Thursday, June 5, 2014

TAIFA STARS: 28 WAITWA KUPIGA KAMBI YA SIKU 3 KUANZIA JUNI 11

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea taarifa za kutolewa wito bungeni wa kulitaka litumie tiketi za elektroniki katika kukusanya mapato.
Tunataka ieleweke wazi kwa umma wa Watanzania kuwa si nia yetu kuchelewesha matumizi ya uingiaji mpirani kwa tiketi za elektroniki. Ieleweke kuwa mfumo wa kuingia kwenye mbuga, KCMC, mipakani ni tofauti na uingiaji mpirani.
Katika mpira wa miguu wanaingia maelfu ya watu katika kipindi kifupi. Kwa kuzingatia umuhimu wa kulinda usalama wa watazamaji na miundombinu ya viwanja ndio maana tulisitisha matumizi ya tiketi za elektroniki hadi tujihakikishie usalama wa matumizi yake.
Tunafanya jitihada kwa karibu na mzabuni benki ya CRDB ili kuhakikisha mfumo huu unaanza kutumika mara moja.
Kwa niaba ya sekta ya michezo tunatoa wito kwa Serikali kushusha au kuondoa kodi kubwa zinazotozwa kwenye vifaa vya michezo, hasa vinavyotumiwa na watoto kuanzia umri wa miaka 6-12, ili watoto wetu waweze kuvipata kirahisi toka kwa wazazi wao ili waweze kujifunza kucheza michezo kisasa tangu wakiwa wadogo.
TAIFA STARS KUINGIA KAMBINI JUNI 11
Kikosi cha Taifa Stars kinaingia tena kambini Jumatano (Juni 11 mwaka huu) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika dhidi ya Msumbiji itakayochezwa Julai 20 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwa na kambi ya siku tatu jijini Dar es Salaam ikijumuisha wachezaji 28. Kwa mujibu wa programu ya Kocha Mart Nooij, Stars itaingia tena kambini Juni 24 mwaka huu.
Wachezaji wanaotakiwa kuripoti kambini ni Deogratias Munishi, Aishi Manula, Benedictor Tinoko, Kelvin Yondani, Said Moradi, Nadir Haroub, Joram Nason, Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Edward Charles, Aggrey Morris na Pato Ngonyani.
Wengine ni Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Amri Kiemba, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Said Juma, Haruna Chanongo, Himid Mao, Said Ndemla, John Bocco, Simon Msuva, Kelvin Friday, Ramadhan Singano, Khamis Mcha, Mrisho Ngasa na Mwegane Yeya.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)