Baada ya kumalizika kwa msimu wa ligi kuu tanzania bara kila timu imejipanga sawasawa katika harakati za usajili pamoja na maandalizi Kabambe
ya msimu mpya wa ligi kuu unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 24
mwaka huu.
Ambapo timu mpya katika ligi kuu na kipenzi kwa wakazi wa jiji la mbeya Mbeya City ya jijini Mbeya
wameanza kujiweka chimbo kujifua chini ya kocha wao mkuu Juma Mwambusi.
Akizungumza na mkali wa dimba Kocha Mwambusi amesema wachezaji kutoka
mikoani wameanza kuwasili kuanzia jana, huku akitanabaisha kuwa anajipanga
kuongeza wachezaji wachache katika kikosi chake alichotoka nacho ligi
daraja la kwanza msimu uliopita.
“Wachezaji
wengi ni walewale, nina mpango wa kuongeza nyota wachache, wengi
nitawapandisha kutoka kikosi B, lakini wachezaji wengi waliopandisha
timu ligi kuu nimewaacha ila kuna nafasi chache nitaziba hivi karibuni”.
Alisema Mwambusi.
Mwambusi
amesema katika kikosi chake hana tabia ya kuwapa majina wachezaji kwa
kuwapa uhakika wa namba, kwani falsafa yake ni kuchezesha wachezaji wote
bila kujali majina yao.
Kuhusu
kusajili wachezaji wenye uzoefu mkubwa na mikikimikiki ya ligi kuu,
Mwambusi alisema hana mpango wa kusajili wakongwe kutokana na kikosi
chake kuwa na vijana wengi ambao wanafanya vizuri.
“Mbeya
City ina kikosi bora cha vijana, ninavyozungumza hapa kipo mkoani
Iringa wilaya ya Mufindi kushiriki michuano ya kombe la Muungano
Mufindi, ni kikosi kizuri sana, kinaongozwa na kocha wangu msaidizi Maka
Mwalwisyi ambaye anafanya kazi nzuri. Ni matumaini yangu hawa vijana ni
msingi mkubwa wa klabu yangu na watapewa nafasi”.
Mwambusi
alisema kikosi chake kinahitaji kujifua kwa nguvu kuhimili mitanannge
ya ligi kuu, kwani ligi ya Tanzania bara imekuwa na ushindani mkubwa
sana.
“Ligi
imebadilika sana, niliifundisha Prisons miaka ya nyuma, sasa naona
mambo yamebadilika sana, lakini nina uhakika kwa uzoefu wangu
nitajipanga vizuri na kupambana hadi mwisho”. Alisema Mwambusi.
Mbeya
City ni miongoni mwa timu tatu zilizopanda ligi kuu soka Tanzania bara
msimu ujao, wakati nyingine ni Maafande wa Rhino Rangers ya Tabora, na
Ashanti United ya Dar es salaam.
Msimu
uliopita timu tatu za Africa Lyon ya Dar es salaam, Toto Africans ya
Mwanza na Polisi Morogoro zilishuka daraja na sasa zinaendelea na
mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi daraja la kwanza.