
African Sports Mabingwa wa Kombe la Jamhuri mnamo mwaka 1988 maarufu Wanakimanumanu" wanatarajiwa kufanya mkutano mkuu wa uchaguzi Agosti 15 mwaka huu baada ya uongozi wa muda uliopo madarakani kumaliza wakati wake.
Akizungumza na mkali wa dimba Msemaji wa Club hiyo Said Karsandas Junior ametanabisha kuwa uchaguzi huo unafanyika kutokana na kuongozwa na viongozi wa muda mrefu.
Hivyo Jr amesema kuitishwa kwa uchaguzi huo nimapendekezo muhimu ambayo yatatoa mwanga na mwelekeo kupata watendaji wapya ambao watakuwa na jukumu la kuingoza klabu hiyo.
Karsandas amesema fomu za kuwania nafasi katika uchaguzi huo zitaanza kutolewa kuanzia Julai 2 mwaka huu kwenye makao makuu ya klabu hiyo zilizopo barabara 12 jijini Tanga baada ya kikao cha kamati ya utendaji wanachama wao.
Aidha ameweka wazi na kuzitaja nafasi ambazo zitagombewa katika uchaguzi huo kuwa ni nafasi ya mwenyekiti, makamu mwenyekiti, katibu mkuu, katibu msaidizi, mweka hazina na msaidizi wake huku nafasi kumi za wajumbe watakaounda kamati ya utendaji wa klabu hiyo nazo zikiwaniwa.
Hata hivyo amesema kuelekea uchaguzi huo wanatarajiwa kutoa fomu mpya za uanachama kwa wanachama wapya ambao wanataka kujiunga na klabu hiyo ambazo zitatoka kuanzia June 22 mpaka Julai 30 mwaka huu.