Thursday, February 13, 2014

TWIGA STAR YAFIKA SALAMA LUSAKA ZAMBIA.

Kikosi cha wachezaji 19 wa Twiga Stars kimetua Lusaka, Zambia leo (Februari 13
mwaka huu) huku Kocha Mkuu Rogasian akiahidi ushindani kwenye mechi dhidi
ya wenyeji itakayochezwa Uwanja wa Nkoloma.
Kocha Kaijage aliwaambia waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kenneth Kaunda mara baada ya kikosi chake kutua kwa ndege ya
Fastjet saa 3.30 asubuhi kwa saa za Zambia kuwa wamekuja kushindana, na si kushiriki.
Twiga Stars ambayo mara ya mwisho ilikutana na Zambia kwenye michuano ya
COSAFA miaka miwili iliyopita na kuibuka na ushindi imefikia hoteli ya Golden
Peacock, na katika uwanja wa ndege ilipokewa na viongozi wa Chama Soka
Zambia (FAZ) na Ofisa Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia, Jeswald Majuva.
Timu hiyo leo saa 9 alasiri kwa saa za Zambia ambapo Tanzania ni saa 10 jioni
itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Nkoloma ambao ndiyo utakaotumika kwa
mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) itakayochezwa kesho.
Wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho ni Amina Ali, Anastazia Katunzi, Asha
Rashid, Donisia Minja, Esther Chabruma, Etoe Mlenzi, Everine Sekikubo, Fatuma
Issa, Fatuma Makusanya, Fatuma Mwisendi, Fatuma Omari, Happiness Mwaipaja,
Maimuna Mkane, Mwapewa Mtumwa, Sherida Boniface,Sophia Mwasikili, Therese
Yona, Vumilia Maarifa na Zena Said.