Tuesday, May 13, 2014

DIEGO COSTA KUELEKEA STAMFORD BRIDGE MAPEMA JUNI


Klabu ya Chelsea imekubali kutoa kiasi cha pauni milioni 32 kwa Atletico Madrid kwaajili ya kukamilisha dili la kumsajili mshambuliji mahiri,Diego Costa.
Costa ambaye amekuwa muhimili mkubwa kwa klabu hiyo ya Uhispania ikiwa na uwezo wa kuchukua La Liga na Ligi ya mabingwa barani Ulaya mpaka sasa, amekuwa akihusishwa na kuhamia London huku Jose Mourinho akihitaji mshambuliaji hatari zaidi.
Mourinho alisisitiza mara baada ya mchezo wa mwisho wa ligi kuu ya Uingereza kuwa alikuwa na malengo ya kufanya usajili mkubwa sana Stamford Bridge katika kipindi cha soko la usajili haraka iwezekanavyo.
Dili la Costa halitarajiwi kutangazwa rasmi mpaka ifikapo mapema mwezi Juni mara baada ya michezo miwili mikubwa ambayo nyota huyo anapambana kuweza kuwa fiti kuisaidia timu yake.
Costa alipata majeraha ya misuli na alikosa mchezo waliotoka sare ya 1-1 dhidi ya Malaga Jumapili,mchezo ambao iwapo Atletico wangeshinda wangekuwa
tayari wametwaa taji la La Liga msimu huu.
Atletico watasafiri mpaka Camp Nou kupambana na Barcelona siku ya Jumapili katika mchezo ambao utaamua kombe linaenda wapi na siku saba baadae watakutana na wapinzani wao wa Jiji,Real Madrid kwenye fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya itakayopigwa Lisbon.
Chelsea walimaliza msimu wa 2013/14 katika nafasi ya tatu,pointi nne nyuma ya Manchester City na pointi mbili nyuma ya Liverpool huku rekodi yao ya kufunga magoli ikionekana ndiyo sababu ya kushindwa kwao kupata taji.
Kikosi cha darajani kilifunga magoli 71 ukilinganisha na magoli 102 ya Man City na 101 ya Liverpool na mchezaji mmoja pekee ndiye alikuwa
mhimili ambaye ni kiungo mshambuliaji Eden Hazard akifunga magoli 14.
Samuel Eto’o,Fernando Torres na Demba Ba walifunga jumla ya magoli 19 pekee wote kati yao hivyo kumshawishi Mourinho kutumia pesa nyingi kwaajili ya kupata saini ya mchezaji kama Costa ambaye amefunga magoli 27 kwenye michezo 33 ya La Liga msimu huu.