Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limewalalamikia wana familia watano wa mpira wa miguu kwa Kamati
ya Maadili kuhusiana na udanganyifu katika mtihani wa utimamu wa mwili
wa waamuzi na usajili wa mchezaji Emmanuel Okwi.
Riziki Majala na Army Sentimea ambao ni
wakufunzi wa waamuzi, na Oden Mbaga na Samwel Mpenzu ambao ni waamuzi
wanadaiwa kughushi nyaraka kuhalalisha mtihani huo kinyume cha taratibu.
Naye Sabri Mtulla analalamikiwa na TFF
kwa madai ya kuidanganya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuwa
hakukuwa na pingamizi lolote juu ya usajili wa mchezaji Emmanuel Okwi
huku akijua wazi kuwa jambo hilo si kweli.
Kwa mujibu wa kanuni, malalamiko hayo
yamefikishwa kwenye Kamati ya Maadili ambayo itachunguza ili
kujiridhisha kama yana msingi au la. Ikibaini kuna kesi ndipo
walalamikiwa watafika mbele ya kamati hiyo.
TWIGA STARS, ZAMBIA KUCHEZA MACHI 2
Mechi ya pili ya raundi ya kwanza
kuwania Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Tanzania (Twiga
Stars) na Zambia (Shepolopolo) itachezwa Machi 2 mwaka huu Uwanja wa
Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
Twiga Stars tayari imeingia kambini
kujiandaa kwa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni.
Twiga Stars chini ya Kocha Rogasian Kaijage inafanya mazoezi yake kwenye
Uwanja wa Karume ambao ni wa nyasi za bandia kama ulivyo ule wa Azam
Complex.
Shepolopolo iliibuka na ushindi wa mabao
2-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Februari 14 mwaka huu kwenye
Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka.
Iwapo Twiga Stars itafanikiwa kuiondoa
Shepolopolo itacheza na mshindi wa mechi kati ya Botswana na Zimbabwe.
Zimbabwe ilishinda mechi ya kwanza ugenini.

Wachezaji wa Twiga Stars waliopo kambini
ni Amina Ali, Anastazia Katunzi, Asha Rashid, Donisia Minja, Esther
Chabruma, Etoe Mlenzi, Everine Sekikubo, Fatuma Issa, Fatuma Makusanya,
Fatuma Mustafa, Fatuma Mwisendi, Fatuma Omari, Flora Kayanda, Happiness
Mwaipaja, Maimuna Mkane, Mwajuma Abdallah, Mwapewa Mtumwa, Pulkeria
Charaji, Sherida Boniface, Sophia Mwasikili, Therese Yona, Vumilia
Maarifa na Zena Said.
STAND UNITED YAIKATIA RUFANI KANEMBWA JKT
Stand United ya Shinyanga imekata rufani
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikipinga Kanembwa JKT ya
Kigoma kuchezesha wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo kwenye
mechi ya kiporo iliyozikutanisha timu hizo.
Mechi hiyo namba 22 ya Ligi Daraja la
Kwanza (FDL) ilichezwa juzi (Februari 16 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Ali
Hassan Mwinyi mjini Tabora ambapo Kanembwa JKT iliibuka na ushindi wa
bao 1-0.
Katika rufani yake, Stand United inadai
kwenye mechi hiyo Kanembwa JKT ilichezesha wachezaji wanane
waliosajiliwa katika dirisha kidogo kinyume na maelekezo kutoka TFF kwa
timu hizo kuwa wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo hawawezi
kucheza mechi hiyo.
Wachezaji wanaodaiwa kusajiliwa dirisha
dogo na kucheza mechi hiyo ni Hamidu Juma, Ibrahim Shaban Issa, Joseph
Mlary, Lucas Charles Karanga, Raji Ismail, Salvatory Kulia Raphael, Seif
Ibrahim Zaid na Yonathan David Sabugowiga.
Dirisha dogo lilifunguliwa Novemba 15 na
kufungwa Desemba 15 mwaka jana, hivyo Stand United katika rufani yake
inaombwa ipewe pointi tatu na mabao matatu kwa Kanembwa JKT kuchezesha
wachezaji wasiostahili.
Awali mechi hiyo ilichezwa Novemba 2
mwaka jana Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, na kuvunjwa na mwamuzi
dakika ya 87 baada ya Kanembwa JKT kugomea pigo la penalti dhidi yao.
RAIS MALINZI AENDA KUJITAMBUSHA CAF
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameondoka leo (Februari 17 mwaka huu)
kwenye Cairo, Misri kujitambulisha kwa uongozi wa juu wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Akiwa Cairo, Rais Malinzi ambaye
alichaguliwa Oktoba 28 mwaka jana atakutana na Rais wa CAF, Issa Hayatou
pamoja na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Hicham El Amrani.
WATATU WAOMBEWA UHAMISHO WA KIMATAIFA
Wachezaji watatu wanaocheza mpira wa
miguu nchini Tanzania wameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ili
wakacheze katika nchi za Thailand na Ujerumani.
Mchezaji Khamis Mroki Jamal aliyekuwa na
timu ya Daraja la Kwanza ya Polisi Dar es Salaam ameombewa ITC na Chama
cha Mpira wa Miguu Thailand (FAT) ili akajiunge na Kabinburi ya nchini
humo.
Said Ali Nassor aliyekuwa akichezea FC
Turkey ya Zanzibar na Samuel Chuonyo wameombewa na ITC na Chama cha
Mpira wa Miguu Ujerumani (DFB) kwa ajili ya kujiunga na klabu ya VfB
Eichstatt.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) linafanyia kazi maombi hayo na mara taratibu zote zitakapokamilika
ikiwemo ridhaa ya klabu zao za hapa Tanzania itatoa ITC hizo.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)