KAMATI ya Sheria na Hadhi za
Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imepitia usajili wa wachezaji wa
klabu za Ligi Kuu ya Vodacom na kumuidhinisha Mrisho Ngasa kuchezea timu ya Yanga
baada ya kukamilisha usajili wake.
Hata hivyo, Kamati hiyo chini ya
Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa imebaini kuwa Ngasa alisaini mkataba mwingine
Simba (katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam) ambapo anatakiwa
kurejesha fedha alizopokea (sh. milioni 30) pamoja na fidia ya asilimia 50 (sh.
milioni 15) ya fedha hizo kwa Simba.
Kamati pia imemfungia mechi sita za
mashindano (kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii), na anatakiwa awe amelipa fedha
hizo ndani ya kipindi hicho cha kukosa mechi hizo. Akishindwa, hataruhusiwa
kucheza hadi atakapolipa fedha hizo.
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni,
Kamati imeagiza wasiruhusiwe kucheza hadi watakapopata Hati za Uhamisho wa
Kimataifa (ITC) pamoja na vibali vya kufanya kazi nchini (work permits).
Kamati hiyo itakutana tena Ijumaa
(Agosti 23 mwaka huu) ili kupata ripoti za pingamizi ilizoagiza ziwe
zimefanyiwa kazi hadi Agosti 22 mwaka huu na kutoa uamuzi kwa pande ambazo
hazikuafikiana.
Wakati huo huo: Kamati ya TFF kwa
kuzingatia mamlaka iliyonayo katika kifungu cha 10(6) cha Kanuni za Uchaguzi za
TFF inasogeza mbele tarehe ya uchaguzi wa TFF kutoka Oktoba 20 mpaka Oktoba 26
na 27 mwaka huu.
Sababu za kusogeza mbele uchaguzi ni
kutokana na ukweli kuwa Oktoba 20 mwaka huu uongozi wa TFF utakuwa na shughuli
nyingi za maandalizi ya mechi ya Simba na Yanga, na hivyo haitawezekana
kusimamia shughuli za Mkutano Mkuu wa Uchaguzi kwa wakati mmoja na mchezo huo.
Siku ya mwisho ya kampeni itakuwa
Oktoba 25 mwaka huu. Ukiondoa mabadiliko hayo ya tarehe ya uchaguzi wa
viongozi wa TFF, ratiba ya mchakato wa uchaguzi na itabaki kama ilivyotangazwa
na Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika mkutano wake na waandishi wa habari Agosti
24 mwaka huu.
Pia Kamati imeamua kuwa uchaguzi wa
Bodi ya Ligi utabakia kuwa Oktoba 18 mwaka huu kama ilivyopangwa awali.
Kamati imesema inaamini wahusika
wote watapokea vizuri mabadiliko hayo na inasikitika kwa usumbufu
utakaosababishwa na mabadiliko hayo.
|