Wednesday, June 12, 2013

SIMBA NA YANGA YAZIWEKEA NGUMU KUSHIRIKI MICHUANO YA KAGAME-SERIKALI


SERIKALI imesisitiza kuwa timu za Simba na Yanga hazitashiriki katika michuano ya klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati maarufu kama kombe la Kagame. Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Amos Makala ametoa taarifa hiyo leo Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Sumve Mheshimiwa Richard Ndasa. Katika swali lake mheshimiwa Ndasa ametaka kujua msimamo wa Serikali juu ya timu za Simba na Yanga kushiriki michuano ya Kagame inayotarajia kuanza Juni 18 hadi Julai 2, mwaka huu huko Sudan Kusini. Akijibu swali hilo mheshimiwa MAKALA amesema kumekuwa na taarifa za hali ya usalama katika Nchi ya Sudan kuwa sio nzuri. Amesema kumekuwa na taarifa kulingana na hali ya usalama nchini Sudan na kwamba Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mheshimiwa Benard Membe tayari amelitolea taarifa na ndani ya Serikali kuna taarifa za kutosha kuwa Sudan hakuna usalama. Amesema msimamo wa Serikali ni kuwa hawawezi kupeleka timu mahali ambapo hakuna usalama.