UTANGULIZI
Kwa niaba ya mteja wetu, Emmanuel Arnold Okwi, napenda kutoa
maelezo kuhusu Uamuzi wa kihistoria katika soka la Tanzania ambao umefanywa na
Kamati ya Sheria na hadhi ya wachezaji ya TFF. Uamuzi huo ni wa kihistoria kwa
misingi ifuatayo:
MOSI: Ni mara ya Kwanza
katika historia ya soka la Tanzania ambapo Kamati inakaa kujadili haki ya
mchezaji dhidi ya klabu kubwa na hatimaye kuamua kwa manufaa ya mchezaji, tena
pasipo kupiga kura kwa misingi ya upenzi na unazi. Kamati ya Mwanasheria
Mashuhuri na mwenye Msimamo Bw. Richard Sinamtwa iliamua kustafsiri kanuni kwa
kufuata ushahidi uliopo na kwa haki kabisa pasipo kujiingiza katika mtego wa
kupiga kura kama ambavyo tumekua tukiiona huko nyuma.
PILI: Kamati
ikiongozwa na Mwenyekiti ilitumia busara ya hali ya juu kwa kukataa ombi la
Yanga la kutengua uteuzi wa Bw. Hans Pope katika Kamati hiyo. Ikumbukwe kuwa
Yanga ilileta hoja ya kumkataa Bw. Hans Pope kwa misingi ya mgongano wa
kimaslahi na kumtaka mwenyekiti atoe uamuzi juu ya suala hilo. Endapo
mwenyekiti angetoa maamuzi ya kumuondoa Hans Pope, basi angejiingiza katika
uvunjaji wa Katiba ya TFF kwasababu yeye sio mamlaka ya uteuzi wa Hans Pope
katika Kamati hiyo. Mwenye mamlaka hayo ni Kamati ya Utendaji ya TFF. Hivyo
Yanga walipaswa kuelewa hilo na si kuishinikiza kamati, hususan Mwenyekiti,
amuondoe Hans Pope kwenye Kikao.
TATU: Maamuzi ya Kamati
yamefungua njia kwa wachezaji wengi ambao mikataba yao inachezewa na vilabu kwa
muda mrefu pasipo kuwa na nafuu yoyote ya kisheria kwa wachezaji hao ambao ndio
nguzo ya muhimu katika mpira wa Tanzania. Hata hivi sasa kuna wachezaji ambao
bado hawajalipwa stahili za mikataba yao ndani ya Yanga. Tunawaomba wajitokeze
ili tuwasaidie wapate haki zao za kisheria kama ambavyo imetokea kwa Okwi.
NNE: Pamoja na madai ya
Yanga ya kukata rufaa FIFA / CAS, naomba wajue kuwa haki yao ya kukata rufaa
inatokana na ukweli kuwa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya TFF
imetekeleza wajibu wake. Uamuzi huo wa Kamati umejenga msingi muhimu sana
katika suala zima la kuheshimu na kutekeleza mikakaba kwa mujibu wa kanuni za
FIFA. Endapo Yanga watakata rufaa kama wanavyodai, itakuwa ni hatua muhimu
katika kuhakikisha nguzo ya kuheshimu mikataba ya wachezaji inapewa msisitizo
unaostahili.
MGOGORO KATI YA YANGA NA OKWI
Mkataba wa Yanga na Okwi, ambao ulisainiwa tarehe 12 Disemba
2014 umekuwa na mapungufu yafuatayo:
1.Mkataba
huo umempa majukumu mchezaji kufuatilia ITC na suala zima la yeye kupata vibali
vya kucheza. Hii ni kinyume na Kanuni za FIFA ambao zinatamka bayana kuwa
jukumu la kufuatilia ITC ni la wanachama wa FA, lakini Yanga walimtwisha Okwi
zigo hilo. Okwi alitekeleza jukumu hilo.
Kamati ililiona hilo na kusema wazi kuwa hilo sio sahihi. Ni
vema wachezaji wajue kuwa hilo sio jukumu lao.
2.Pili
Yanga, kwa mujibu wa mkataba, walikuwa na haki ya kumkata mchezaji theluthi
moja ya mshahara wake wa mwezi endapo atakosa mechi tatu au zaidi. Yanga
walimkata Okwi Mishahara ya miezi mitano, kinyume na matakwa ya mkataba na
pasipo maelelzo yoyote.
3.Yanga
na Okwi walikubaliana kuwa mchezaji atalipwa ada ya kusaini mkataba (signing on
– fee) ya US$ 100,000, kwa Awamu mbili. Awamu ya kwanza wakati wa kusaini
mkataba na awamu ya pili tarehe 27 Januari 2014. Mpaka hivi sasa, Yanga
wamelipa US$ 50,000 tu na bado kuna deni la US$ 50,000. Huu ni uvunjaji wa
mkataba wa wazi kabisa.
4. Kipindi
chote mchezaji akiwa na klabu ya Yanga, hajapewa nyumba kama ambayo
walikubaliana. Huu ni ukiukwaji mwingine wa mkataba.
Baada ya Okwi kuanza kudai haki zake tajwa hapo juu, Yanga
waliamua kutomlipa mteja wetu mishahara ya miezi mitano kinyume na matakwa ya
mkataba kati yao.
MPANGO WA SIRI WA YANGA
Yanga walikuwa na mpango wa siri wa kuvunja mkataba na Emmanuel
Okwi ili wamkomoe mteja wetu, ashindwe kucheza mpira, kiwango chake kiporomoke
na itumike kama onyo kwa wachezaji wengine ambao wanadai haki zao. Mpango huu
ulitekelezw kama ifuatavyo:
a.Tarehe
27 Juni 2014, Yanga waliandika barua kwenda TFF, ikiitaka TFF, pamoja mambo
mengine, itambue kuwa mkataba kati yao na Okwi umefutwa. Barua hiyo haikuwa na
nakala kwa Okwi, ambaye ndiye upande wa pili wa mkataba ambao unapaswa kufutwa.
b.Tarehe
25 Julai 2014, Yanga waliandika barua ya pili kukumbushia barua yao ya tarehe
27 Juni 2014. Barua hiyo ya pili haikuwa na nakala kwa Okwi, ambaye ndiye
upande wa pili wa mkataba ambao unapaswa kufutwa.
c.Tarehe
20 Agosti 2014 Yanga waliandika barua nyingine tena wakikumbushia hoja zao
tajwa hapo juu. Kwa mara ya tatu, barua hiyo haikuwa na nakala kwa Okwi, ambaye
ndiye upande wa pili wa mkataba ambao unapaswa kufutwa.
d. Yanga
waliandika barua nyingine ya nne tarehe 25 Agosti 2014 ikiwa na hoja zile zile
za kusitisha mkataba na mteja wetu. Kwa mara ya nne barua hiyo haikuwa na
nakala kwa Okwi, ambaye ndiye upande wa pili wa mkataba ambao unapaswa kufutwa.
Baada ya TFF kupanga tarehe ya kikao cha Kamati ya Sheria na
hadhi ya wachezaji na kutoa barua ya wito tarehe 27 Agosti 2014 ndipo kwa mara
ya kwanza mchezaji Emmanuel Okwi akafahamu kuwa Yanga wameomba kuvunja mkataba
wake.
Tarehe 27 Agosti 2014,
Emmanuel Okwi aliiandikia Yanga KUKUBALI ombi lao la kuvunja mkataba.
Mosi, Kama Mkataba ulikuwa
ni kati ya Yanga na Okwi, ni kitu gani kiliifanya Yanga ishindwe kumpa angalau
nakala ya barua nne ambazo ilizipeleka TFF?
Pili, Wakati Yanga
wanaomba kuvunja mkataba, walikuwa wameshamlipa Okwi stahili zake kwa mujibu wa
Mkataba huo?
Tatu, Je visingizio vya
kuvunjwa kwa mkataba wa Okwi vina uhusiano na idadi ya majina ya wachezaji wa
kigeni wa Yanga?
Ni bayana kuwa Yanga walitafuta kila aina ya kisingizio ili
mteja wetu aonekane kuwa ndio amevunja mkataba wakati ni wazi kuwa Yanga ndio
waliokuwa wa kwanza kuvunja mkataba huo tarehe 27 Januari 2014 kwa kushindwa
kumlipa mteja wetu US$ 50,000 za ada ya kusaini mkataba.
HOJA MBELE YA KAMATI
Mbele ya Kamati Yanga walileta hoja kuwa: Hans Pope ana mgongano
wa maslahi kwa kuwa amemsajili Okwi Simba na yeye ni mjumbe wa Kamati hii; Okwi
amekataa kuongeza au kupunguza mkataba kama ilivyopendekezwa na Yanga; Okwi
ameleta madai yasiyo na msingi ya kutaka apewe nyumba ya kuishi; hajacheza
mechi 6 hivyo kuikosesha Yanga ubingwa. Okwi amefanya makubaliano na Klabu ya
Wadi Geldi ya Misri wakati ana mkataba na Yanga. Hivyo basi Yanga waliitaka
Kamati itamke kuwa mkataba kati yao na Okwi umesitishwa, imfungie Okwi kucheza
mpira Tanzania Maisha na ailipe Yanga dola za kimarekani laki mbili.
Tukimwakilisha Okwi, tulitoa hoja kuwa: Mteja wetu amekubali
ombi la Yanga la kuvunja mkataba ambalo limo katika barua zake nne; Yanga ndio
wamevunja mkataba kwa kushindwa kulipa signing fee US$ 50,000; Mishahara ya
miezi mitano US$ 15,000 na kodi ya nyumba US$ 2,800. Madai hayo ni kwa mujibu
wa mkataba.
Baada ya Maswali toka kwa Kamati kwa pande zote mbili, Yanga
waliomba kufuta barua zao, ombi ambalo lilitupiliwa mbali na kamati.
Kamati, hatimaye ilifanya maamuzi ya kihistoria katika kulinda
haki za kimkataba za wachezaji kama ambayo imeelezwa hapo juu.Kwa mtu yoyote
mwenye akili timamu, anapaswa kuipongeza kwa dhati kamati kwa maamuzi ambayo
wanajenga mpira wa nchi hii. Vilabu vinapaswa kufahamu kuwa haki za mchezaji
lazima ziheshimiwe.
Hoja za Yanga kuwa hakukuwa na madai ya fedha sio sahihi
kwasababu Majibu toka kwa Okwi na mabishano ya maneno mbele ya kamati hiyo
ilijadili kwa kina madai ya fedha ya Okwi na hata Yanga walikiri kutolipa madai
hayo. Hivyo basi si sahihi kusema kuwa eti suala la madai ya fedha
halikujadiliwa. (ona kiambatisho MNA1)
Msingi wa malalamiko ya Yanga ni barua ya tarehe 27 Juni 2014,
ambayo hakuna sehemu ambayo inatamka suala la Simba. Kama kuna kesi dhidi ya
Simba, wasubiri wakati wa kupitia pingamizi za usajili lakini suala ambalo
Yanga walilalamikia ni kusitisha mkataba na Okwi na madai ya fidia.
Kamati ya Sheria na Mwenyekiti wake hawana mamlaka ya kujadili
uteuzi au uwepo wa Hans Pope kwenye kikao hicho. Mamlaka ya Uteuzi ndio, kwa
mujibu wa katiba ya TFF, yenye uwezo wa kutoa uamuzi kuhusu suala hilo.
Kwakuwa rufaa ni haki ya kila mtu, Uamuzi wa kukata rufaa Fifa /
CAS ni haki ya kisheria lakini tuwakumbushe Yanga kuwa “UKITAKA HAKI, TENDA
HAKI KWANZA”.
DK. DAMAS DANIEL NDUMBARO (PhD)
Maleta & Ndumbaro Advocates
Muwakili wa Mchezaji