MENEJA wa klabu ya AC
Milan, Clerence Seedorf amedai kuwa klabu hiyo inaendelea kuimarika
pamoja na kupata sare ya kufungana mabao 1-1 na Torino katika mchezo wa
Serie A uliofanyika jana. Katika mchezo huo uliofanyika katika Uwanja wa
San Siro wageni Torino ndio walioanza kupata bao kipindi cha kwanza
kupitia kwa Ciro Immobile lakini wenyeji walirudisha bao hilo katika
kipindi cha pili kupitia kwa Adil Rami. Sare hiyo inaonekana
kumfurahisha Seedorf ambaye anadai kuwa wachezaji wake wameanza kuzoea
mfumo anaofundisha. Seedorf amesema ni jambo jema kuona kikosi chake
kikianza kuelewana taratibu na kudai kuwa ni dalili nzuri za kufanya
vyema huko mbele. Sare hiyo imeiacha Milan katika nafasi ya tisa ya
Serie A, wakiwa wanajikongoja toka alipotimuliwa kocha Massimiliano
Allegri Januari mwaka huu.