
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limelitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuanza upya mchakato wa uchaguzi baada ya kubaini kasoro iliyotokana na ukosefu wa kutokuwepo vyombo vya kushughulikia ukiukwaji wa maadili. FIFA ambayo ilituma ujumbe wake katikati ya mwezi uliopita kufanya utafiti kuhusu mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa TFF ambao ulisimamishwa baada ya baadhi ya wagombea kulalamika, imetaka uchaguzi ufanyike kabla ya tarehe 30 Oktoba 2013, lakini ukitanguliwa na mabadiliko ya katiba ambayo yatahusisha uundwaji wa vyombo vya kushughulikia ukiukwaji wa maadili. Rais wa TFF, Leodegar Tenga aliwaambia waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa shirikisho hilo kuwa suala la Tanzania lilijadiliwa kwenye kikao cha Kamati ya Dharura ya FIFA kilichofanyika tarehe 28 Aprili 2013 na maamuzi yake kutumwa juzi kwa barua iliyosainiwa na KatibuMkuuwa FIFA, Jerome Valcke. Baada ya kupokea barua hiyo, Rais wa TFF alifunga safari kwenda Dodoma jana kukutana na Mheshimiwa Waziri na Naibu wake pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT). “Matarajio yetu sote yalikuwa kupokea majina ya waliopitishwa ili tufanye uchaguzi. Kinyume chake tumepokea maagizo hayo. Hata hivyo tumeona kuwa hili ni jambo la kheri kwa vile siyo tu haki itatendeka bali pia itaonekana imetendeka.” alisema Tenga, ambaye alishatangaza kuwa hatagombea tena urais baada ya kuliongoza Shirikisho kwa vipindi viwili vya miaka minne kila kimoja. “Lengo letu ni kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa na uchaguzi kufanyika mapema iwezekanvyo kabla ya tarehe iliyotolewa. Yale mambo nayoweza kufanyika kwa pamoja yatafanyika ili tuharakishe utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na FIFA." Uchaguzi wa TFF ulipangwa kufanyik tarehe 23 na 24 Februari 2013 na ulikuwa ukielekea ukingoni, lakini baadhi ya wagombea walienguliwa katika hatua ya mwisho na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF na ndipo walipo andika barua FIFA kuomba iingilie kati. Rais Tenga alisema kuwa ujumbe wa FIFA ulikutana na pande zote zilizoathiriwa na mchakato wa uchaguzi na kwamba baada ya kukusanya taarifa hizo, maagizohayo ya FIFA sasa yatakuwa ni suluhisho la matatizo ya muda mrefu katika uendeshaji wa mpira wa miguu nchini.
Katika barua hiyo, FIFA imeiagizaTFF:
1. Kuunda vyombo sahihi (Kamati ya Maadili itakayokuwa na vyombo viwili ambavyo ni cha kutoa maamuzi ya awali na cha rufaa) ambavyo mamlaka yake yatakuwa ni kushughulikia masuala ya ukiukwaji wa maadili;
2. Kufanya mabadiliko ya katiba kwa kuzingatia uundwaji wa vyombo hivyo;
3. Kuanza upya kwa mchakato wa uchaguzi wa Kamati ya Utendaji kwa kufungua milango kwa wagombea ambao walishachukua fomu na wagombea wapya:
4. Shughuli hiyo ikamilike ifikapo tarehe 30 Oktoba 2013.
Katika kutekeleza hayo, TFF inatakiwa iitishe Mkutano Mkuu wa Dharura kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya kuunda kamati hizo za maadili na Kanuni za Uchaguzi kabla ya kuendelea na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Kamati Mpya ya Utendaji.
Katika maoni yake FIFA imeeleza kuwa katika mchakato, Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliwaengua au kupitisha baadhi ya wagombea kwa kubaini kuwa walikiuka Ibara ya 9 (7) ya Kanuni za Uchaguzi na pia Ibaray a 29 (7) ya Katiba ya TFF ambavyo vinahusisha suala la kufungua kesi mahakamani, kufuja fedha za shirikisho na ukosefu wa uwajibikaji wa pamoja.
Hata hivyo, FIFA ilisema kuwa watu hao walitakiwa waadhibiwe kwanza na kamati husika (kamati za maadili) kabla ya kuenguliwa na kamati za uchaguzi za TFF.
Kutokana na ukosefu wa kamati za maadili matokeo yake, mmoja wa wagombea amekuwa akienguliwa kwenye uchaguzi kila anapombea bila ya kujua adhabu yake ni ya muda gani,” inasema barua hiyo ya FIFA.
Rais Tenga ameagiza kuitishwa kwa kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya TFF kupokea maagizo ya FIFA na kupanga ratiba ya utekelezaji wake kwa lengo la kuhakikisha kuwa mchakato huu unatekelezwa mapema iwezekanavyo.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mei 1, 2013
MIKOA 18 YAPATA MABINGWA WA MIKOA
Mikoa 18 kati ya 27 ya kimpira tayari imeshapata mabingwa wao kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa itakayoanza Mei 12 mwaka huu chini ya usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Timu tatu za juu katika Ligi hiyo ya Mabingwa zitapanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao (2013/2014). Ligi ya FDL ina jumla ya timu 24 ambapo tatu katika ligi hiyo zilizoshuka daraja msimu huu ni Moro United ya Dar es Salaam, Small Kids ya Rukwa na Morani FC ya Manyara.
Mabingwa waliopatikana hadi sasa na mikoa yao kwenye mabano ni Abajalo SC (Dar es Salaam 2), Biharamulo FC (Kagera), Flamingo SC (Arusha), Friends Rangers (Dar es Salaam 3), Katavi Warriors (Katavi), Kiluvya United (Pwani), Kimondo FC (Mbeya) na Machava FC (Kilimanjaro).
Wengine ni Magic Pressure FC (Singida), Mbinga United (Ruvuma), Mji Njombe (Njombe), Polisi Jamii Bunda FC (Mara), Red Coast FC (Dar es Salaam 1), Rukwa United (Rukwa), Saigon FC (Kigoma), TECKFOLT FC ya Kilombero ambayo ni Shule ya Sekondari (Morogoro) na UDC FC ya Ukerewe (Mwanza).
Kila klabu inatakiwa kulipa ada ya ushiriki ambayo ni sh. 100,000 wakati usajili wa wachezaji wa timu hizo ni uleule uliofanyika katika Ligi ya Mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa ajili ya uthibitisho. TFF inapenda kusisitiza kuwa hakuna usajili mpya wa wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo.
MTANZANIA AOMBEWA ITC ACHEZE NORWAY
Shirikisho la Mpira wa Miguu Norway (NFF) limetuma maombi ya kupatiwa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa mchezaji Mtanzania Godfrey Mlowoka ili aweze kucheza mpira nchini humo.
NFF inamuombea hati hiyo Mlowoka ili aweze kujiunga na klabu ya Ekne IL kama mchezaji wa ridhaa ambapo klabu yake ya zamani aliyokuwa akiichezea nchini imetajwa kuwa Sadani.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linafanyia kazi maombi hayo na mara taratibu zote zitakapokamilika hati hiyo ya uhamisho itatumwa nchini Norway.
AZAM YAENDELEA KUJINOA MOROCCO
Timu ya Azam ambayo iko jijini Rabat kwa ajili ya mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabati ya huko inaendelea vizuri na mazoezi.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari Msaidizi wa Azam FC, Jaffer Idd maandalizi yanakwenda vizuri kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa Jumamosi (Mei 4 mwaka huu). Jaffer Idd anapatikana kwa namba +212671146092.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)