MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Colombia, Radamel Falcao amesema nia yake kubwa ni kuisadia klabu ya Monaco ya Ufaransa kuwa moja ya klabu bora barani Ulaya kwa mara nyingine tena. Akihojiwa baada ya mazoezi na timu yake ya taifa jana Alhamisi Falcao amesema anajisikia fahari kubwa kuwapo Monaco hivyo kutokana na kuvutiwa na mipango waliyokuwa nayo katika kipindi kijacho hivyo mategemeo yao nikuifikisha timu hiyo katika anga za mafanikio. Akiwa Monaco nyota huyo wa zamani wa klabu ya Atletico Madrid ataungana na winga James Rodriguez ambaye pia ni raia wa Colombia baada ya kukubali uhamisho akitokea klabu ya FC Porto. Falcao amesema ana mahusiano mazuri na winga huyo na sio katika soka pekee bali wamekuwa marafiki wa karibu hata nje ya uwanja, na kummwagia sifa kwamba ni mchezaji bora ndio maana Monaco wametumia fedha nyingi kumsajili.