Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi
ili kufanya uamuzi wenye manufaa kwa washabiki wa mpira wa miguu baada ya
tarehe ya uchaguzi aliyotangaza kuingilia na mechi ya watani wa jadi (Simba na
Yanga) ya Ligi Kuu ya Vodacom.
Sekretarieti
ya TFF imepokea maoni kutoka kwa wapenzi mbalimbali wa mpira wa miguu wakiomba
matukio hayo mawili (Uchaguzi wa TFF na mechi ya Simba na Yanga) yafanyike
katika siku tofauti.
Wakati
Kamati ya Uchaguzi inatangaza uchaguzi kufanyika Oktoba 20 mwaka huu tayari
ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom ilikuwa imeshatoka, na ikionesha kuwa timu ambazo
zina historia ya kipekee katika mpira wa miguu zitacheza siku hiyo.
Sekretarieti
imelazimika kumwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi kwa vile yeye na
kamati yake ndiye wenye mamlaka ya kuitisha Mkutano wa Uchaguzi. Huko nyuma TFF
imeshafanya mikutano huku kukiwa na mechi za timu ya Taifa (Taifa Stars), jambo
ambalo liliwezekana kutokana na mikutano hiyo kuwa na ajenda moja tu.
Tayari Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni ameitisha
kikao cha kamati yake kujadili barua hiyo ya sekretarieti.
COCA COLA YATOA MIPIRA 100, FULANA 800
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa shukrani kwa kampuni ya Coca Cola kwa
kukabidhi fulana 800 na mipira 100 kwa ajili ya ngazi ya mashindano ya vijana
wenye umri chini ya miaka 15 ngazi ya mikoa yanayoanza Septemba Mosi mwaka huu.
Coca Cola
ndiyo inayodhamini mashindano hayo yaliyoanzia ngazi ya wilaya ambapo mwaka huu
yatachezwa kwa kanda na baadaye fainali itakayochezwa kuanzia Septemba 7-14
mwaka huu jijini Dar es Salaam ikishirikisha mikoa 16 itakayokuwa imefanya
vizuri katika ngazi ya kanda.
Kila mkoa utapata fulana 25 na mipira mitatu ikiwa ni sehemu ya
maandalizi ya timu zao kwa ajili ya michuano hiyo ngazi ya kanda itakayomazika
Septemba 6 mwaka huu.
Kanda hizo
ni Mwanza itakayokuwa na timu za mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma, Mara, Mwanza,
Shinyanga, Simiyu na Tabora. Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Singida
inaunda Kanda ya Arusha.
Zanzibar
itakuwa na Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na mikoa miwili ya Unguja wakati Kanda
ya Dar es Salaam ina Ilala, Kinondoni, Lindi, Mtwara, Temeke na mkoa mmoja wa
Unguja.
Kanda ya Mbeya inaundwa na
Iringa, Katavi, Mbeya, Njombe, Rukwa na Ruvuma wakati Dodoma, Morogoro, Pwani
na Tanga zinaunda Kanda ya Morogoro.
Mwanza
itatoa timu nne kucheza hatua ya fainali wakati kanda nyingine za Arusha timu
mbili, Zanzibar (2), Mbeya (3) na Kanda ya Morogoro itaingiza timu mbili.
Wakati huo huo, semina ya
makocha 32 wa timu za mikoa zitakazoshiriki michuano ya U15 FIFA Copa Coca-Cola
iliyokuwa ikiendeshwa na mkufunzi Govinder Thondoo kutoka Mauritius inafungwa
leo (Agosti 16 mwaka huu) saa 9 alasiri kwenye ukumbi wa Msimbazi Center, Dar
es Salaam.
RAMBIRAMBI MSIBA WA
MWANDISHI GRACEMO BAMBAZA
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha aliyekuwa
mwandishi wa habari za michezo wa Radio ABM ya Dodoma, Gracemo Bambaza
kilichotokea Agosti 14 mwaka huu katika Hospitali ya Ocean Road, Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa katika
sekta ya habari na mpira wa miguu kwani Bambaza kwa kipindi chote akiwa
mwandishi alikuwa akifanya kazi nasi, hivyo mchango wake katika mpira wa miguu
tutaukumbuka daima.
Bambaza aliyezaliwa mwaka
1973 na ambaye pia aliwahi kufanya kazi katika vituo vya redio vya Wapo cha Dar
es Salaam na Pride cha Mtwara amesafirishwa jana (Agosti 15 mwaka huu) kwenda
Karagwe mkoani Kagera kwa ajili ya mazishi.
TFF tunatoa pole kwa familia
ya marehemu Bambaza, ABM Radio na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo
Tanzania (TASWA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki
kigumu cha msiba huo mzito.
Mungu aiweke roho ya
marehemu Bambaza mahali pema peponi. Amina
TIKETI MECHI YA YANGA, AZAM KUUZWA ASUBUHI
Tiketi kwa ajili ya mechi ya
Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Azam itakayochezwa kesho (Agosti 17 mwaka huu)
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitaanza kuuzwa saa 3 asubuhi.
Vituo vitakavyouza tiketi
hizo Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers
ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live
Mbagala na BMM Barber Shop iliyoko Sinza Madukani.
Katika vituo
hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari yote yanayouza tiketi
yatahamia uwanjani saa 7 kamili mchana.
Viingilio
katika mechi hiyo ni sh. 7,000 kwa viti vya rangi ya kijani na bluu wakati viti
vya rangi ya chungwa ni sh. 10,000. Watakaiongia viti vya VIP C watalipa sh.
15,000, viti vya VIP B ni sh. 20,000 wakati VIP A watalipa sh. 30,000.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF)