Katika taarifa iliyoripotiwa na vyombo vya habari nchini Hispania vimeripoti kuwa wachezaji sita wa timu ya taifa ya Hispania wameibiwa fedha zao katika vyumba walivyofikia katika hoteli moja jijini Recife wakati wanacheza mchezo wao ufunguzi wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Uruguay. Mojawapo ya wachezaji waliokumbwa na zahama hilo ni beki wa Barcelona, Gerard Pique ambaye aligundua kaibiwa wakati aliporejea chumbani kwake baada ya mchezo dhidi ya Uruguay ambao walishinda kwa mabao 2-1. Msemaji wa Shirikisho la Soka Dunia-FIFA, Pekka Odriozola alikiri kupata taarifa hizo lakini wameziachia mamlaka husika kushughulikia na kisha kuwaletea taarifa kamili. Hispania ambao wako kundi B jana wamefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo kwa ushindi mkubwa baada ya kuitandika Tahiti kwa mabao 10-0 wakati wawakilishi pekee wa Afrika kwenye mashindano hayo walishindwa kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Uruguay.