Monday, September 2, 2013

WENGER AFUNJA UKIMYA

KLABU ya Arsenal imekubali kutoa kitita cha paundi milioni 42.4 kwa ajili ya kumsajili kiungo Mesut Ozil kutoka Real Madrid ya Hispania. Ozil mwenye umri wa miaka 24 naye amefikia makubaliano binafsi na klabu hiyo lakini anatakiwa kufanyiwa vipimo vya afya kabla Arsenal hawajakamilisha usajili huo ambao utavunja rekodi ya klabu hiyo. Kwasasa Ozil yuko katika majukumu ya kimataifa hivyo vipimo vya afya atafanyiwa nchini kwao Ujerumani. Arsenal pia wako katika mazungumzo na Chelsea kwa ajili ya kumsajili kwa mkopo mshambuliaji Demba Ba huku wakiwa tayari wamekamilisha usajili mwingine wa mkopo kwa kipa wa Palermo Emiliano Viviano.

ILALA, KASKAZINI UNGUJA ZAANZA COPA KWA SARE

Timu za Ilala na Kaskazini Unguja zimetoka sare ya mabao 3-3 katika moja ya mechi za ufunguzi za michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 iliyoanza leo (Septemba 2 mwaka huu) katika vituo mbalimbali nchini.


Wafungaji wa Ilala katika mechi hiyo iliyochezwa asubuhi Uwanja wa Tamco ulioko Kibaha, Pwani yalifungwa na Ally Shaban (mawili) wakati lingine lilifungwa na Haruni Said. Mabao ya Kaskazini Unguja yalifungwa na Jecha Ally (mawili) na Shehe Ally.


Katika kituo cha Mbeya, Njombe imeanza vizuri baada ya kuifunga Katavi mabao 2-1. Mabao ya washindi yalifungwa na Rackson Mligo dakika ya 13 wakati lingine lilifungwa na Kelvin Gama dakika kumi kabla ya filimbi ya mwisho.


Bao la Katavi katika mechi hiyo iliyochezwa uwanja wa Sekondari ya Iyunga lilifungwa dakika ya 15 kupitia Joseph Edward.


Wenyeji Mbeya wameitandika Ruvuma mabao 3-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Iyunga. Mabao ya washindi yalifungwa na Joel Mwasambungu dakika 9 wakati mengine yalifungwa na Jackson Mwaibambe dakika ya 18 na 55.  


Kesho (Septemba 3 mwaka huu) katika kituo hicho kutakuwa na mechi kati ya Rukwa na Katavi itakayochezwa saa 4 asubuhi wakati Iringa na Ruvuma zitaumana kuanzia saa 2 asubuhi.


Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

HENRY JOSEPH AITWA TAIFA STARS

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amemjumuisha mchezaji Henry Joseph wa Simba kwenye kikosi chake kinachojiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Gambia itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu jijini Banjul.

Tayari Joseph amesharipoti kwenye kambi ya timu hiyo iliyoko hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam. Taifa Stars ambayo iko chini ya udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager imeingia kambini tangu Agosti 29 mwaka huu, na leo jioni itafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

Programu ya timu hiyo inaonesha kuwa kesho (Septemba 3 mwaka huu) itafanya mazoezi yake asubuhi na jioni kwenye uwanja huo huo wa Kumbukumbu ya Karume.

Wakati huo huo, kesho (Septemba 3 mwaka huu) saa 6 kamili mchana Kocha Kim Poulsen atakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari.

LIUNDA KUTATHMINI WAAMUZI CL
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Leslie Liunda wa Tanzania kuwa mtathmini wa waamuzi kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Coton Sport ya Cameroon na Esperance ya Tunisia.

Mechi hiyo ya kundi B itachezwa Septemba 21 mwaka huu kwenye Uwanja wa Omnisport Roumdeadjia mjini Garoua, Cameroon. Kamishna atakuwa Bema Doumbia wa Ivory Coast.

Waamuzi wanatoka Madagascar wakiongozwa na Hamada Nampiandraza. Wasaidizi wake ni Jean Eric Pierre Andrivoavonjy, Ferdinand Velomanana Linoro na Bruno Marie Andrimiharisia.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Friday, August 16, 2013

MOURINHO ASEMA NATAKA KUWEKA POA FAMILIA YA WANACHELSEA

Meneja wa Chelsea, Jose Mourinho amesema  lengo kuu anataka kurudisha upya familia ya wadau wa Chelsea ambayo ilivunjika baada ya kocha aliyeondoka Rafa Benitez kumrithi kocha kipenzi cha mashabiki Roberto Di Matteo na kusababisha tofauti kwa mashabiki wa klabu hiyo.
Chelsea waliingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe baada ya kumfukuza kocha aliyewapa ubingwa wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, na hata baada ya Benitez kushinda kombe la Uropa haikumnusuru kufungashiwa virago.
Ambapo mmiliki Roman Abramovich alimgeukia tena kwa mara ya pili  Mourinho majira haya ya kiangazi na amefanikiwa kumrejesha.
Kocha huyo mwenye Umri wa miaka 50, raia wa Ureno aliliambia gazeti la The Sun: “Nawataka kuwa nasi kama familia ya Chelsea-familia ambayo kwa muda fulani mwaka jana ilionekana kuvunjika”.

SUAREZ ARUDI NYUMBANI ANFIELD BAADA YA MISUKOSUKO YA HAPA NA PALE YA KUTAKA KUONDOKA"

Mshambuliaji nyota Luis Suárez leo amerudi kikosini huko Anfield na kuanza Mazoezi tena pamoja na Kikosi cha Kwanza cha Timu ya Liverpool baada ya kuzuiwa kufanya hivyo na Meneja Brendan Rodgers kwa kuishambulia Klabu kwa madai ya kuvunja ahadi ya kumruhusu ahame ikiwa haitafuzu kucheza UEFA CHAMPIONZ LIGI Msimu huu.
Jumanne iliyopita Suarez alilazimishwa kufanya Mazoezi peke yake na kutakiwa kuiomba Klabu radhi kwa kauli zake na inaaminika Mchezaji huyo ametii amri hiyo na ndio maana amerudishwa tena Mazoezini kwenye Kikosi cha Kwanza.
Suarez amekuwa akisinikiza kuihama Liverpool na Arsenal ilishatoa Ofa ya Pauni 40,000,001 kumnunua lakini Liverpool imekataa na kusisitiza Mchezaji huyo hauzwi.
Msimamo huo ulisisitizwa zaidi na Mmiliki mkuu wa Liverpool kutoka Marekani, John W Henry, ambae Wiki iliyopita alitamka Suarez hatauzwa kwa Arsenal au kwa Klabu yeyote Ulaya.
Kwa sasa Suarez yupo kwenye Kifungo cha Mechi 10 alichopewa mwishoni mwa Msimu uliokwisha Mwezi Mei kwa kumng’ata meno Beki wa Chelsea Branislav Ivanovic kwenye Mechi na tayari ameshatumuikia Mechi 4 na bado 6.
Wakati huo huo, Liverpool imefanikiwa kukubaliana na Klabu ya Spain, Valencia, ili kumchukua Beki wao wa kushoto Aly Cissokho kwa Mkopo wa Msimu mmoja.
Meneja wa Liverpool Brendan Rodgers alikuwa akisaka Mchezaji wa pozisheni hiyo ili kuleta ushindani kwa Beki wake José Enrique na waliwahi kuwawania Lorenzo Melgarejo wa Benfica na Guilherme Siqueira wa Granada ili kujaza Nafasi hiyo.

KAMATI YASHERIA NA HADHI ZA WACHEZAJI YA TFF YATOA MAAMUZI KUHUSU NGASA"


KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imepitia usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom na kumuidhinisha Mrisho Ngasa kuchezea timu ya Yanga baada ya kukamilisha usajili wake.
Hata hivyo, Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa imebaini kuwa Ngasa alisaini mkataba mwingine Simba (katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam) ambapo anatakiwa kurejesha fedha alizopokea (sh. milioni 30) pamoja na fidia ya asilimia 50 (sh. milioni 15) ya fedha hizo kwa Simba.
Kamati pia imemfungia mechi sita za mashindano (kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii), na anatakiwa awe amelipa fedha hizo ndani ya kipindi hicho cha kukosa mechi hizo. Akishindwa, hataruhusiwa kucheza hadi atakapolipa fedha hizo.

Vilevile Kamati imepitia pingamizi zote zilizowasilishwa kuhusu usajili wa wachezaji, kukatiza mikataba ya wachezaji na kuzitaka klabu husika ziwe zimetatua masuala hayo hadi Alhamisi (Agosti 22 mwaka huu).
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni, Kamati imeagiza wasiruhusiwe kucheza hadi watakapopata Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) pamoja na vibali vya kufanya kazi nchini (work permits).
Kamati hiyo itakutana tena Ijumaa (Agosti 23 mwaka huu) ili kupata ripoti za pingamizi ilizoagiza ziwe zimefanyiwa kazi hadi Agosti 22 mwaka huu na kutoa uamuzi kwa pande ambazo hazikuafikiana.
Wakati huo huo: Kamati ya TFF kwa kuzingatia mamlaka iliyonayo katika kifungu cha 10(6) cha Kanuni za Uchaguzi za TFF inasogeza mbele tarehe ya uchaguzi wa TFF kutoka Oktoba 20 mpaka Oktoba 26 na 27 mwaka huu.
Sababu za kusogeza mbele uchaguzi ni kutokana na ukweli kuwa Oktoba 20 mwaka huu uongozi wa TFF utakuwa na shughuli nyingi za maandalizi ya mechi ya Simba na Yanga, na hivyo haitawezekana kusimamia shughuli za Mkutano Mkuu wa Uchaguzi kwa wakati mmoja na mchezo huo.
Siku ya mwisho ya kampeni itakuwa Oktoba 25 mwaka huu. Ukiondoa  mabadiliko hayo ya tarehe ya uchaguzi wa viongozi wa TFF, ratiba ya mchakato wa uchaguzi na itabaki kama ilivyotangazwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika mkutano wake na waandishi wa habari Agosti 24 mwaka huu.
Pia Kamati imeamua kuwa uchaguzi wa Bodi ya Ligi utabakia kuwa Oktoba 18 mwaka huu kama ilivyopangwa awali.
Kamati imesema inaamini wahusika wote watapokea vizuri mabadiliko hayo na inasikitika kwa usumbufu utakaosababishwa na mabadiliko hayo.




KAMATI YA UCHAGUZI KUJADILI SIMBA, YANGA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ili kufanya uamuzi wenye manufaa kwa washabiki wa mpira wa miguu baada ya tarehe ya uchaguzi aliyotangaza kuingilia na mechi ya watani wa jadi (Simba na Yanga) ya Ligi Kuu ya Vodacom.
Sekretarieti ya TFF imepokea maoni kutoka kwa wapenzi mbalimbali wa mpira wa miguu wakiomba matukio hayo mawili (Uchaguzi wa TFF na mechi ya Simba na Yanga) yafanyike katika siku tofauti.
Wakati Kamati ya Uchaguzi inatangaza uchaguzi kufanyika Oktoba 20 mwaka huu tayari ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom ilikuwa imeshatoka, na ikionesha kuwa timu ambazo zina historia ya kipekee katika mpira wa miguu zitacheza siku hiyo.
Sekretarieti imelazimika kumwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi kwa vile yeye na kamati yake ndiye wenye mamlaka ya kuitisha Mkutano wa Uchaguzi. Huko nyuma TFF imeshafanya mikutano huku kukiwa na mechi za timu ya Taifa (Taifa Stars), jambo ambalo liliwezekana kutokana na mikutano hiyo kuwa na ajenda moja tu.
Tayari Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Hamidu Mbwezeleni ameitisha kikao cha kamati yake kujadili barua hiyo ya sekretarieti.
COCA COLA YATOA MIPIRA 100, FULANA 800
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa shukrani kwa kampuni ya Coca Cola kwa kukabidhi fulana 800 na mipira 100 kwa ajili ya ngazi ya mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 15 ngazi ya mikoa yanayoanza Septemba Mosi mwaka huu.
Coca Cola ndiyo inayodhamini mashindano hayo yaliyoanzia ngazi ya wilaya ambapo mwaka huu yatachezwa kwa kanda na baadaye fainali itakayochezwa kuanzia Septemba 7-14 mwaka huu jijini Dar es Salaam ikishirikisha mikoa 16 itakayokuwa imefanya vizuri katika ngazi ya kanda.
Kila mkoa utapata fulana 25 na mipira mitatu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya timu zao kwa ajili ya michuano hiyo ngazi ya kanda itakayomazika Septemba 6 mwaka huu.
Kanda hizo ni Mwanza itakayokuwa na timu za mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Tabora. Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Singida inaunda Kanda ya Arusha.
Zanzibar itakuwa na Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na mikoa miwili ya Unguja wakati Kanda ya Dar es Salaam ina Ilala, Kinondoni, Lindi, Mtwara, Temeke na mkoa mmoja wa Unguja.
Kanda ya Mbeya inaundwa na Iringa, Katavi, Mbeya, Njombe, Rukwa na Ruvuma wakati Dodoma, Morogoro, Pwani na Tanga zinaunda Kanda ya Morogoro.
Mwanza itatoa timu nne kucheza hatua ya fainali wakati kanda nyingine za Arusha timu mbili, Zanzibar (2), Mbeya (3) na Kanda ya Morogoro itaingiza timu mbili.
Wakati huo huo, semina ya makocha 32 wa timu za mikoa zitakazoshiriki michuano ya U15 FIFA Copa Coca-Cola iliyokuwa ikiendeshwa na mkufunzi Govinder Thondoo kutoka Mauritius inafungwa leo (Agosti 16 mwaka huu) saa 9 alasiri kwenye ukumbi wa Msimbazi Center, Dar es Salaam.

RAMBIRAMBI MSIBA WA MWANDISHI GRACEMO BAMBAZA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari za michezo wa Radio ABM ya Dodoma, Gracemo Bambaza kilichotokea Agosti 14 mwaka huu katika Hospitali ya Ocean Road, Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa katika sekta ya habari na mpira wa miguu kwani Bambaza kwa kipindi chote akiwa mwandishi alikuwa akifanya kazi nasi, hivyo mchango wake katika mpira wa miguu tutaukumbuka daima.
Bambaza aliyezaliwa mwaka 1973 na ambaye pia aliwahi kufanya kazi katika vituo vya redio vya Wapo cha Dar es Salaam na Pride cha Mtwara amesafirishwa jana (Agosti 15 mwaka huu) kwenda Karagwe mkoani Kagera kwa ajili ya mazishi.
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Bambaza, ABM Radio na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Mungu aiweke roho ya marehemu Bambaza mahali pema peponi. Amina 

TIKETI MECHI YA YANGA, AZAM KUUZWA ASUBUHI
Tiketi kwa ajili ya mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Azam itakayochezwa kesho (Agosti 17 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitaanza kuuzwa saa 3 asubuhi.
Vituo vitakavyouza tiketi hizo Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala na BMM Barber Shop iliyoko Sinza Madukani.
Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari yote yanayouza tiketi yatahamia uwanjani saa 7 kamili mchana.
Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 7,000 kwa viti vya rangi ya kijani na bluu wakati viti vya rangi ya chungwa ni sh. 10,000. Watakaiongia viti vya VIP C watalipa sh. 15,000, viti vya VIP B ni sh. 20,000 wakati VIP A watalipa sh. 30,000.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)