Mkutano Mkuu wa Marekebisho ya Katiba ya
klabu ya Simba umepangwa kufanyika Machi 16 mwaka huu badala ya Machi
23 kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali.
Uamuzi wa kurudisha nyuma tarehe ya
mkutano huo ulifikiwa jana (Jumatano), katika kikao cha Kamati ya
Utendaji ya Klabu kilichokutana usiku Makao Makuu ya Klabu, Mtaa wa
Msimbazi, jijini Dar es Salaam.
Kamati ya Utendaji ya Simba imefikia
uamuzi huo kufuatia maelekezo kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
iliyowataka wanachama wake wote mpaka kufikia Machi 20 mwaka huu wawe
wameshazifanyia marekebisho katiba zao kwa kuweka kipengele
kinachoitambua Kamati za Maadili.

Mbali na kipengele hicho mkutano huo pia
utajadili mapendekezo yote ya marekebisho ya katiba yaliyowasilishwa
kwa uongozi ili kujadiliwa na kutolewa maamuzi.
Uongozi wa Simba unawataka wanachama wake kujitokeza kwa wingi siku hiyo kushiriki katika zoezi hilo kwa maslahi ya klabu yao.
Kwa sasa uongozi unafanya mipango ya
kutafuta mahali pazuri utakapofanyika mkutano huo na mara baada ya
kupatikana basi uongozi utawatangazia wanachama wake.
Asha Muhaji
Ofisa Habari, Simba Sports Club