Wednesday, May 7, 2014

MAMBO YAIVA,RAIS MPYA SIMBA SC KUPATIKANA JUNI 29

Kamati ya uchaguzi ya Simba imepanga uchaguzi mkuu wa klabu hiyo kufanyika juni 29 mwaka huu baada ya msajili wa vyama vya michezo na klabu kuipitisha katiba yao iliyofanyiwa marekebisho.
DSC_0027 Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Simba yalipopo mtaa wa Msimbazi Kariakoo, jijini Dar es salaam leo mchana, mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Simba sc, mwanasheria na wakala wa wachezaji wa FIFA, Dkt. Damas Ndumbaro amesema kamati yake imekutana jana na kuamua tarehe hiyo ya uchaguzi ili kupata rais mpya, makamu wa rais na wajumbe wapya wa kamati ya utendaji.
“Kamati yangu ina watu makini na wenye uadilifu mkubwa. Pia wana mawazo ya kuijenga klabu ya Simba”.
“Jana tulikutana na kupanga ratiba ya uchaguzi. Hatutakuwa na huruma na watu watakaoenda kinyume na kanuni za uchaguzi”. Alisema Ndumbaro.

Ndumbaro alisema kuanzia mei 9 mwaka huu mchakato wa kuanza kutoa fomu kwa watu wenye nia ya kuwania nafasi za uongozi utaanza rasmi, na siku ya kurudisha fomu ni mei 14 mwaka huu.