Mshambuliaji nyota Luis
Suárez leo amerudi kikosini huko Anfield na kuanza Mazoezi tena pamoja na
Kikosi cha Kwanza cha Timu ya Liverpool baada ya kuzuiwa kufanya hivyo
na Meneja Brendan Rodgers kwa kuishambulia Klabu kwa madai ya kuvunja
ahadi ya kumruhusu ahame ikiwa haitafuzu kucheza UEFA CHAMPIONZ LIGI
Msimu huu.
Jumanne iliyopita Suarez alilazimishwa
kufanya Mazoezi peke yake na kutakiwa kuiomba Klabu radhi kwa kauli zake
na inaaminika Mchezaji huyo ametii amri hiyo na ndio maana amerudishwa
tena Mazoezini kwenye Kikosi cha Kwanza.
Suarez amekuwa akisinikiza kuihama
Liverpool na Arsenal ilishatoa Ofa ya Pauni 40,000,001 kumnunua lakini
Liverpool imekataa na kusisitiza Mchezaji huyo hauzwi.
Msimamo huo ulisisitizwa zaidi na
Mmiliki mkuu wa Liverpool kutoka Marekani, John W Henry, ambae Wiki
iliyopita alitamka Suarez hatauzwa kwa Arsenal au kwa Klabu yeyote
Ulaya.
Kwa sasa Suarez yupo kwenye Kifungo cha
Mechi 10 alichopewa mwishoni mwa Msimu uliokwisha Mwezi Mei kwa
kumng’ata meno Beki wa Chelsea Branislav Ivanovic kwenye Mechi na tayari
ameshatumuikia Mechi 4 na bado 6.
Wakati huo huo, Liverpool imefanikiwa
kukubaliana na Klabu ya Spain, Valencia, ili kumchukua Beki wao wa
kushoto Aly Cissokho kwa Mkopo wa Msimu mmoja.
Meneja wa Liverpool Brendan Rodgers
alikuwa akisaka Mchezaji wa pozisheni hiyo ili kuleta ushindani kwa Beki
wake José Enrique na waliwahi kuwawania Lorenzo Melgarejo wa Benfica na
Guilherme Siqueira wa Granada ili kujaza Nafasi hiyo.