Monday, December 1, 2014

WAZIRI WA FEDHA AWATAKA WAHADHIRI WA VYUO KUTOA ELIMU WA WANAFUNZI KULINGANA NA SOKO LA AJIRA

 
WAZIRI wa fedha Saada Mkuya amewataka wahadhiri wa vyuo mbalimbali nchini kutoa elimu kwa wanafunzi kulingana na soko la ajira ikiwa ni pamoja na fani inayoendana na cheti alichopata ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.
Waziri Mkuya ameyabainisha hayo kwenye mahafali ya 12 ya taasisi ya uhasibu (TIA) kampasi ya Mbeya yaliyofanyika katika viwanja vya taasisi hiyo mjini Mbeya ambapo waziri Mkuya aliwakilishwa na mkuu wa wilaya ya Mbeya dokta Norman Sigala.
Amesema kuwa hivi sasa kuna ushindani wa vyuo na ukosefu wa ajira nchini hivyo ni vema wahadhiri wakatoa wanafunzi wenye sifa kulingana na vyeti wanavyopata ili kukidhi soko la ajira ikiwa ni pamoja na kujiajiri wenyewe na sio kusubiri kuajiriwa.
Ameongeza kuwa wajibu wa vyuo ni kuandaa watalaam mbali mbali ili waweze kutumikia taifa na kukidhi haja ya nchi katika kujiletea maendeleo kwa wahitimu kufuata walitofundishwa madarasani na kutumia taaluma yao kupambana na changamoto zilizopo uraiani.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji mkuu wa Tasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Dokta Joseph Kihanda,amesema katika mwaka wa masomo 2013/2014 jumla ya wanafunzi 1960 wakiwemo wanawake 947 na wanaume 1013 wamehitimu katika fani za cheti cha awali, Stashahada na stashahada ya uzamili katika kampasi ya Mbeya.

ATHUMANI IDD CHUJI AWEKA WAZI KUU YEYE NI JEMBE KULIKO MBRAZIL EMRSON.

Athumani Idd Chuji  Kiungo mkabaji wa zamani wa Yanga, amesema kuwa uwezo wake kamwe hauwezi kuulinganisha na Mbrazili Emerson Roque ambae ni kiungo mpya wa timu hiyo.
Emerson tayari yuko jijini Dar es Salaam ambapo tayari ameanza mazoezi na timu ya Yanga.
Chuji alitupiwa viragoooo na Yanga katika usajili wa msimu huu wa Ligi Kuu Bara baada ya mkataba wake kumalizika kabla ya kwenda Oman kwenye majaribio na kurejea nchini kwa kile kilichoelezwa kushindwa, akiwa na Betram Mwombeki na Mkenya, Jerry Santo.

Hata hivyo Chuji kwa sasa yupo katika timu ya Mwadui FC ya shinyanga inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ambapo ameweka wazi kuwa yeye ni jembe kuliko Emerson.

TAIFA STARS MABORESHO YAINGIA KAMBI

Kikosi cha Taifa Stars Maboresho kimeingia kambini leo (Desemba 1 mwaka huu) Bulyanhulu mkoani Shinyanga kujiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi itakayochezwa Desemba 9 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Ikiwa chini ya Kocha Mart Nooij, Stars Maboresho itapiga kambi mkoani humo hadi Desemba 6 mwaka huu ambapo itarejea jijini Dar es Salaam tayari kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa.

Wachezaji walioingia kambini ni Abubakar Ally (Coastal Union), Abubakar Ally Mohamed (White Bird), Aishi Manula (Azam), Andrew Vicent (Mtibwa Sugar), Atupele Green (Kagera Sugar), Edward Charles (Yanga) na Emmanuel Semwanda (African Lyon).

Gadiel Michael (Azam), Hashim Magoma (Stand United), Hassan Banda (Simba), Hassan Mwasapili (Mbeya City), Joram Mgeveke (Simba), Kassim Mohamed Simbaulanga (African Lyon), Kelvin Friday (Azam) na Makarani Ally (Mtibwa Sugar).

Miraji Adam (Simba), Mohamed Hussein (Simba), Muzamir Ally (Mtibwa Sugar), Omari Nyenje (Ndanda), Pato Ngonyani (Yanga), Rashid Mandawa (Kagera Sugar), Said Hamisi (Simba), Salim Hassan Mbonde (Mtibwa Sugar) na Shiza Ramadhan (Mtibwa Sugar).

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaishukuru kampuni ya kuchimba madini ya Acacia Mining PLC (zamani African Barrick Gold PLC) kwa kufadhili kambi ya Stars kupitia mgodi wa Bulyanhulu.


IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

Sunday, November 30, 2014

BENO NJOVU AWASHUKURU WANACHAMA WA CLUB YA YANGA

Katibu Mkuu wa Yanga Beno Njovu ambaye anamalizia muda wake kuitumikia Timu ya yabga amesema anawashukuru wanachama na mashabiki wa klabu hiyo.

Njovu amesema anawashukuru kwa ushirikiano wao kwa kipindi chote alichokuwa Jangwani.

Njovu amesema yanga ni klabu kubwa, changamoto ni nyingi sana. Lakini nawashukuru wanachama na mashabiki kwa ushirikiano wao.

Hata hivyo amesema ataendelea kuwa mwanachama wa Yanga tena mwaminifu. Nimejifunza mengi, lakini sasa ni wakati wa kukabili changamoto nyingine.

Njovu amekuwa mmoja wa makatibu wa Yanga waliofanya vizuri katika kipindi wakiwa madarakani.

Ameamua kutoongeza mkataba baada ya ule aliokuwa nao kwisha muda wake.

Friday, November 28, 2014

TFF YAKIRI KUFANYA MAKOSA KURUHUSU KUFUNGULIWA DIRISHA DOGO LA USAJILI.


Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekiri kufanya makosa kuruhusu kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili kabla ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

VPL ilisimama kwa wiki saba Novemba 9 baada ya kuchezwa kwa mechi 49 za raundi ya kwanza hadi ya saba kupisha usajili wa dirisha dogo, mashindano ya Kombe la Uhai yanayoshirikisha Timu B za klabu za Ligi Kuu na michuano ya Kombe la Chalenji.
TFF ilifungua dirisha dogo la usajili Novemba 15 na litafungwa Desemba 15 huku mechi za raundi ya nane hadi ya 13 ya mzunguko wa kwanza wa VPL bado hazijachezwa, hivyo kutoa mwanya kwa baadhi ya wachezaji watakaozihama timu zao kipindi hiki cha usajili kucheza mechi tatu dhidi ya timu moja.


Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa amekiri shirikisho hilo kujisahau katika suala hilo lakini akasisitiza kuwa hakuna tatizo kubwa mchezaji kucheza mechi tatu dhidi ya timu moja.
Mwesigwa amesema haijawahi kutokea hapa kwetu (Tanzania), tumejifunza kitu lakini mchezaji kucheza mechi tatu dhidi ya timu moja VPL haina tatizo, tatizo kubwa ni mchezaji kusajiliwa na zaidi ya timu mbili msimu mmoja. Hili linakatazwa kikanuni.

Kiungo mkongwe wa Simba Amri Kiemba amejiunga na Azam FC kwa mkopo huku klabu hiyo ya Msimbazi ikiwabana wanalambalamba wasimtumie katika mechi zinazozikutanisha timu hizo mbili msimu huu.
TFF kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Mshindano, Boniface Wambura imepinga vikali uamuzi huo wa Simba kwa kuwa kanuni zinamruhusu mchezaji huyo kukipiga dhidi ya timu iliyomtoa kwa mkopo kwenda timu nyingine, hata hivyo.
Mchezaji wa Ndanda FC aliyecheza dhidi ya Azam FC msimu huu, akisajiliwa Simba atacheza dhidi ya Azam mara tatu katika mechi za msimu mmoja wa ligi kuu, ikiwa ni mfano wa kilichokosewa na TFF kuruhusu dirisha dogo la usajili msimu huu lifunguliwe ilhali mechi za mzunguko wa kwanza bado hazijakamilika.

CECAFA YASEMA BADO WANAHANGAIKIA MICHUANO YA CHALLENGE CUP KUFANYIKA

BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limesema bado linahangaikia kufanyika kwa michuano ya Kombe la Challenge mwaka huu.

Meneja wa Vyombo vya Habari wa CECAFA, Rogers Mulindwa amesema leo kwamba,  michuano ya Challenge ambayo awali ilikuwa ifanyike Ethiopia, lakini ikajivua uenyeji, bado ipo kwenye uwezekano wa kufanyika.Kamati Kuu ya CECAFA chini ya Mwenyekiti, Mhandisi Leodgar Tenga na Katibu Mkuu, Nicholas Musonye bado inafanyia kazi uwezekano wa kuhakikisha michuano hiyo inafanyika mwaka huu,” amesema Mulindwa.
Mganda huyo amesema kwamba  CECAFA baadaye itatoa taarifa rasmi juu ya mustakabali wa mashindano ambayo hufanyika mwishoni mwa Novemba hadi mwanzoni mwa Desemba.
Nchi wanachama wa CECAFA ni Sudan, Ethiopia, Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Somalia, Eritrea, Djibouti, Zanzibar na Sudan Kusini.

KLOPP KOCHA WA DORTMUND ASEMA MASHABIKI WA ARSENAL KUWA KIPIGO CHA 2-0 CHA UEFA HAWAWEZI KUPATA KAZI

MENEJA wa klabu ya Brussia Dortmund, Jurgen Klopp ametania kuwa mashabiki wa Arsenal hawatamuhitaji tena baada ya kuona timu yake ikitandikwa mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya juzi.
Klopp amekuwa akihusishwa na tetesi za kuchukua mikoba ya kionoa Arsenal katika wiki kadhaa zilizopita baada ya kuzuka msukumo kwa Arsene Wenger kufuatia kuanza vibaya msimu wa Ligi Kuu. 
Kocha huyo amekiri hivi karibuni kuwa anadhani anaweza kumudu kuhamia katika Ligi Kuu kama akiamua kuondoka Dortmund lakini sasa anadhani nafasi yake ya kutua Arsenal imetoweka. 

Akihojiwa Klopp amesema hafikirii baada ya kiwango cha Dortmund walichokionyesha katika Uwanja wa Emirates kama mashabiki wa Arsenal watamuhitaji. 
Klopp aliteuliwa kuwa kocha wa Dortmund kuanzia mwaka 2008 na kuisaidia timu hiyo kushinda mataji mawili ya Bundesliga, Kombe la Ujerumani, Supercup na kutinga fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.