Sunday, February 2, 2014

LIBYA WATWAA UBINGWA WA CHAN KWA MARA YA KWANZA VS GHANA

TIMU ya taifa ya Libya wametawadhwa mabingwa wapya wa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani, CHAN baada ya kuifunga Ghana kwa changamoto ya mikwaju ya penati katika mchezo wa fainali uliochezwa katika Uwanja wa Cape Town nchini Afrika Kusini. Libya walinyakuwa taji lao hilo la kwanza la kihistoria kwa kuigaragaza Ghana kwa penati 4-3 baada ya mchezo huo kumalizika bila ya kufungana mpaka katika muda wa nyongeza. Hiyo inakuwa mechi ya tatu kwa Libya kushinda kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya kuziengua Gabon na Zimbabwe katika hatua ya robo fainali na nusu fainali. Kwa wa mechi ya kutafuta mshindi wa tatu Nigeria walifanikiwa kuibuka kidedea baada ya kuifunga Zimbabwe kwa bao 1-0.

TPLB YATAKIWA KUKETI MEZANI KUTATHIMINI MECHI YA STEND UNITED VS KANEMBWA JKT

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Tanzania (TFF) imeiagiza Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ifanyie marejeo (review) uamuzi wake wa kuagiza mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) irudiwe mkoani Tabora.
Maagizo hayo yametolewa na Kamati ya Utendaji iliyokutana jana (Februari 1 mwaka huu) baada ya kupokea vielelezo vipya kuhusiana na mechi hiyo iliyochezwa Novemba 22 mwaka jana mjini Shinyanga.
Mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Kambarage ilivunjwa na mwamuzi dakika ya 87 baada ya kupigwa na wachezaji wa Kanembwa JKT.
Pia Kamati ya Nidhamu ya TFF inatarajiwa kukutana wiki ijayo kujadili tukio hilo la Shinyanga wakiwemo wachezaji wanane wa Kanembwa JKT waliripotiwa kumpiga mwamuzi wa mechi hiyo.

TFF,CRDB KUKETI KUTATHIMINI TIKETI ZA ELEKTRONIC

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeagiza kifanyike kikao cha dharura kati ya Sekretarieti ya TFF, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) na benki ya CRDB ili kutathimini maendeleo ya matumizi ya tiketi za elektroniki.
Lengo la kikao hicho ni kutathimini maendeleo ya utekelezaji wa mfumo huo wa tiketi za elektroniki ni kutafuta ufumbuzi pamoja changamoto zake.
Viwanja vinane nchini vimefungwa mfumo huo wa tiketi za elektroniki. Viwanja hivyo ni Uwanja wa Azam uliopo Chamazi, Uwanja wa Kaitaba, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, Uwanja wa Mkwakwani, na CCM Kirumba.

TARIMBA MWENYEKITI WA ZAMANI WA YANGA APEWA KAMATI YA NIDHAMU TFF

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imefanya uteuzi wa wajumbe kuunda kamati mbili za awali za haki, na kamati mbili za rufani za vyombo hivyo.
Rais wa zamani wa Yanga, Tarimba Abbas ambaye pia kitaaluma ni mwanasheria ataongoza Kamati ya Nidhamu. Wajumbe wanaounda kamati hiyo ni Wakili Jerome Msemwa (Makamu Mwenyekiti), Kassim Dau, Nassoro Duduma na Kitwana Manara.
Kamati ya Rufani ya Nidhamu inaendelea kuongozwa na Profesa Mgongo Fimbo wakati makamu wake ni Wakili Hamidu Mbwezeleni. Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Titus Bandawe, Twaha Mtengera na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) mstaafu Boniface Mpaze.
Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio ambaye pia kitaaluma ni mwanasheria anaongoza Kamati ya Maadili. Wajumbe ni Wakili Ezekiel Maganja, Wakili Victoria Mandari, Kanali mstaafu Enos Mfuru na Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi, Said Mtanda.
Kamati ya Rufani ya Maadili inaundwa na Jaji mstaafu Stephen Ihema (Mwenyekiti), Wakili Alesia Mbuya (Makamu Mwenyekiti), Lilian Kitomari, Jabir Shekimweri na Chabanga Hassan Dyamwale.

Tuesday, January 28, 2014

TFF YAANZA KUUZA TIKETI ZA ELECTRONIC COAST VS YANGA

Mauzo ya tiketi za elektroniki kwa mechi tatu kati ya nne za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zitakazochezwa keshokutwa (Januari 27 mwaka huu) tayari yameanza, hivyo wanatakiwa kununua mapema.
Mechi hizo ni kati ya Coastal Union na Yanga itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar itakayochezwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na ile ya Azam dhidi ya Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Kwa washabiki wa Dar es Salaam watakaokwenda Tanga kushuhudia mechi kati ya Coastal Union na Yanga wanashauriwa kuanza safari wakiwa na tiketi zao mikononi, hasa kwa wale watakaonunua kupitia maduka ya Fahari Huduma.
Tiketi pia zinaweza kununuliwa kupitia mtandao wa M-Pesa kwa kupiga namba *150*03*02#. Kwa wanaotumia CRDB simbanking wanaingia kawaida kwa *150*03.
Vilevile tunawakumbusha washabiki kuwa kwa viwanja ambavyo tayari vina mfumo wa tiketi za elektroniki hakuna tiketi zitakazouzwa uwanjani, hivyo wanaokwenda kwenye mechi wanatakiwa kuwa na tiketi zao mikononi.

YANGA YAANZA LIGI KWA KITITA CHA PESA MIL.86

Mechi za Ligi Kuu ya Vodacom zilizohusisha timu za Simba na Yanga na kuchezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wikiendi zimeingiza jumla ya sh. 139,850,000.
Yanga iliyoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ashanti United pambano lake liliingiza sh. 86,035,000 kutokana na watazamaji 14,261. Mechi ya Simba ambayo ilishinda bao 1-0 dhidi ya Rhino Rangers kutoka Tabora iliingiza sh. 53,815,00 kwa watazamaji 9,629.
Mgawanyo kwa mechi ya Yanga ulikuwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 13,123,983.05, gharama za kuchapa tiketi sh. 2,910,300 wakati kila klabu ilipata sh. 20,650,211.50.
Uwanja sh. 10,500,107.54, gharama za mechi sh. 6,300,064.53, Bodi ya Ligi sh. 6,300,064.53, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,150,032.26 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,450,025.09.
Mechi ya Simba mgawo ulikuwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 8,209,067.80, gharama za kuchapa tiketi sh. 2,910,300 wakati kila klabu ilipata sh. 12,595,211.50.
Uwanja sh. 6,404,344.83, gharama za mechi sh. 3,842,606.90, Bodi ya Ligi sh. 3,842,606.90, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,921,303.45 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,494,347.13.
Vilevile tiketi zinapatikana kupitia maduka ya CRDB Fahari Huduma ambayo yapo katika maeneo mbalimbali nchini. Watakaonunua kupitia maduka hayo watapata tiketi na kwenda moja kwa moja uwanjani.

Monday, September 2, 2013

WENGER AFUNJA UKIMYA

KLABU ya Arsenal imekubali kutoa kitita cha paundi milioni 42.4 kwa ajili ya kumsajili kiungo Mesut Ozil kutoka Real Madrid ya Hispania. Ozil mwenye umri wa miaka 24 naye amefikia makubaliano binafsi na klabu hiyo lakini anatakiwa kufanyiwa vipimo vya afya kabla Arsenal hawajakamilisha usajili huo ambao utavunja rekodi ya klabu hiyo. Kwasasa Ozil yuko katika majukumu ya kimataifa hivyo vipimo vya afya atafanyiwa nchini kwao Ujerumani. Arsenal pia wako katika mazungumzo na Chelsea kwa ajili ya kumsajili kwa mkopo mshambuliaji Demba Ba huku wakiwa tayari wamekamilisha usajili mwingine wa mkopo kwa kipa wa Palermo Emiliano Viviano.