MAKOCHA wa timu za Taifa za Tanzania
(Taifa Stars) na Burundi (Intamba Mu Rugamba), Salum Mayanga na mwenzake
Niyungeko Alain Olivier wameahidi burudani ya nguvu kwenye mechi yao
itakayochezwa kesho (Aprili 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ya kirafiki ambayo ni
sehemu ya maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar itachezeshwa na
refa Anthony Ogwayo kutoka Kenya na itaanza saa 10 kamili jioni.
Ogwayo atasaidiwa na Gilbert
Cheruiyot na Oliver Odhiambo wote pia kutoka Kenya.
Mwamuzi wa mezani atakuwa Israel
Mujuni wa Tanzania wakati Kamishna ni Charles Ndagala.
Mayanga amesema wanatumia mechi hiyo
kama sehemu ya maandalizi ya mechi za mchujo za Kombe la mataifa ya Afrika, na
ameahidi kuchezesha baadhi ya wachezaji waliopatikana kwenye mpango wa
maboresho ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager.
Naye Niyungeko amesema amekuja na
kikosi imara ambacho pia kitakuwa na washambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe na
Didier Kavumbagu wa Yanga, lengo lao ni kuhakikisha wanapata ushindi kwa vile
Taifa Stars imekuwa ikiwasumbua kila wanapokutana nayo.
Viingilio katika mechi hiyo ni sh.
5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani. Kwa VIP A kiingilio
kitakuwa sh. 20,000 wakati VIP B na C ni sh. 10,000.
Wakati huo huo, Kocha Mkuu mpya wa
Taifa Stars, Martinus Ignatius Maria maarufu kama Mart Nooij atatambulishwa kwa
waandishi wa habri kesho Jumamosi (Aprili 26 mwaka huu) saa 8 kamili mchana
kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Taifa. |
|