Wednesday, May 7, 2014

KINDA ANAEKIPIGA UJERUMANI AOMBA KUITWA STARS

Mwanandinga Kinda anayekipiga barani ulaya soka ya kulipwa Ujerumani, Charles Mishetto ameomba kuitwa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars aisaidie katika kampeni za kuing’oa Zimbabwe.
Hatua hiyo inakuja baada ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuikubalia TP Mazembe ya DRC ambayo imegoma kuwaachia Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu kuitumikia Taifa Stars katika mechi ya kuwania kushiriki fainali zijazo za Afrika (AFCON) dhidi ya Zimbabwe.
FIFA imesema klabu hazitashurutishwa kuwaachilia wachezaji wao ili washiriki mechi za kufuzu kwa michuano hiyo itakayofanyika Morocco mwakani, kwa sababu ipo nje kalenda ya mechi za shirikisho hilo.
Boniface Wambura, Ofisa Habari na Mwasiliano wa  TFF amesema kuwa wawili hao hawatakuwamo kwenye kikosi cha kovha
mpya Mholanzi Mart Nooij kitakachoivaa Zimbabwe mwishoni mwa wiki ijayo kwa vile wanahitajika kwenye klabu yao.
Mechi za kuwania kufuzu AFCON zitafanyika Mei 16-18, tarehe ambayo haipo kwenye ratiba ya FIFA na kwa hivyo haitakuwa lazima wachezaji wa klabu kuruhusiwa kuondoka.
Hata hivyo, michuano ya makundi itakayoshirikisha Ghana, Nigeria na Cameroon, zitakuwa katika tarehe iliyoidhinishwa na FIFA , ikimaanisha kuwa klabu vya soka kote duniani lazima ziwaruhusu wachezaji wao kushiriki mechi hizo.
Mbali na Samata na Ulimwengu, wachezaji kama Edward Sadomba, wataathiriwa na mgongano wa tarehe zilizo kati ya mechi za kufuzu zitakazofanyika 2015 na michuano ya klabu. Sadomba atahitajika kwa wakati mmoja na klabu yake ya Al Ahli Benghazi pamoja na timu yake ya taifa Zimbabwe itakayokipiga dhidi ya Taifa Stars.
Lakini FIFA lilikaririwa na BBC juzi likieleza kuwa wachezaji wanaweza tu kuondoka ikiwa maafisa wa klabu na mashirikisho ya nchi husika wanaweza kukubaliana.