Thursday, May 15, 2014

TFF YASAINI MKATABA UDHAMINI SOKA LA WANAWAKE

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) hapa nchini limeendeleza kutunisha msuli baada ya jana kusaini mkataba na kampuni ya proin Promotions kwa ajili ya kudhamini mashindano ya Kombe la Taifa kwa wanawake yatakayofanyika kati ya mwezi Septemba na Oktoba mwaka huu.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, Johnson Rukaza, alisema kuwa makubaliano hayo waliyoingia na TFF yatakuwa ni ya miaka miwili na yatawagharimu zaidi ya Sh.
 milioni 150 ili kufanikisha michuano hiyoRukaza alisema kuwa kupitia mashindano hayo ya Kombe la Taifa wanaamini vipaji vya wachezaji wanawake vitaonekana na baadaye kuisaidia timu ya Taifa ya jinsia hiyo (Twiga Stars) kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ambayo inashiriki.
Amesema kwamba wao wamefungua njia kudhamini mashindano hayo na wanawaomba makampuni na taasisi nyingine kujitokeza kudhamini mashindano hayo ikiwamo na vituo vya televisheni lengo likiwa ni kutangaza soka la wanawake.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi, alisema kuwa uongozi wake unawashukuru wadhamini hao wapya na inaahidi uongozi wake utahakikisha soka la wanawake linasonga mbele.
Malinzi amesema kwamba wanawaomba wazazi na walezi kuwaruhusu watoto wa kike kushiriki mchezo huo kwa sababu utawasaidia kiafya, kupata burudani na kuinua hali zao za kichumi pale watakapofanikiwa kupata klabu za kucheza.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake Tanzania (TWFA), Lina Kessy, alisema kwamba wanaamini sasa mpira wa wanawake utacheza na jana ilikuwa ni siku ya kihistoria kwenye medani ya mchezo huo kwa upande wa wanawake.
Kessy amesema kwamba TFF na TWFA itahakikisha jitihada za kusaka wadau wengine zinaendelea ili mchezo huo uchezwe sehemu zote hapa nchini.
Amesema kwamba zaidi ya mikoa 17 inatarajiwa kushiriki mashindano hayo ambayo mara ya mwisho yalifanyika mwaka 2008.