Thursday, August 15, 2013

YANGA, AZAM KUVAANA NGAO YA JAMII J’MOSI

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom, Yanga na makamu bingwa Azam wanavaana keshokutwa (Jumamosi) kwenye mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kuashiria uzinduzi wa msimu mpya wa 2013/2014.

Mechi hiyo inayotarajiwa kuwa kivutio kwa wapenzi wa mpira wa miguu nchini itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni ambapo mshindi atakabidhiwa ngao.


Iwapo dakika 90 za mechi hiyo hazitatoa mshindi, timu hizo zitatenganishwa kwa mikwaju ya penalti huku asilimia 10 ya mapato ya mechi hiyo yakienda kwa kituo cha kulelea watoto cha SOS.


Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 7,000 kwa viti vya rangi ya kijani na bluu wakati viti vya rangi ya chungwa ni sh. 10,000. Watakaiongia viti vya VIP C watalipa sh. 15,000, viti vya VIP B ni sh. 20,000 wakati VIP A watalipa sh. 30,000.

LIGI DARAJA LA KWANZA KUANZA SEPT 14

Michuano ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoshirikisha timu 24 zilizogawanywa katika makundi matatu msimu huu (2013/2014) itaanza kutimua vumbi Septemba 14 mwaka huu.


Kila timu itakayoongoza kundi lake katika ligi itakayochezwa kwa mikondo miwili (nyumbani na ugenini) ndiyo itakayopanda daraja kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2014/2015.


Mechi za ufunguzi kwa kundi A zitakuwa kati ya Tessema vs Green Warriors (Uwanja wa Karume, Dar es Salaam) wakati Septemba 15 mwaka huu ni Transit Camp vs Polisi Dar (Uwanja wa Mabatini, Pwani), Ndanda vs Friends Rangers (Uwanja wa Nangwanda, Mtwara) wakati Villa Squad vs African Lyon itachezwa Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.


Kundi B ni Burkina Faso vs Polisi Moro (Uwanja wa Jamhuri, Morogoro), Mkamba Rangers vs Lipuli (Uwanja wa CCM Mkamba, Morogoro), Majimaji vs Mlale JKT (Uwanja wa Majimaji, Songea) wakati Septemba 15 mwaka huu Kimondo SC vs Kurugenzi (Uwanja wa Sokoine, Mbeya).


Mechi za ufunguzi kundi C ni Polisi Mara vs Polisi Dodoma (Uwanja wa Karume, Musoma), Kanembwa JKT vs Polisi Tabora (Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma), Stand United vs Mwadui (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga), na Pamba vs Toto Africans (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza).


Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo utamalizika Oktoba 26 mwaka huu wakati wa pili utamalizika Machi 22 mwakani. (Ratiba imeambatanishwa)


Boniface Wambura

Ofisa Habari

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

RIBERY AWAHI KUFIKIRIA KUICHEZEA BARCELONA PAMOJA NA REAL MADRID"

Winga wa club ya Bayern Munich, Franck Ribery amekiri kuwahi kufikiria kuihama klabu hiyo na kwenda Barcelona katika kipindi cha majira ya kiangazi mwaka 2009 lakini aliamua kuheshimu mkataba wake na kubakia. Winga huyo wa kimataifa wa Ufaransa pia alikuwa akihusishwa na kutaka kusajiliwa na Real Madrid miaka michache iliyopita lakini sasa ameweka wazi kuwa Madrid sio klabu pekee iliyokuwa ikimhitaji nchini Hispania. 

Ribery amedai kuwa mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya Ufaransa, Eric Abidal ambaye alikuwa akicheza chini ya Pep Guardiola akiwa Barcelona alimfuata na kumwambia suala hilo katika msimu wa 2008-2009. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 alikiri kufikiria kujiunga na klabu hiyo kwa kipindi hicho kwasababu walikuwa na kikosi bora duniani. Ribery aliendelea kudai kuwa alikuwa katika kipindi kigumu kufanya uchaguzi lakini kwasababu ya umuhimu wa Karl-Heinz Rummenigge na Uli Hoeness ambaye ndiye rais wa klabu hiyo kwake aliamua kuheshimu mkataba wake na kutulia.

Wednesday, August 14, 2013

SUAREZ AJA NA MTAZAMO MPYA KUHUSU KUBAKIA LIVERPOOL

Mshambuliaji mahiri wa club ya Liverpool, Luis Suarez amebadili mawazo kuhusu mustakabali wake na kusisitiza kuwa ameamua kubakia Anfield. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uruguay amekuwa akitaka kuondoka Uingereza kutokana na kuchoshwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo lakini Liverpool walikuwa hawako tayari kumuachia nyota huyo. Arsenal ambao ushiriki wao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ulionyesha kumvutia Suarez, walijitahidi kujaribu kumsajili nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 kwa kutoa ofa ya paundi milioni 42 ambayo ingevunja rekodi yao ya usajili lakini walikataliwa. Akihojiwa jijini Tokyo akiwa katika majukumu ya timu yake ya taifa, Suarez amebainisha kuwa ameamua kubakia kwa ajili ya mashabiki wa klabu hiyo ambao wameonyesha mapenzi makubwa kwake.

YANGA YAINGIA KAMBINI KUJINOA DHIDI YA AZAM NGAO YA JAMII



MABINGWA wa ligi kuu msimu uliopita  YANGA SC wameingia kambini makao makuu ya klabu yao, Jangwani, Dar es Salaam maarufu kama Jangwani City kujiandaa na mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC Jumamosi, Uwanja wa Taifa, Jijini.
Wakati mabingwa hao wa Ligi Kuu, wakiingia kambini Jangwani, wapinzani wao Azam FC waliorejea jana kutoka Afrika Kusini walipoweka kambi ya takriban wiki mbili, wamefikia kwenye makao yao makuu, Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mchezo huo wa kuashiria kufungua pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara umeteka hisia za wengi na kila timu inaonekana kupania kushinda ili kuwasha taa za kijani kuelekea mbio za ubingwa.
Yanga iliifunga Azam FC katika mechi zote tatu za msimu uliopita walizokutana, hivyo kulipa kisasi cha kufungwa na timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa mara nne msimu uliotangulia katika mashindano yote waliyokutana.  
Katika kujiandaa na msimu, Yanga SC walicheza mechi saba na kushinda tatu, kufungwa moja na sare tatu.
Walizifunga Mtibwa Sugar 3-1, SC Villa ya Uganda 4-1 na 3Pillars ya Nigeria 1-0, na kutoa sare ya 1-1 na Express, 2-2 na URA zote za Uganda na 0-0 na Rhino FC mjini Tabora, wakati walifungwa 2-1 na Express ya mjini Shinyanga.
Kwa upande wa washindi wa pili wa Ligi Kuu, Azam kabla ya kwenda Afrika Kusini walicheza mechi nne na kushinda tatu, 1-0 na komabini ya JKT, 4-0 na African Lyon na 5-1 Ashanti United. Azam pia ilicheza mechi tatu na kikosi chake cha pili, Azam Akademi na kushinda zote, 1-0 mara mbili na 2-1 mara moja.
Na ikiwa Afrika Kusini, ilicheza mechi nne na kufungwa tatu na kushinda moja- ilifungwa 3-0 na Kaizer Chiefs, 2-1 na Orlando Pirates na 1-0 na Moroka Swallows, wakati yenyewe ilishinda 1-0 dhidi ya Mamelodi Sundowns.


UCHAGUZI TFF KUFANYIKA OKTOBA 18

Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetoa tangazo la uchaguzi wa Kamati ya mpya ya Utendaji ambao utafanyika Oktoba 20 mwaka huu. Pia Kamati hiyo imetoa tangazo za uchaguzi wa Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania (TPL Board) ambao utafanyika Oktoba 18 mwaka huu.

Akitangaza mchakato huo wa uchaguzi leo (Agosti 14 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Hamidu Mbwezeleni amesema nafasi zitakazogombewa kwa upande wa TFF ni Rais, Makamu wa Rais na wajumbe 13 wa Kamati ya Utendaji wakiwakilisha kanda mbalimbali.

Fomu kwa wagombea zitatolewa kuanzia Agosti 16 mwaka huu kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 kamili jioni kwenye ofizi za TFF. Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni Agosti 20 mwaka huu. Fomu kwa nafasi ya Rais ni sh. 500,000, Makamu wa Rais ni sh. 300,000 wakati wajumbe ni sh. 200,000.

Mbwezeleni amesema kwa wale ambao walilipia fomu katika mchakato uliofutwa na wanakusudia kugombea nafasi zilezile walizolipia, hawatalipia tena ada ya fomu husika bali watatakiwa kuambatanisha risiti za malipo wakati wa kurudisha fomu za maombi hayo ili kuthibitisha malipo yao.

Kwa upande wa uchaguzi wa TPL Board, fomu zitaanza kutolewa Agosti 16 hadi 20 mwaka huu, na nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti ambapo ada ni sh. 200,000 wakati wajumbe wa Bodi ada ni sh. 100,000.

KAMATI YA SHERIA SASA KUPITIA USAJILI IJUMAA
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji iliyokuwa ikutane jana (Agosti 13 mwaka huu) na leo (Agosti 14 mwaka huu) kupitia usajili wa wachezaji kwa klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza sasa itakutana keshokutwa (Agosti 16 mwaka huu) saa 4 asubuhi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Alex Mgongolwa amepanga tarehe hiyo mpya baada ya kikao cha jana kushindwa kupata akidi. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ina wajumbe saba, na ili kikao kiweze kufanyika ni lazima wapatikane wajumbe kuanzia wanne.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

WILAYA YA KORONGWE YAZIDI KUTAKATA KIMICHEZO


TIMU ya Kandanda ya wilaya ya Korogwe leo imetawadhwa kuwa mabingwa wapya wa Mashindano ya Vijana ya Copa Coca Cola ngazi ya mkoa baada ya kufanikiwa kuitandika Muheza mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa uwanja wa Mkwakwani mjini hapa.

Mchezo huo ambao ulianza majira ya saa nane mchana ulikuwa mkali na wenye upinzani wa hali ya juu kutokana na timu zote kushambuliana kwa zamu na kuonyesha kandanda nzuri na la kuvutia ambapo hadi timu zote zinakwenda mapumziko,Korogwe walikuwa wakiongoza bao 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo timu zote ziliingia uwanjani hapo zikiwa na hari ya mchezo baada ya kufanya mabadiliko kwa baadhi ya wachezaji wake.

Mabao ya Korogwe yalifungwa na Erick Msagati ambaye alipachika mabao yote kwenye mchezo huo ambao ulikuwa wa aina yake.

SCOLARI ANENA KUHUSU MCHEZAJI NYOTA MESSI

Luis Felipe Scolari kocha wa timu ya taifa ya Brazil,  ametabiri kuwa nyota wa Barcelona Lionel Messi ataendelea kuwa mchezaji bora duniani kwa kipindi cha miaka mingine miwili zaidi. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina ameshinda tuzo nne mfululizo za Ballon d’Or na Scolari bado anaamini kuna vitu vingi vinakuja kutoka kwa nyota huyo mwenye miaka 26 kabla ya umri haujaanza kutafuna kiwango chake. 

Scolari pia alimsifu mchezaji huyo kwa kuwa na kipaji cha hali ya juu na uwezo mkubwa wa kubadili mchezo mwenyewe pindi timu yake inapozidiwa. 

Mbali na Messi, Scolari pia alimnadi mshambuliaji mpya wa Barcelona Neymar kuwa naye atakuja kung’ara kama ilivyo kwa Messi katika kipindi kifupi kijacho. Scolari amesema msimu huu utakuwa muhimu kwa Neymar kwa ajili ya kusoma na kuyazoea mazingira mapya ya Ulaya lakini hana shaka kwamba atachukua kipindi kifupi kuzoea hali hilo na kufanya maajabu kama ilivyokuwa Brazil.