Ikiwa zimebaki siku 10 kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu msimu wa 2014-2015 wadhamini wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Vodacom watoa jezi kwa vilabu vyote 14 vitakavyoshiriki ligi hiyo.
Katika hafla ya kukabidhi vifaa kwa timu za Ligi Kuu msimu mpya leo, Vodacom wamekabidhi jezi za rangi ya kijani na njano kwa Yanga na nyekundu na nyeupe kwa Simba, lakini muundo ni mmoja kila kitu.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliwakilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ambaye alihakikisha timu zote 14 za Ligi Kuu zinapatiwa vifaa hivyo.
Timu zote 14 zilituma wawakilishi wao katika hafla hiyo iliyofanyika makao makuu ya Vodacom, Mlimani City, Dar es Salaam.
Ligi Kuu inatarajiwa kuanza Septemba 20, mwaka huu, mabingwa watetezi, Azam FC wakifungua dimba na Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mechi nyingine za ufunguzi za Ligi Kuu zitakuwa kati ya Stand United watakaoikaribisha Ndanda ya Mtwara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mgambo JKT wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Mabingwa wa zamani wa ligi hiyo, Simba SC wataanza kampeni ya kutwaa tena taji hilo Septemba 21 dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ligi hiyo itatanguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii utakaochezwa Jumapili wiki hii, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Azam FC na Yanga SC.