KLABU ya Arsenal
imekubali kutoa kitita cha paundi milioni 42.4 kwa ajili ya kumsajili
kiungo Mesut Ozil kutoka Real Madrid ya Hispania. Ozil
mwenye umri wa miaka 24 naye amefikia makubaliano binafsi na klabu hiyo
lakini anatakiwa kufanyiwa vipimo vya afya kabla Arsenal
hawajakamilisha usajili huo ambao utavunja rekodi ya klabu hiyo. Kwasasa Ozil yuko katika majukumu ya kimataifa hivyo vipimo vya afya atafanyiwa nchini kwao Ujerumani. Arsenal
pia wako katika mazungumzo na Chelsea kwa ajili ya kumsajili kwa mkopo
mshambuliaji Demba Ba huku wakiwa tayari wamekamilisha usajili mwingine
wa mkopo kwa kipa wa Palermo Emiliano Viviano.
Monday, September 2, 2013
ILALA, KASKAZINI UNGUJA ZAANZA COPA KWA SARE
Timu
za Ilala na Kaskazini Unguja zimetoka sare ya mabao 3-3 katika moja ya
mechi za ufunguzi za michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri
chini ya miaka 15 iliyoanza leo (Septemba 2 mwaka huu) katika vituo
mbalimbali nchini.
Wafungaji
wa Ilala katika mechi hiyo iliyochezwa asubuhi Uwanja wa Tamco ulioko
Kibaha, Pwani yalifungwa na Ally Shaban (mawili) wakati lingine
lilifungwa na Haruni Said. Mabao ya Kaskazini Unguja yalifungwa na Jecha
Ally (mawili) na Shehe Ally.
Katika
kituo cha Mbeya, Njombe imeanza vizuri baada ya kuifunga Katavi mabao
2-1. Mabao ya washindi yalifungwa na Rackson Mligo dakika ya 13 wakati
lingine lilifungwa na Kelvin Gama dakika kumi kabla ya filimbi ya
mwisho.
Bao la Katavi katika mechi hiyo iliyochezwa uwanja wa Sekondari ya Iyunga lilifungwa dakika ya 15 kupitia Joseph Edward.
Wenyeji
Mbeya wameitandika Ruvuma mabao 3-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa
Iyunga. Mabao ya washindi yalifungwa na Joel Mwasambungu dakika 9 wakati
mengine yalifungwa na Jackson Mwaibambe dakika ya 18 na 55.
Kesho
(Septemba 3 mwaka huu) katika kituo hicho kutakuwa na mechi kati ya
Rukwa na Katavi itakayochezwa saa 4 asubuhi wakati Iringa na Ruvuma
zitaumana kuanzia saa 2 asubuhi.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
HENRY JOSEPH AITWA TAIFA STARS
Kocha
Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amemjumuisha mchezaji Henry Joseph wa
Simba kwenye kikosi chake kinachojiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la
Dunia dhidi ya Gambia itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu jijini Banjul.
Tayari
Joseph amesharipoti kwenye kambi ya timu hiyo iliyoko hoteli ya
Accomondia jijini Dar es Salaam. Taifa Stars ambayo iko chini ya
udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager imeingia kambini tangu Agosti 29
mwaka huu, na leo jioni itafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Karume.
Programu
ya timu hiyo inaonesha kuwa kesho (Septemba 3 mwaka huu) itafanya
mazoezi yake asubuhi na jioni kwenye uwanja huo huo wa Kumbukumbu ya
Karume.
Wakati huo huo, kesho (Septemba 3 mwaka huu) saa 6 kamili mchana Kocha Kim Poulsen atakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari.
LIUNDA KUTATHMINI WAAMUZI CL
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Leslie Liunda wa Tanzania kuwa
mtathmini wa waamuzi kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya
Coton Sport ya Cameroon na Esperance ya Tunisia.
Mechi
hiyo ya kundi B itachezwa Septemba 21 mwaka huu kwenye Uwanja wa
Omnisport Roumdeadjia mjini Garoua, Cameroon. Kamishna atakuwa Bema
Doumbia wa Ivory Coast.
Waamuzi
wanatoka Madagascar wakiongozwa na Hamada Nampiandraza. Wasaidizi wake
ni Jean Eric Pierre Andrivoavonjy, Ferdinand Velomanana Linoro na Bruno
Marie Andrimiharisia.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Friday, August 16, 2013
MOURINHO ASEMA NATAKA KUWEKA POA FAMILIA YA WANACHELSEA
Meneja wa Chelsea, Jose Mourinho amesema lengo kuu anataka kurudisha upya familia ya
wadau wa Chelsea ambayo ilivunjika baada ya kocha aliyeondoka Rafa Benitez
kumrithi kocha kipenzi cha mashabiki Roberto Di Matteo na kusababisha
tofauti kwa mashabiki wa klabu hiyo.
Chelsea
waliingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe baada ya kumfukuza kocha
aliyewapa ubingwa wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, na hata baada ya
Benitez kushinda kombe la Uropa haikumnusuru kufungashiwa virago.
Ambapo mmiliki Roman Abramovich alimgeukia tena kwa mara ya pili Mourinho majira haya ya kiangazi na amefanikiwa kumrejesha.
Kocha
huyo mwenye Umri wa miaka 50, raia wa Ureno aliliambia gazeti la The
Sun: “Nawataka kuwa nasi kama familia ya Chelsea-familia ambayo kwa muda
fulani mwaka jana ilionekana kuvunjika”.
SUAREZ ARUDI NYUMBANI ANFIELD BAADA YA MISUKOSUKO YA HAPA NA PALE YA KUTAKA KUONDOKA"
Mshambuliaji nyota Luis
Suárez leo amerudi kikosini huko Anfield na kuanza Mazoezi tena pamoja na
Kikosi cha Kwanza cha Timu ya Liverpool baada ya kuzuiwa kufanya hivyo
na Meneja Brendan Rodgers kwa kuishambulia Klabu kwa madai ya kuvunja
ahadi ya kumruhusu ahame ikiwa haitafuzu kucheza UEFA CHAMPIONZ LIGI
Msimu huu.
Jumanne iliyopita Suarez alilazimishwa
kufanya Mazoezi peke yake na kutakiwa kuiomba Klabu radhi kwa kauli zake
na inaaminika Mchezaji huyo ametii amri hiyo na ndio maana amerudishwa
tena Mazoezini kwenye Kikosi cha Kwanza.
Suarez amekuwa akisinikiza kuihama
Liverpool na Arsenal ilishatoa Ofa ya Pauni 40,000,001 kumnunua lakini
Liverpool imekataa na kusisitiza Mchezaji huyo hauzwi.
Msimamo huo ulisisitizwa zaidi na
Mmiliki mkuu wa Liverpool kutoka Marekani, John W Henry, ambae Wiki
iliyopita alitamka Suarez hatauzwa kwa Arsenal au kwa Klabu yeyote
Ulaya.
Kwa sasa Suarez yupo kwenye Kifungo cha
Mechi 10 alichopewa mwishoni mwa Msimu uliokwisha Mwezi Mei kwa
kumng’ata meno Beki wa Chelsea Branislav Ivanovic kwenye Mechi na tayari
ameshatumuikia Mechi 4 na bado 6.
Wakati huo huo, Liverpool imefanikiwa
kukubaliana na Klabu ya Spain, Valencia, ili kumchukua Beki wao wa
kushoto Aly Cissokho kwa Mkopo wa Msimu mmoja.
Meneja wa Liverpool Brendan Rodgers
alikuwa akisaka Mchezaji wa pozisheni hiyo ili kuleta ushindani kwa Beki
wake José Enrique na waliwahi kuwawania Lorenzo Melgarejo wa Benfica na
Guilherme Siqueira wa Granada ili kujaza Nafasi hiyo.
KAMATI YASHERIA NA HADHI ZA WACHEZAJI YA TFF YATOA MAAMUZI KUHUSU NGASA"
KAMATI ya Sheria na Hadhi za
Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imepitia usajili wa wachezaji wa
klabu za Ligi Kuu ya Vodacom na kumuidhinisha Mrisho Ngasa kuchezea timu ya Yanga
baada ya kukamilisha usajili wake.
Hata hivyo, Kamati hiyo chini ya
Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa imebaini kuwa Ngasa alisaini mkataba mwingine
Simba (katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam) ambapo anatakiwa
kurejesha fedha alizopokea (sh. milioni 30) pamoja na fidia ya asilimia 50 (sh.
milioni 15) ya fedha hizo kwa Simba.
Kamati pia imemfungia mechi sita za
mashindano (kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii), na anatakiwa awe amelipa fedha
hizo ndani ya kipindi hicho cha kukosa mechi hizo. Akishindwa, hataruhusiwa
kucheza hadi atakapolipa fedha hizo.
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni,
Kamati imeagiza wasiruhusiwe kucheza hadi watakapopata Hati za Uhamisho wa
Kimataifa (ITC) pamoja na vibali vya kufanya kazi nchini (work permits).
Kamati hiyo itakutana tena Ijumaa
(Agosti 23 mwaka huu) ili kupata ripoti za pingamizi ilizoagiza ziwe
zimefanyiwa kazi hadi Agosti 22 mwaka huu na kutoa uamuzi kwa pande ambazo
hazikuafikiana.
Wakati huo huo: Kamati ya TFF kwa
kuzingatia mamlaka iliyonayo katika kifungu cha 10(6) cha Kanuni za Uchaguzi za
TFF inasogeza mbele tarehe ya uchaguzi wa TFF kutoka Oktoba 20 mpaka Oktoba 26
na 27 mwaka huu.
Sababu za kusogeza mbele uchaguzi ni
kutokana na ukweli kuwa Oktoba 20 mwaka huu uongozi wa TFF utakuwa na shughuli
nyingi za maandalizi ya mechi ya Simba na Yanga, na hivyo haitawezekana
kusimamia shughuli za Mkutano Mkuu wa Uchaguzi kwa wakati mmoja na mchezo huo.
Siku ya mwisho ya kampeni itakuwa
Oktoba 25 mwaka huu. Ukiondoa mabadiliko hayo ya tarehe ya uchaguzi wa
viongozi wa TFF, ratiba ya mchakato wa uchaguzi na itabaki kama ilivyotangazwa
na Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika mkutano wake na waandishi wa habari Agosti
24 mwaka huu.
Pia Kamati imeamua kuwa uchaguzi wa
Bodi ya Ligi utabakia kuwa Oktoba 18 mwaka huu kama ilivyopangwa awali.
Kamati imesema inaamini wahusika
wote watapokea vizuri mabadiliko hayo na inasikitika kwa usumbufu
utakaosababishwa na mabadiliko hayo.
|
KAMATI YA UCHAGUZI KUJADILI SIMBA, YANGA
Sekretarieti
ya TFF imepokea maoni kutoka kwa wapenzi mbalimbali wa mpira wa miguu wakiomba
matukio hayo mawili (Uchaguzi wa TFF na mechi ya Simba na Yanga) yafanyike
katika siku tofauti.
Wakati
Kamati ya Uchaguzi inatangaza uchaguzi kufanyika Oktoba 20 mwaka huu tayari
ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom ilikuwa imeshatoka, na ikionesha kuwa timu ambazo
zina historia ya kipekee katika mpira wa miguu zitacheza siku hiyo.
Sekretarieti
imelazimika kumwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi kwa vile yeye na
kamati yake ndiye wenye mamlaka ya kuitisha Mkutano wa Uchaguzi. Huko nyuma TFF
imeshafanya mikutano huku kukiwa na mechi za timu ya Taifa (Taifa Stars), jambo
ambalo liliwezekana kutokana na mikutano hiyo kuwa na ajenda moja tu.
Tayari Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni ameitisha
kikao cha kamati yake kujadili barua hiyo ya sekretarieti.
COCA COLA YATOA MIPIRA 100, FULANA 800
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa shukrani kwa kampuni ya Coca Cola kwa
kukabidhi fulana 800 na mipira 100 kwa ajili ya ngazi ya mashindano ya vijana
wenye umri chini ya miaka 15 ngazi ya mikoa yanayoanza Septemba Mosi mwaka huu.
Coca Cola
ndiyo inayodhamini mashindano hayo yaliyoanzia ngazi ya wilaya ambapo mwaka huu
yatachezwa kwa kanda na baadaye fainali itakayochezwa kuanzia Septemba 7-14
mwaka huu jijini Dar es Salaam ikishirikisha mikoa 16 itakayokuwa imefanya
vizuri katika ngazi ya kanda.
Kila mkoa utapata fulana 25 na mipira mitatu ikiwa ni sehemu ya
maandalizi ya timu zao kwa ajili ya michuano hiyo ngazi ya kanda itakayomazika
Septemba 6 mwaka huu.
Kanda hizo
ni Mwanza itakayokuwa na timu za mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma, Mara, Mwanza,
Shinyanga, Simiyu na Tabora. Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Singida
inaunda Kanda ya Arusha.
Zanzibar
itakuwa na Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na mikoa miwili ya Unguja wakati Kanda
ya Dar es Salaam ina Ilala, Kinondoni, Lindi, Mtwara, Temeke na mkoa mmoja wa
Unguja.
Kanda ya Mbeya inaundwa na
Iringa, Katavi, Mbeya, Njombe, Rukwa na Ruvuma wakati Dodoma, Morogoro, Pwani
na Tanga zinaunda Kanda ya Morogoro.
Mwanza
itatoa timu nne kucheza hatua ya fainali wakati kanda nyingine za Arusha timu
mbili, Zanzibar (2), Mbeya (3) na Kanda ya Morogoro itaingiza timu mbili.
Wakati huo huo, semina ya
makocha 32 wa timu za mikoa zitakazoshiriki michuano ya U15 FIFA Copa Coca-Cola
iliyokuwa ikiendeshwa na mkufunzi Govinder Thondoo kutoka Mauritius inafungwa
leo (Agosti 16 mwaka huu) saa 9 alasiri kwenye ukumbi wa Msimbazi Center, Dar
es Salaam.
RAMBIRAMBI MSIBA WA MWANDISHI GRACEMO BAMBAZA
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha aliyekuwa
mwandishi wa habari za michezo wa Radio ABM ya Dodoma, Gracemo Bambaza
kilichotokea Agosti 14 mwaka huu katika Hospitali ya Ocean Road, Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa katika
sekta ya habari na mpira wa miguu kwani Bambaza kwa kipindi chote akiwa
mwandishi alikuwa akifanya kazi nasi, hivyo mchango wake katika mpira wa miguu
tutaukumbuka daima.
Bambaza aliyezaliwa mwaka
1973 na ambaye pia aliwahi kufanya kazi katika vituo vya redio vya Wapo cha Dar
es Salaam na Pride cha Mtwara amesafirishwa jana (Agosti 15 mwaka huu) kwenda
Karagwe mkoani Kagera kwa ajili ya mazishi.
TFF tunatoa pole kwa familia
ya marehemu Bambaza, ABM Radio na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo
Tanzania (TASWA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki
kigumu cha msiba huo mzito.
Mungu aiweke roho ya
marehemu Bambaza mahali pema peponi. Amina
TIKETI MECHI YA YANGA, AZAM KUUZWA ASUBUHI
TIKETI MECHI YA YANGA, AZAM KUUZWA ASUBUHI
Tiketi kwa ajili ya mechi ya
Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Azam itakayochezwa kesho (Agosti 17 mwaka huu)
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitaanza kuuzwa saa 3 asubuhi.
Vituo vitakavyouza tiketi
hizo Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers
ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live
Mbagala na BMM Barber Shop iliyoko Sinza Madukani.
Katika vituo
hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari yote yanayouza tiketi
yatahamia uwanjani saa 7 kamili mchana.
Viingilio
katika mechi hiyo ni sh. 7,000 kwa viti vya rangi ya kijani na bluu wakati viti
vya rangi ya chungwa ni sh. 10,000. Watakaiongia viti vya VIP C watalipa sh.
15,000, viti vya VIP B ni sh. 20,000 wakati VIP A watalipa sh. 30,000.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF)
Subscribe to:
Posts (Atom)