Kocha
wa Taifa Stars, Mart Nooij amesema wachezaji wake wako tayari kwa ajili
ya mechi ya Kombe la Afrika dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors)
itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam leo (Mei 16 mwaka huu), Nooij amesema kabla ya kuja
Tanzania alikuwa akifuatilia Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), hivyo
anawafahamu wachezaji wengi.
Amesema wachezaji wanaounda kikosi chake
ni wenye uzoefu na mechi za kimataifa, hivyo wapo tayari kwa ajili ya
mechi hiyo, kwani wamepata mechi za kirafiki na mazoezi ya kutosha
kwenye kambi iliyokuwa Tukuyu mkoani Mbeya ambapo kulikuwa na utulivu
mkubwa.
Nooij amesema ujio wa washambuliaji
Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (RDC) kutaongeza morali ya kikosi chake.
Samata na Ulimwengu watawasili nchini
Jumamosi mchana, saa 7.30 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines
wakitokea Khartoum, Sudan ambapo leo (Mei 16 mwaka huu) wanacheza mechi
ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Hilal ya huko.
Wachezaji waliopo kambini kwa sasa ni
Deogratias Munishi, Aishi Manula, Said Moradi, Oscar Joshua, Kelvin
Yondani, Erasto Nyoni, Nadir Haroub, Shomari Kapombe, Aggrey Morris,
Himid Mao, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Amri Kiemba, Jonas Mkude,
Haruna Chanongo, Simon Msuva, Mrisho Ngasa, Khamis Mcha, Ramadhan
Singano, John Bocco, Elias maguli na Kelvin Friday.
Wakati huo huo, timu ya Zimbabwe (Mighty
Warriors) inawasili kesho alfajiri (Mei 17 mwaka huu) kwa ndege ya
Ethiopian Airlines ikiwa na msafara wa watu 27. Kesho saa 4 asubuhi (Mei
17 mwaka huu) Kocha wa timu hiyo atakuwa na mkutano na waandishi wa
habari katika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zinaanza
kuuzwa kesho (Mei 17 mwaka huu) kwenye vituo vya Shule ya Sekondari
Benjamin Mkapa, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Ohio na Samora, OilCom
Ubungo, Uwanja wa Taifa, kituo cha mafuta Buguruni na Dar Live Mbagala.
Viingilio ni sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 20,000 tu.
…MDAU AAHIDI WACHEZAJI MIL 5/-
Mdau mmoja wa mpira wa miguu ambaye
hataki jina lake litajwe ameahidi kutoa sh. milioni tano kwa wachezaji
wa Taifa Stars iwapo wataifunga Zimbabwe katika mechi ya Jumapili.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) linamshukuru mdau huyo, na linatoa mwito kwa wadau wengine
wajitokeze kutoa motisha kwa Taifa Stars.
Bonasi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa wachezaji wa Taifa Stars itatolewa kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
TFF YAOMBOLEZA VIFO VYA WASHABIKI DR CONGO
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za rambirambi mwenzake wa
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- FECOFA, Omar Constant kutokana na vifo
vya washabiki.
Washabiki 12 walipoteza maisha uwanjani
wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya nchi hiyo kati ya TP Mazembe na AS Vita
iliyochezwa kwenye Uwanja wa Tata Raphael, jijini Kinshasa.
“Tumeguswa na msiba huo mzito, tunatoa
salamu za rambirambi kwako (Rais wa FECOFA), familia za marehemu pamoja
na wadau wote wa mpira wa miguu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,”
imesema sehemu ya barua hiyo ya Rais Malinzi.
KOZI ZA UKOCHA LESENI A, B KUFANYIKA JUNI
Kocha a ukocha wa mpira wa miguu kwa
ajili ya leseni A na B zinazotambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF) zitafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 2 mwaka huu.
Ada kwa kozi zote ni sh. 300,000 ambapo
wale watakaofanya ya A (equivalent) itaanza Julai 21-26 mwaka huu.
Washiriki wa kozi hiyo ni wale wenye leseni B za ukocha za CAF.
Kwa wale watakaoshiriki kozi ya leseni B
ambao ni wale wenye leseni C watakuwa na vipindi viwili. Kipindi cha
kwanza ni kuanzia Juni 2-15 mwaka huu wakati cha pili kinaanza Juni 23
mwaka huu na kumalizika Juni 28 mwaka huu.
Wakufunzi wanaotambuliwa na CAF
watakaoendesha kozi hiyo ni Sunday Kayuni na Salum Madadi kutoka
Tanzania, na washiriki watajigharamia kwa kila kitu. Baadaye CAF
watatuma Mkufunzi mwingine kwa ajili ya mitihani.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)