Timu ya Nigeria (Flying Eagles)
imewasili nchini kwa ajili ya mechi ya michuano ya Afrika kwa vijana
wenye umri chini ya miaka 20 dhidi ya Tanzania (Ngorongoro Heroes)
itakayochezwa Jumapili (Mei 11 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Flying Eagles yenye msafara wa watu 32
imewasili leo (Mei 8 mwaka huu) alfajiri kwa ndege ya Ethiopian Airlines
ambapo imefikia hoteli ya Sapphire. Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya
pili itafanyika kuanzia saa 10 kamili
jioni.
Nigeria inayofundishwa na kocha Manu
Garba itafanya mazoezi leo (Mei 8 mwaka huu) saa 10 jioni itafanya
mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa ambao ndiyo utakaotumika kwa mechi siku
ya Jumapili.
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh.
2,000 kwa sehemu zote wakati upande wa VIP itakuwa ni sh. 5,000. Tiketi
zitauzwa uwanjani siku ya mechi katika magari maalumu.
Ngorongoro Heroes ambayo katika raundi
ya kwanza iliitoa Kenya kwa jumla ya mabao 4-3 inaendelea kujinoa jijini
Dar es Salaam chini ya Kocha wake John Simkoko na Msaidizi wake Mohamed
Ayoub kujiweka sawa kwa mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu na washabiki
wa mpira wa miguu nchini.
Nigeria kama ilivyo kwa nchi nyingine 12
imeanzia moja kwa moja raundi ya pili kutokana na ratiba iliyopangwa na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Nchi hizo ni Afrika Kusini,
Angola, Benin, Burkina Faso, Cameroon, Gabon, Ghana, Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC), Mali, Misri, Morocco na Zambia.
MICHUANO YA BEACH SOOCER YAINGIA ROBO FAINALI
Michuano ya mpira wa miguu wa ufukweni
(beach soccer) inayoendeshwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) ikishirikisha vyuo mbalimbali vya Dar es Salaam imeingia hatua ya
robo fainali.

Robo fainali hiyo inayoshirikisha timu
nane itachezwa Jumamosi (Mei 10 mwaka huu) kwenye ufukwe wa Escape One
uliopo Mik
ocheni kuanzia saa 5 asubuhi, huku Chuo cha Elimu ya Biashara
(CBE) na Taasisi ya Ustawi wa Jamii (SWI) zikicheza robo fainali ya
kwanza.
Chuo Kikuu cha Ardhi (AU) na Chuo cha
Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere watcaheza robo fainali ya pili kuanzia saa
6 kamili. Saa 8 kamili itaanza robo fainali ya tatu itakayozikutanisha
Taasisi ya Uhasibu (TIA) na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).
Robo fainali ya mwisho itakayoanza saa 9
kamili itakuwa kati ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na
Chuo cha Utumishi Magogoni. Washindi watacheza nusu fainali Jumapili
(Mei 11 mwaka huu) kwenye ufukwe huo huo.
Mechi za kutafuta mshindi wa tatu, na ile ya fainali zitachezwa kwenye ufukwe huo huo wikiendi ya Mei 17 mwaka huu.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)