MABINGWA wa ligi kuu msimu uliopita YANGA SC wameingia kambini makao makuu
ya klabu yao, Jangwani, Dar es Salaam maarufu kama Jangwani City kujiandaa na
mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC Jumamosi, Uwanja wa Taifa,
Jijini.
Wakati mabingwa hao wa Ligi Kuu,
wakiingia kambini Jangwani, wapinzani wao Azam FC waliorejea jana kutoka Afrika
Kusini walipoweka kambi ya takriban wiki mbili, wamefikia kwenye makao yao
makuu, Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mchezo huo wa kuashiria kufungua pazia
la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara umeteka hisia za wengi na
kila timu inaonekana kupania kushinda ili kuwasha taa za kijani kuelekea mbio
za ubingwa.
Yanga iliifunga Azam FC katika mechi
zote tatu za msimu uliopita walizokutana, hivyo kulipa kisasi cha kufungwa na
timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa mara nne msimu uliotangulia
katika mashindano yote waliyokutana.
Katika kujiandaa na msimu, Yanga SC
walicheza mechi saba na kushinda tatu, kufungwa moja na sare tatu.
Walizifunga Mtibwa Sugar 3-1, SC Villa
ya Uganda 4-1 na 3Pillars ya Nigeria 1-0, na kutoa sare ya 1-1 na Express, 2-2
na URA zote za Uganda na 0-0 na Rhino FC mjini Tabora, wakati walifungwa 2-1 na
Express ya mjini Shinyanga.
Kwa upande wa washindi wa pili wa Ligi
Kuu, Azam kabla ya kwenda Afrika Kusini walicheza mechi nne na kushinda tatu,
1-0 na komabini ya JKT, 4-0 na African Lyon na 5-1 Ashanti United. Azam pia
ilicheza mechi tatu na kikosi chake cha pili, Azam Akademi na kushinda zote,
1-0 mara mbili na 2-1 mara moja.
Na ikiwa Afrika Kusini, ilicheza mechi
nne na kufungwa tatu na kushinda moja- ilifungwa 3-0 na Kaizer Chiefs, 2-1 na
Orlando Pirates na 1-0 na Moroka Swallows, wakati yenyewe ilishinda 1-0 dhidi
ya Mamelodi Sundowns.
|
|
|
|