Friday, June 21, 2013

NAE DAVID LUHENDE APATA NAFASI AONGEZWA KATIKA KIKOSI CHA TAIFA STARS.


BEKI wa Yanga, David Luhende ameongezwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Uganda (The Cranes) kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Kocha Kim Poulsen amesema kutokana na uamuzi huo wa kumuongeza beki huyo wa kushoto amemuondoa mchezaji mmoja kwenye kikosi chake. Mchezaji huyo ni mshambuliaji Zahoro Pazi wa JKT Ruvu.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager sasa itaingia kambini kwenye hoteli ya Tansoma jijini Dar es Salaam, Julai 3 mwaka huu badala ya Julai 4 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali.

Mechi ya Uganda itachezwa Julai 13 mwaka huu, saa 9 kamili alasiri kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati ile ya marudiano itachezwa wiki mbili baadaye jijini Kampala, Uganda.

Wachezaji wanaotakiwa kambini ni Aggrey Morris (Azam), Aishi Manula (Azam), Ally Mustafa (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruni Chanongo (Simba), John Bocco (Azam), Juma Kaseja (Simba), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar) na Kelvin Yondani (Yanga).

Wengine ni Khamis Mcha (Azam), Mrisho Ngasa (Simba), Mudathiri Yahya (Azam), Mwadini Ali (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Nadir Haroub (Yanga), Salum Abubakar (Azam), Shomari Kapombe (Simba), Simon Msuva (Yanga) na Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar).
TIMU NNE KUCHEZA NUSU FAINALI RCL
Timu nne zimefuzu kucheza hatua ya nne (nusu fainali) ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) baada ya kushinda mechi zao za hatua ya tatu ya michuano hiyo itakayotoa washindi watatu watakaocheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao.
Katika hatua hiyo Polisi Jamii ya Mara itaikaribisha Kimondo SC ya Mbeya kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma wakati Stand United FC ya Shinyanga itakuwa mgeni wa Friends Rangers ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Azam Chamazi.

Mechi za kwanza zitachezwa Juni 23 mwaka huu wakati zile za marudiano zitafanyika kwenye viwanja vya Sokoine jijini Mbeya na Kambarage mjini Shinyanga, Juni 30 mwaka huu.

Kwenye hatua ya tatu ya RCL, Friends Rangers iliing’oa Kariakoo ya Lindi kwa jumla ya mabao 2-0, Stand United FC ikaitoa Machava FC ya Kilimanjaro kwa mabao 2-1, Kimondo SC ikaishinda Njombe Mji mabao 6-5 wakati Polisi Jamii iliitambia Katavi Warriors kwa mabao 7-6.

Hatua ya mwisho ya ligi hiyo itachezwa Julai 3 mwaka huu kwa mechi za kwanza wakati zile za marudiano zitakuwa Julai 7 mwaka huu.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

AFRICAN SPORT WAJIPANGA NA UCHAGUZI WA VIONGOZI WAPYA.


African Sports  Mabingwa wa Kombe la Jamhuri mnamo mwaka 1988 maarufu Wanakimanumanu" wanatarajiwa kufanya mkutano mkuu wa uchaguzi Agosti 15 mwaka huu baada ya uongozi wa muda uliopo madarakani kumaliza wakati wake.
Akizungumza na mkali wa dimba Msemaji wa Club hiyo Said Karsandas Junior ametanabisha kuwa uchaguzi huo unafanyika kutokana na kuongozwa na viongozi wa muda mrefu.
Hivyo Jr amesema kuitishwa kwa uchaguzi huo nimapendekezo muhimu ambayo yatatoa mwanga na mwelekeo kupata watendaji wapya ambao watakuwa na jukumu la kuingoza klabu hiyo.
Karsandas amesema fomu za kuwania nafasi katika uchaguzi huo zitaanza kutolewa kuanzia Julai 2 mwaka huu kwenye makao makuu ya klabu hiyo zilizopo barabara 12 jijini Tanga baada ya kikao cha kamati ya utendaji wanachama wao.
Aidha ameweka wazi na kuzitaja nafasi ambazo zitagombewa katika uchaguzi huo kuwa ni nafasi ya mwenyekiti, makamu mwenyekiti, katibu mkuu, katibu msaidizi, mweka hazina na msaidizi wake huku nafasi kumi za wajumbe watakaounda kamati ya utendaji wa klabu hiyo nazo zikiwaniwa.
Hata hivyo amesema kuelekea uchaguzi huo wanatarajiwa kutoa fomu mpya za uanachama kwa wanachama wapya ambao wanataka kujiunga na klabu hiyo ambazo zitatoka kuanzia June 22 mpaka Julai 30 mwaka huu.

JE? WAJUA NANI ZAIDI KATIKA UFUNGAJI MSIMU ULIPITA TAFAKARI"".

KATIKA Kabumbu /Soka/ Kandanda kila timu huwa kuna wachezaji ambao kazi yao ni kufunga mabao. Timu inapokosa wafunga mabao makini huyumba kwa asilimia kubwa Hivyo mkali wa dimba tz.blogspo inakupa wafungaji walitikisa msimu uliopita ambapo??
Katika msimu uliopita, kulikuwa na wafungaji kadhaa ambao walitikisa, lakini nyota wa Hispania katika ligi ya BBVA LA LIGA ndio walionyesha umahiri zaidi.
Wafuatano ni nyota watano ambao ndiyo wakali wa kutikisa nyavu Ulaya. Nyota watatu kati yao ni kutoka Ligi Kuu Hispania.
1. Lionel Messi (Barcelona)
Mabao 46 katika mechi 32 za ligi. Huyu ameonyesha uwezo na umwamba mkubwa kwa kuwapita wachezaji wengine wa Ulaya kwa mabao zaidi ya 12.





2. Cristiano Ronaldo (Real Madrid)
Mabao 34 katika mechi 34 za ligi. Mchezaji huyo ana wastani wa kufunga bao moja kwenye kila mechi ya Ligi Kuu Hispania msimu uliomalizika.
Amefunga jumla ya mabao 146 kwenye mechi 135 za ligi tangu alipotua kwenye kikosi cha Real Madrid mwaka 2009.
hivyo kila mtu anafahamu kabisa kuwa Ronald ndie mpinzani mkuu wa messi ambapo tokea alipotua Madrid ameonyesha upinzani mkubwa kwa messi lakini bado alionekana kuwa nyuma ya messi katika kutupia mabao.

3. Radamel Falcao (Atletico Madrid)
Mabao 28 katika mechi 33 za ligi. Nyota huyo raia wa Colombia, ameisaidia timu yake kushika nafasi ya tatu msimu huu.Hakufanya vizuri kwenye ligi kuu pekee, bali pia kwenye mechi za Super Cup na Europa League ambapo alifunga mabao sita kwenye michuano hiyo mikubwa .Ni mmoja kati ya wachezaji wanaosakwa mno. Chelsea ndio klabu inayomwania kwa karibu kwa kuwa Jose Mourinho  amerudi Stamford, huenda akamnasa kirahisi.
4. Edinson Cavani (Napoli)
Mabao 28 katika mechi 33 za ligi. Mbinu, kasi, maarifa na nguvu ndio mambo yanayomfanya nyota huyo asakwe na klabu kubwa za Ulaya msimu huu.
Huenda akasajiliwa na Man City au Chelsea kwani ndio timu zilizo mstari wa mbele kuwania saini yake.Hata hivyo Napoli imesema kuwa haiwezi kumuuza kwa chini ya Pauni 50 milioni.

5. Zlatan Ibrahimovic (PSG)
Mabao 27 katika mechi 32 za ligi. Mchezaji huyo raia wa Sweden amekuwa na kiwango kizuri tangu alipohamia PSG akitokea AC Milan katika msimu wa usajili wa majira ya joto mwaka jana.Amevunja rekodi na kuwa nyota wa kwanza kufunga mabao mengi kwenye Ligi Kuu Ufaransa mbele ya Jean-Pierre Papin ambaye alijitahidi kufanya vizuri mwaka 1992.Mabao hayo yamemfanya Zlatan awanie tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu uliopita.

PIRLO KUIKOSA BRAZIL KOMBE LA MABARA KUNDI" A"

KIUNGO mkongwe na mahiri wa kimataifa wa Italia, Andrea Pirlo anatarajiwa kukosa mchezo wa mwisho wa kundi A dhidi ya wenyeji Brazil kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho "Kombe la Mabara" baada ya kupata majeraha ya msuli katika mguu wake wa kulia. Kocha wa viungo wa nchi hiyo. 
Aidha Enrico Castellacci amesema anamatumaini Pirlo anaweza kurejea katika mechi ya nusu fainali lakini ukijumuisha na kukosekana kwa Daniele De Rossi ambaye naye pia atakosa mchezo wa mwishoni itabidi kocha wa timu hiyo Cesar Prandelli abadili kikosi chake. Italia ilitinga hatua ya nusu fainali baada ya kuibugiza Japan ka mabao 4-3 na kufikisha alama sawa na Brazil katika kundi lao ambapo mechi ya mwisho ndio itakayoamua nani atasonga mbele kama mshindi wa kundi. Timu zote mbili itabidi zipange vikosi vyao kamili ili kutafuta ushindi na kuepuka kukutana na bingwa wa dunia Hispania katika hatua ya nusu fainali.

NANI ZAIDI KESHO RED'S MISS TANGA 2013 MKWAKWANI.

Kesho ndio Kesho  Juni 22,2013 Katika Uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga utakutanisha walimbwende washindano la Miss Tanga 2013 litakalo fanyika katika uwanja huu.
Wakizungumza na mkali wa dimba mkaoni hapa baadhi ya walimbwende hao wamesema wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanakonga Nyoyo za wadau mbalimbali  watakao jitokeza katika kushuhudia mvutano huo.
Aidha mamiss hao walikuwa katika ziara ya Makamu wa Rais, Dk Mohammed Ghalib Bilal kuzindua mradi wa uwekezaji wa viwanda katika eneo pongwe jijini hapamapema leo asubuhi.  Katika uzinduzi huo awali Rais Dk. Jakaya Kikwete ndiye aliyetarajiwa kuja kuzindua mradi huo, lakini badala yake amekuja Dk Bilal. 
Hivyo katika shindano hilo mshindi wa kwanza anatarajiwa kujinyakulia kitita cha sh.laki tano 500,000 huku msanii wa muziki wa kizazi kipya, Tunda Man, akiongoza kwa upande wa Burudani, katika shindano litakalofanyika Jumamosi katika uwanja wa Mkwakwani.
Akizungumza na mkali wa dimba jijini hapa Mkurugenzi wa Kampuni ya DATK Intertainment Asha Kigundula,amesema kuwa maandalizi ya shindano hilo yapo vizuri kwa asilimia 100% ambapo zawadi kwa mshindi wa pili atajinyakulia kitita cha shilingi 300,000.
Mshindi wa tatu atazawadiwa kitita cha shilingi  250, 000 wakati mshindi wa nne na tano wakipata sh.200, 000 kila mmoja na warembo wengine watakaosalia watapata kitita cha sh.laki moja moja kila mmoja 100,000 kama kifuta jasho pamoja na zawadi kwa mrembo mwenye nidhamu ili kuweza kuboresha shindano hilo.
Kwa upande wa Burudani msanii wa kizazi kipya, Tunda Man, ataongoza safu ya burudani, ambapo itakuwa na wasanii mbalimbali wakiwemo Dr John, Nabisha kutoka kundi la THT, Fady Dady na wasanii chipukizi kutoka mkoani hapa.

Warembo hao ni Hawa Ramadhani (18),Hazina Mbaga (19)Like Abdulraman (19), Irene Thomas(20), Tatu Athumani (19), Winfrida Gutram (21)Lulu Mbonela (19) ,Hazina Daniel (19),Lulu Matawalo(22),Judithi Moleli (21),Neema Jonas na Hawa Twaybu(21)

Wakati huo huo Warembo hao wanaowania Taji la Mlimbwende wameiomba Halmashuri ya Jiji la Tanga kuifanyia marekebisho barabara inayokwenda katika mapango ya Amboni ili iweza kuwa nzuri na ipitike kirahisi nyakati zote.

MIAMI HEAT YATWAA TAJI LA PILI LIGI YA NBA-MAREKANI"

 TIMU ya mpira wa kikapu Miami Heat imefanikiwa kutwaa taji la pili mfululizo la Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani-NBA baada ya kuibamiza timu ya San Antonio Spurs kwa vikapu 95-88 katika fainali ya saba iliyofanyika katika Uwanja wa American Airlines uliopo jijini Miami, Florida. San Antonio walibakiza kidogo kulinyakuwa taji hilo Jumanne kabla ya Miami kupambana na kushinda hivyo kuzifanya timu hizo kutoka sare ya kufunga 3-3 katika fainali ya sita kati ya saba ambazo wanatakiwa kucheza. 
Katika mchezo wa Alfajiri kuamkia leo nyota wa timu ya Heat, LeBron James mwenye umri wa miaka 28 alifanikiwa kuisadia vyema timu yake kwa kufunga vikapu 37 na kutajwa kuwa mchezaji mwenye thamani zaidi katika ligi hiyo kwa mara ya pili mfululizo. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo James ambaye aliingia matatani baada ya kudaiwa kucheza chini ya kiwango katika mechi muhimu amesema anajisikia fahari kunyakuwa taji hilo katika uwanja wao wa nyumbani na yote yaliyopita yanabaki kuwa historia.

WANANDINGA WA HISPAIN WAPORWA HOTELI-BRAZIL

Katika taarifa iliyoripotiwa na vyombo vya habari nchini Hispania vimeripoti kuwa wachezaji sita wa timu ya taifa ya Hispania wameibiwa fedha zao katika vyumba walivyofikia katika hoteli moja jijini Recife wakati wanacheza mchezo wao ufunguzi wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Uruguay. Mojawapo ya wachezaji waliokumbwa na zahama hilo ni beki wa Barcelona, Gerard Pique ambaye aligundua kaibiwa wakati aliporejea chumbani kwake baada ya mchezo dhidi ya Uruguay ambao walishinda kwa mabao 2-1. Msemaji wa Shirikisho la Soka Dunia-FIFA, Pekka Odriozola alikiri kupata taarifa hizo lakini wameziachia mamlaka husika kushughulikia na kisha kuwaletea taarifa kamili. Hispania ambao wako kundi B jana wamefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo kwa ushindi mkubwa baada ya kuitandika Tahiti kwa mabao 10-0 wakati wawakilishi pekee wa Afrika kwenye mashindano hayo walishindwa kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Uruguay.