KIUNGO Mahiri wa klabu ya AC
Milan ya Italia, Kaka amebainisha kuwa Lionel Messi na Zinedine Zidane
ni wachezaji bora aliokutana nao na kudai kuwa Cristiano Ronaldo ndio
mchezaji bora kabisa kuwahi kucheza naye. Kiungo huyo wa kimataifa wa
Brazil, amewahi kukutana na Messi mara kadhaa wakati akicheza Real
Madrid ambako alikuwa akicheza sambamba na Ronaldo. Kaka aliandika
katika ukurasa rasmi wa twitter wa Milan wakati akijibu maswali ya
mashabiki ambapo amesema wachezaji bora aliowahi kucheza dhidi yao ni
Zidane na Messi huku akimtaja Ronaldo kama mchezaji bora aliyewahi
kucheza naye. Kaka pia alimtaja Paulo Maldini kama beki bora kabisa
duniani kuwahi kucheza naye kabla hajaondoka Milan kwenda Madrid.