Saturday, November 22, 2014

JE WAJUA:MBEYA CITY,PRISON,STAND HAZINA MCHEZAJI ALICHEZA SIMBA WALA YANGA

Tanzani Prisons,Mbeya City na Stand United ndizo timu pekee ambazo hazijafanikiwa kutwaa mchezaji yeyote aliyewahi kucheza Yanga ama Simba katika vikosi vyao msimu huu.
Baada ya kuchezwa mechi saba, uchunguzi umeonyesha kuwa Yanga ina wachezaji 20 na Simba 19 wanaocheza katika timu 11 kati ya 14 zinazoshiriki ligi hiyo.
Timu ambazo zina wachezaji waliowahi kucheza Simba na Yanga kwa vipindi tofauti na sasa wapo timu hizo ni Azam, JKT Ruvu, Kagera Sugar, Mgambo Shooting, Mtibwa Sugar, Ndanda, Polisi Morogoro, Ruvu Shooting , Simba na Yanga.
Hali hiyo inawapa nafuu Yanga na Simba katika baadhi ya michezo yao kwani kuna kasumba ya baadhi ya wachezaji kuwa na unazi uliopitiliza kwa vigogo hao.
Madai ya mapenzi ya Usimba na Uyanga yamewakuta  wachezaji wengi wanapocheza dhidi ya timu zao za zamani huku baadhi yao wakituhumiwa kucheza chini ya kiwango kisa walitoka kwenye mojawapo ya timu hizo.
Hata hivyo, Simba imeonekana kuwa na wachezaji wengi wa Yanga wakati watani zao, Yanga wameonyesha wana idadi kubwa ya wachezaji kwenye kikosi cha JKT Ruvu na Azam.
Wachezaji waliowahi kuichezea Simba ambao sasa wapo Yanga ni Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Kaseja, Ali Mustapha ‘Barthez’ na beki Kelvin Yondani, wakati wachezaji waliopo Simba na ambao wamewahi kupita Yanga ni Amri Kiemba, Ivo Mapunda na Emmanuel Okwi.
Simba pia ina wachezaji wawili JKT Ruvu ambao ni Ramadhan Shamte na Jabir Aziz, wakati Yanga katika kikosi cha maafande hao ina wachezaji watatu ambao ni Benjamin Haule, Jackson Chove na  Reliant Lusajo.
Yanga ina wachezaji watatu Azam, Frank Domayo, Gaudence Mwaikimba na Didier Kavumbagu, wakati watani zao Simba pia wana wachezaji wawili kwenye kikosi cha mabingwa hao, ambao ni Said Morad na Shomari Kapombe.
Katika kikosi cha Mtibwa Sugar, Simba ina wachezaji wawili, Mussa Hassan Mgosi na Abdallah Juma, wakati Yanga wana Vicent Barnabas, Said Mohamed na David Luhende. Kwenye kikosi cha Kagera Sugar, Yanga wana wachezaji Abubakary Mtiro na Atupele Green, wakati Simba wana Adam Kingwande na Salum Kanoni.
Polisi Morogoro, Simba inajivunia wachezaji Edward Christopher, Danny Mrwanda na Salum Machaku, wakati Yanga inajivunia Chacha Marwa na Lulanga Mapunda.
Yanga pia ina wachezaji wawili Coastal Union ambao ni Hussein Sued na Razack Khalfan, wakati watani zao Simba hawana mchezaji yeyote kwenye kikosi hicho, lakini wanawazidi Yanga kwani wana wachezaji wawili Ndanda ambao ni Paul Ngalema na Wilbert Mweta na wapinzani wao hawana mchezaji ndani ya kikosi hicho.
Source:Mwananchi