TIMU YA WATOTO WA MITAANI YATINGA FAINALI BRAZIL
Timu ya Taifa ya Watoto wa Mitaani ya
Tanzania imetinga fainali za mashindano ya Kombe la Dunia la Watoto wa
Mitaani baada ya kuichapa Marekani mabao 6-1 katika mchezo wa kwanza wa
nusu fainali uliochezwa jana (Aprili 5 mwaka huu) jijini Rio de Janeiro,
Brazil.
Hadi mapumziko Tanzania ilikuwa mbele
kwa mabao 4-0. Bao pekee la Marekani katika mchezo huo ambayo hadi nusu
fainali ilikuwa haijafungwa lilifungwa dakika za mwisho.
Kwa matokeo hayo, Tanzania inacheza
Fainali na Burundi. Mechi hiyo inachezwa leo (Aprili
6 mwaka huu) ambapo
Burundi imetinga hatua hiyo baada ya kuifunga Pakistan mabao 4-3 katika
nusu fainali ya pili.

Mchezo huo wa fainali unachezwa uwanja
mkongwe na maarufu wa klabu ya Fluminense katikati ya Jiji la Rio de
Janeiro huku mgeni rasmi akiwa Waziri wa Fedha wa Uingereza, George
Osborne.
Katika mechi ya kwanza katika kundi B la michuano hiyo, Tanzania ilicheza na Burundi na kutoka sare ya mabao 2-2.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF