Sunday, July 14, 2013

Coastal Union yanasa saini ya Udula wa Bandari ya Kenya


Na Paul Mkai,Tanga.
UONGOZI wa Klabu ya Coastal Union ya Tanga umesema tayari umeshamalizana na aliyekuwa mshambulizi wa timu ya Bandari ya Kenya,Christian Udula kwa mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kuichezea timu kwenye msimu mpya ambao utaanza Agosti mwaka huu.

Akizungumza na Blogg hii,Katibu Mkuu wa timu ya Coastal Union ya Tanga,Kassim El Siagi alisema baada ya kumalizina na mchezaji huyo anatarajiwa kutua mkoani Tanga wiki ya leo akiwa na mchezaji mwengine wa timu hiyo Jerry Santos.

Siagi alisema msimu huu wamedhamiri kufanya usajili wa nguvu ambao utaifanya timu hiyo kuwa tishio kwenye mechi zao za Ligi kuu ya Tanzania bara kwani malengo yao ni kuchukua ubingwa wa mashindano hayo makubwa hapa nchini.

Aidha alisema timu hiyo itacheza mechi mbalimbali za majaribio nchini Kenya na timu za Sofapaka,Bandari na Goromahia lengo likiwa ni kukipa makali kikosi hicho ambacho kinatarajiwa kuwa tishio.

Katibu huyo aliwataka wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kuendelea kujitokeza kuisapoti timu hiyo ili iweze kutimiza azma yao waliyojiwekea kwenye michuano hiyo.

Mwisho.

Friday, July 12, 2013

KAMPUNI YA MADUKA NCHINI BRAZIL WATISHIA KWENDA MAHAKANI KUHUSU USAJILI NEYMAR

Kampuni ya DIS inayomiliki maduka makubwa nchini Brazil na ambao wanamiliki asilimia 40 ya haki za usajili wa Neymar wametishia kwenda mahakamani kuhusiana na mgao wao kwa nyota huyaa o katika usajili wake kwenda Barcelona. Kampuni hiyo inayoendeshwa na Idi Sonda imedai kuwa na haki ya kupata fedha zaidi juu ya makubaliano ya ziada kati ya klabu ya Santos na Barcelona ambayo yako nje ya ada ya uhamisho wake ambayo ilifikia kiasi cha euro milioni 57. Mkurugenzi Mtendaji wa DIS, Roberto Moreno ameomba kupewa taarifa kamili ya hati ya uhamisho wa Neymar kwenda Barcelona ili kupata ufafanuzi kuhusu malipo ya baadae watakayopewa Santos. Moreno amesema mpaka kipindi hicho hawajaonyeshwa hati yoyote, hivyo atafunga safari kwenda makao makuu ya Santos kufuatilia hati hiyo na baada ya hapo wataamua kama watahitaji kwenda mahamani. Hatua ya kampuni hiyo imekuja kufuatia taarifa zilitolewa na vyombo vya habari nchini humo kwamba Santos watapata nyongeza ya euro milioni mbili kama mchezaji huyo atakuwemo katika orodha ya wachezaji watatu kwenye tuzo ya Ballon d’Or kwenye kipindi cha miaka mitano ijayo.

FIFA YA FUATILIA KWA KARIBU KASHFA YA UPANGAJI MATOKEO

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA linafuatilia kwa karibu kashfa ya upangaji matokeo inayozikabili vilabu viwili vya soka vya ridhaa nchini Nigeria iliyotokea wiki iliyopita. Katika matokeo ambayo yanaonekana kama ya mchezo wa kriketi, klabu ya Plateau United Feeders iliibugiza Akurba FC kwa mabao 79-0 wakati Police Machine wao waliitandika Bubayaro FC kwa mabao 67-0 mwishoni mwa wiki iliyopita. Hatua uchunguzi kwa vilabu hivyo imekuja kutokana na timu hizo kuhitaji matokeo ya aina hiyo ili waweze kupanda daraja. Ambapo katika taarifa yake FIFA imedai kuwa inafuatilia tukio hilo la tmu hizo za Nigeria kwa karibu ili kuona jinsi gani Shirikisho la Soka la nchi hiyo, NFF litatatua tatizo hilo. FIFA inafanya hivyo kwa kutambua kuwa suala hilo ni la ndani hivyo NFF ina wajibu wa kufanya uchunguzi na kuchukua hatua zinazostahiki kama ikigundulika aina yoyote ya udanganyifu katika mechi hizo.

TAIFA STARS SASA MMEIVA KUPAMBANA- TENGA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kikosi cha Taifa Stars sasa kina uwezo wa kushindana katika mashindano yoyote, kwani tayari kimeiva.
Akizungumza na wachezaji wa timu hiyo kambini kwao hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam, Rais Tenga aliwaambia kuwa kiwango walichoonesha kwenye mechi zilizopita za mchujo za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco na Ivory Coast kimethibitisha hilo.
“Kiwango mlichoonyesha katika mechi hizo kila Mtanzania anayewafuatilia amekiona, hivyo hatuna shaka kuwa mtatuwakilisha vizuri kwenye mechi ya kesho dhidi ya Uganda,” amesema Rais Tenga na kuwataka kupigana kwa ajili ya Tanzania.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kesho (Julai 13 mwaka huu) saa 9 kamili alasiri Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itacheza na Uganda (The Cranes) katika mechi ya kwanza ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza Fainali za CHAN zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Rais Tenga amesema TFF, mdhamini Kilimanjaro Premium Lager, Kamati ya Ushindi na Watanzania kwa ujumla wanawaunga mkono kwani wamekuwa wakiboresha kiwango chao kila wanavyozidi kucheza mechi tangu wake chini ya Kocha Kim Poulsen, Mei mwaka jana.
Wakati huo huo, Rais Tenga ameahidi kumpatia tiketi ya kwenda Uganda kwenye mechi ya marudiano mshabiki Wiseman Mwakyusa Luvanda anayetembea kwa miguu kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam kushuhudia mechi ya kesho.
“Kama ni kweli anakuja kwa kutembea, huyu ameonyesha kiwango kikubwa cha uzalendo kwa timu ya Taifa, nitampatia tiketi ya kwenda Kampala kuishangilia Taifa Stars kwenye mechi ya marudiano,” amesema Rais Tenga.

POULSEN, MICHO WATABIRI MECHI KALI
Makocha wa timu hizo Kim Poulsen wa Taifa Stars na Sredojvic Micho wa The Cranes wamesema mechi ya kesho itakuwa ngumu kwa vile kila mmoja amejiandaa kuhakikisha anafanya vizuri.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari leo, makocha wote waliezea ubora wa wapinzani wao, lakini wakasisitiza kuwa wanaingia uwanjani kuhakikisha wanashinda ili kujiweka katika mazingira mazuri kwa ajili ya mechi ya marudiano itakayochezwa Kampala wiki mbili zijazo.
Kim alisema Uganda ndiyo inayoongoza kwa ubora wa viwango vya FIFA katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo ni changamoto kwao ingawa wachezaji wake tayari wamejipanga vizuri kwa ajili ya mechi hiyo.
Naye Micho aliyefuatana na nahodha wake Hassan Wasswa alisema Taifa Stars imekuwa ikifanya vizuri tangu iwe chini ya Kim, na itakuwa na wachezaji tisa wa kikosi cha kwanza kinachocheza mechi za mchujo za Kombe la Dunia wakati kwa upande wake atakuwa na wachezaji wawili tu.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Thursday, July 11, 2013

DROGBA ATANGAZA KUJENGA HOSPITAL 5 ZA KINA MAMA NA WATOTO"NCHINI IVORY" COAST


Didier Drogba mshambuliaji nyota wa zamani wa Chelsea ametangaza kuwa atajenga Hospitali 5 ili kuwasaidia wakina Mama na Watoto huko Nchini Ivory Coast kwa gharama ya Dola Milioni 5.
Uamuzi huu umetangazwa huko Mjini Abidjan na Katibu wa Didier Drogba Foundation, Guy Roland Tanoh, ambae amesema itajengwa Hospitali moja katika Miji mitano ya Ivory Coast ambayo ni Abidjan, Yamoussoukro, Man, Korhogo na San Pedro.
Kwenye Tafrija huko London tulichangisha na kukusanya Dola Milioni 4 na zilizobaki si tatizo ili kukamilisha Mradi huu ambao uko moyoni kabisa mwa Drogba.”
Tanoh pia ametoboa pia kuwa Taasisi hiyo ya Drogba imeshatoa misaada kwa Watoto yatima na wale ambao wapo kwenye mazingira magumu.
Taasisi ya Didier Drogba ilianzishwa Mwaka 2007 na ilipanga kujenga Hospitali yenye gharama ya Pauni Milioni 3 lakini hadi leo ilikuwa haijajengwa na Tanoh hakufafanua kama Hospitali hiyo ni moja ya hizo tano zitakazojengwa.
Wakati huo, Drogba, mwenye Miaka 35 hivi sasa na ambae anachezea Klabu ya Turkey Galatasaray, alisema ujenzi wa Hospitali hiyo utatokana na malipo ya Picha na Matangazo yake na Kampuni ya Pepsi.

TIMU YA AFRICAN LYON ILIYOSHUKA DARAJA YAPATA HASARA YA SH.180.3

TIMU ya soka ya African Lyon ya jijini Dar es Salaam imetangaza hasara ya sh. milioni 180.3 kutokana na ushiriki wake katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Lyon ni miongoni mwa timu tatu zilizoshuka daraja kutoka katuika ligi hiyo kubwa ya soka nchini, nyingine ni Toto African na Polisi Moro.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Meneja wa Fedha wa Lyon, Ibrahim Salim, alisema timu yao imetumia zaidi ya sh. 388,614,500 kwa ajili ya maandalizi hadi michezo yake.
Salim amesema katika makusanya na matumizi yao, walilazimika kutumia kiasi cha sh. milioni 268.09 katika mzunguko wa kwanza, kabla ya kutumia sh. 123.6.
"Katika matumizi yote haya, fedha ambayo tumeiingiza kama klabu kupitia viingilio na vyanzo vingine ni sh. milioni 207.6, na hapo ndipo unapopata tofauti ya sh. milioni 180.3, ambayo ni hasara," Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Lyon, Rahim Kangezi, alisema soka ya Tanzania inaendeshwa kwa hasara huku wenye dhamana ya kusaidia wakiwa hawatendi haki kwa baadhi ya vipengele.
Kangezi alisema timu yake imeingia katika hasara ya sh. milioni 180.3 kutokana na uendeshaji, lakini bado wameshuka daraja, huku akisisitiza kuwa hakuna anayeshutumiwa kwa kushuka kwa timu hiyo"Unaweza kuona changamoto ambayo tunakumbana nayo katika uendeshaji wa taasisi kamam a hizi, tunapopiga kelele kwa wadhamini kutuwahishia fedha tunamaanisha."Angalieni mfano mdogo kwa fedha za wadhamini (Vodacom), ambazo awamu ya mwisho zimetufikia Mei mwaka huu, tukiwa tumebakiza mechi moja ya Ligi Kuu, sasa zingetusaidia katika nini? Alihoji mmiliki huyo.
Akizungumzia kuhusu uendeshwaji wa Ligi Kuu na changamoto walizokutana nazo, Kangezi alisema bado hakujakuwa na usimamizi mzuri katika kuhakikisha kuwa ligi hiyo inakuwa bora.
Katika hatua nyingine, Kangezi amesema timu yake inajivunia mafanikio waliyochangia kusogeza maendeleo ya soka nchini kutokana na kutoa nafasi kwa Mrisho Ngassa kwenda kujaribu soka ya kulipwa na kucheza katika kikosi cha Seattke Soundowns dhidi ya Manchester United.
"Tulifanikiwa pia kuileta timu kubwa ya Ligi Kuu ya Brazil (Atletico Parenese) kwa ziara ya kimichezo nchini, tulitoa wachezaji watano kwa ajili ya kujaribu soka ya kulipwa sambamba na kufanya semina mbili juu ya uongozi wa michezo," aliongeza.