, Kolo Toure anayekipiga katika klabu ya Manchester City na Emmanuel Eboue wa klabu ya Galatasaray wanakabiliwa na adhabu ya kufungiwa kuitumikia timu ya taifa ya nchi hiyo kufuatia kauli walizozitoa katika vyombo vya habari kulishambulia Shirikisho la Soka la nchi hiyo. Wachezaji hao wawili wameenguliwa katika kikosi cha nchi hiyo ambacho kitapambana na Gambia na Tanzania katika mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2014. Hatua hiyo ya kuwaacha wachezaji hao ilifikiwa na kamati ya nidhamu ya shirikisho hilo kufuatia malalamiko yaliyofikishwa na kocha anayekinoa kikosi hicho Sabri Lamouchi. Ivory Coast inatarajia kuchuana Gambia Juni 8 mwaka huu kabla ya kupambana na Taifa Stars Juni 16 katika michezo ya kundi C ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia.