Thursday, December 4, 2014

MECHI YA NANI MTANI JEMBE KUCHEZWA TAREHE 13 DISEMBA

Mechi ya Nani Mtani Jembe 2 kati ya Simba na Yanga zinazodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itachezwa Jumamosi, Disemba 13, 2014 saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Meneja Udhamini wa TBL, George Kavishe amesema kwamba “Tayari Simba na Yanga zimesaini makubaliano ya kucheza mechi ya Nani Mtani Jembe 2 (Nani Mtani Jembe 2 Match).
 Pambano hili ni zawadi ya kufungia mwaka kwa mashabiki na kila timu imetia saini makubaliano kwamba itachezesha kikosi cha kwanza ili kuwapa mashabiki burudani ya uhakika.”
Kavishe aliongeza kuwa mechi hii ni maalumu kwa ajili ya kuhitimisha kampeni ya Nani Mtani Jembe 2 ambayo imeendeshwa kwa zaidi ya miezi miwili ikiwapa fursa mashabiki wa timu hizi kuchangia timu zao kila wanapoburudika na bia ya Kilimanjaro Premium Lager.
Alisema Nani Mtani Jembe 2 inahusisha mashabiki wa klabu za Simba na Yanga ambapo zawadi ya shilingi milioni 100 itatolewa na kugawanywa ifuatavyo.
  • Shilingi Milioni 20 ni zawadi ya mechi ya Nani Mtani Jembe ambapo timu itakayoshinda itapata sh milioni 15 na timu itakayofungwa itapata shilingi milioni 5.
  • Kampeni hii inaendeshwa kwa njia ya sms ambapo mashabiki wanapiga kura kwa njia ya sms na shilingi milioni 80 zimegawanywa kati ya timu hizo mbili ambapo kila timu ilianza na shillingi milioni 40 kwenye benki maalumu mtandaoni.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli alisema mashabiki wa Simba na Yanga wanaweza kushiriki kwa kununua bia ya Kilimanjaro Premium Lager yenye ujazo wa mililita 500 ambapo mteja atabandua ganda la kizibo cha bia ya Kilimanjaro Premium Lager na kuona namba maalumu. Ataandika jina la timu yake (SIMBA au YANGA) ikifuatiwa na namba hiyo ya kwenye kizibo ambayo anatuma kwenda namba 15415 na kwa kufanya hivyo anakuwa amepunguza pesa taslimu shilingi 10,000 kutoka timu pinzani na kuichangia timu yake.
Kikuli pia alizikabidhi timu hizo jezi maalumu itakayovaliwa mahususi kwa ajili ya mechi hiyo na kuwahimiza mashabiki waendelee kuzipigia kura timu zao na kikubwa kuhakikisha wanafika uwanja wa taifa na kujionea wenyewe pambano hilo ambalo lazima mshindi apatikane.
Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura aliwakaribisha mashabiki na kuwaomba wajitokeze kwa wingi kwani hivi sasa timu hizo ziko kambini zikijiandaa na mtanage huo wa kukata na shoka unaotarajiwa kuwa na msisimko mkubwa.
Alitaja viingilio vya mechi hiyo kuwa ni shilingi 30,000 kwa VIP B, 20,000/= VIP C, 15,000/= kwa viti vya rangi ya chungwa kiingilio kitakuwa ni sh 15,000 huku viti vya bluu na kijani tiketi zikiuzwa kwa sh. 7,000/=.
Wambura alisema pambano hilo litakalosimamiwa na TFF litaanza saa kumi kamili na litachezwa kwa dakika 90 tu ambapo kama muda huo timu hizo hazitafungana basi mikwaju ya penati itapigwa ili mshindi apatikane.
Taji la Nani Mtani Jembe linashikiliwa na Simba ambao waliwafunga mahasimu wao 3-1 katika mechi iliyochezwa Disemba 21, 2013.

Tuesday, December 2, 2014

MANDAWA MCHEZAJI BORA WA VPL NOVEMBA

Mshambuliaji wa timu ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa mwezi Novemba mwaka huu ambapo atazawadiwa kitita cha sh. milioni moja.
Mandawa ambaye kwa mwezi huo alichuana kwa karibu na mshambuliaji Fulgence Maganda wa Mgambo Shooting ya Tanga na nahodha wa Simba, Joseph Owino atakabidhiwa zawadi yake na wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya Vodacom.

Hafla ya kukabidhi zawadi hiyo inatarajiwa kufanyika wakati wa mechi ya raundi ya nane ya ligi hiyo kati ya Simba na Kagera Sugar itakayochezwa Desemba 26 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
KOZI YA UKUFUNZI WA UTAWALA YA FIFA SASA MACHI.
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limesogeza mbele kozi ya ukufunzi ya utawala wa mpira wa miguu iliyokuwa ifanyika Desemba mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa FIFA, kozi hiyo sasa itafanyika Machi mwakani katika tarehe itakayotangazwa baadaye.

TFF imepokea maombi ya zaidi ya washiriki 40 kwa ajili ya kozi hiyo itakayoshirikisha washiriki 30. Kutokana na maombi kuzidi idadi ya nafasi zilizopo, FIFA itafanya mchujo wa washiriki.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

MIKOA MITANO YATAKIWA KUWASILISHA USAJILI COPA 2014

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeitaka mikoa mitano kuwasilisha usajili wa wachezaji wake kwa ajili ya mashindano ya Taifa ya Copa Coca-Cola 2014 kabla ya Desemba 5 mwaka huu.

Mikoa hiyo ambayo haijawasilisha usajili wake hadi sasa kwa ajili ya michuano hiyo inayoanza Desemba 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam ni Arusha, Dodoma, Katavi, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Mjini Magharibi na Simiyu.

Kwa mujibu wa Kamati ya Mashindano ya michuano hiyo, mkoa ambao hautawasilisha usajili wake kwa ajili ya uhakiki wa umri wa wachezaji utakaonza Desemba 10 mwaka huu utaondolewa katika fainali hizo zitakazomalizika Desemba 20 mwaka huu.

Wachezaji watakaobainika kuzidi umri hawataruhusiwa kushiriki katika michuano hiyo inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 15. Kwa mujibu wa Kanuni ya 29 ya michuano kuhusu idadi ya wachezaji, kila timu inatakiwa kuwa na wachezaji wasiozidi 20 na wasiopungua 16.

Hivyo, kila timu inatakiwa kuhakikisha inakuwa na idadi hiyo ya wachezaji, kwani kikanuni wakipungua 16 itaondolewa kwenye mashindano.

Timu 16 kwa upande wa wavulana zitashiriki katika fainali hizo wakati kwa upande wa wasichana ni timu nane. Mikoa iliyoingiza timu za wasichana kwenye fainali hizo ni Arusha, Dodoma, Ilala, Kinondoni, Mbeya, Mwanza, Temeke na Zanzibar.

CAF YAWEKA HADHARANI MAJINA YA TIMU SPECHO KWA DROO KUPANGWA.

WASHIRIKI 16 wa Fanali za Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2015, ambazo zitachezwa huko Nchini Equatorial Guinea kuanzia Januari 17, watajua nani Wapinzani kwenye Makundi yao Leo Jumatano makundi ya Timu 4 kila moja kutajwa kwa ajili ya Droo hiyo na CAF.
Droo hiyo itafanyika Mjini Malabo Nchini Equatorial Guinea.
Timu hizo 16 zimepangwa kwenye Vyungu Vinne vya Timu 4 kila moja na kwenye Droo kila Chungu kitatoa Timu moja ili kupanga Makundi Manne.
CHUNGU 1
Equatorial Guinea, Ghana, Zambia, Burkina Faso
CHUNGU 2
Ivory Coast, Mali, Tunisia, Algeria
CHUNGU 3
Cape Verde, South Africa, Gabon, DR Congo
CHUNGU 4
Cameroon, Senegal, Guinea, Congo

POLISI MORO NA MWADUI FC ZAMTOLEA MACHO KINDA MIRAJI ADAM LA SIMBA

Timu Polisi ya Morogoro na Mwadui FC ya Shinyanga zimewasilisha barua kumuomba beki wa pembeni Miraj Adam wa Simba SC kwa mkopo baada ya kushushwa Simba B.
Polisi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania inapambana na Mwadui FC, inayopigania kupanda Ligi Kuu pia kuwania huduma za beki huyo aliyetokea timu ya vijana ya Wekundu hao wa Msimbazi.
Mwadui wanaamini wanaweza kumpata kwa urahisi beki huyo kwa sababu ya mahusiano mazuri ya kocha wao, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na klabu ya Simba SC.
Lakini Polisi nayo inaamini inaweza kumpata kwa urahisi beki huyo wa kulia, Miraj, kwa sababu inacheza Ligi Kuu kwa sasa na Morogoro si mbali sana na Dar es Salaam anakoishi mchezaji huyo.

Kwa sasa, Miraj ameshushwa kikosi cha pili baada ya mechi saba za awali za Ligi Kuu, lakini Simba SC bado haijaamua kumtoa kwa mkopo hadi hapo itakapofanikisha kusajili mchezaji mwingine wa nafasi hiyo.

VITA KALI YA BALLON D"OR MESS VS RONALDO VS NEUER JAN 12/2015.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limetangaza orodha ya wachezaji watatu watakaogombea tuzo ya mchezaji ya mchezaji bora wa mwaka wa dunia maarufu kama Ballon d’Or. 
Wachezaji hao watatu waliopenya katika mchujo wa wachezaji 23 ni pamoja na nyota wa kimataifa wa Ureno na klabu ya Real Madrid Cristiano Ronaldo, Lionel Messi wa Argentina na klabu ya Barvelona na Manuel Neuer kutoka Ujerumani na timu ya Bayern Munich.
Sherehe za utoaji tuzo inatarajiwa kufanyika Januari 12 mwakani huku Ronaldo akiwa ndio mshindi wa mwaka jana. Kwa upande wa wanawake walioteuliwa kugombea tuzo hiyo ni pamoja na Nadine Kessler wa Ujerumani, Marta wa Brazil na Abby Wambach kutoka Marekani. 
Kwa upande wa makocha walioteuliwa kugombea tuzo ni pamoja na Carlo Ancelotti wa Real Madrid, Joachim Loew aliyeiwezesha Ujerumani kunyakuwa Kombe la Dunia na kocha wa Atletico Madrid Diego Simeone.

Monday, December 1, 2014

WATOTO OBAMA VITUKO NDANI YA SKENDO CHAFU YA MAVAZI YA UWAZI.TAZAMA PICHA ZOTE HAPA

 


Rais Barrack Obama na wanawe Sasha na Malia. Afisa mmoja wa chama cha Republican amewakosoa mavazi yao.Watoto wa rais wa Marekani Barrack Obama, Sasha na Malia wameshtumiwa kwa kukosa heshima na afisa mmoja wa chama cha Republican baada ya kuhudhuria sherehe za kutoa shukrani.
Elizabeth Lauten ,ambaye ni mkurugenzi wa mawasiliano wa mbunge Stephen Fincher alitoa matamshi yake katika mtandao wa 
facebook
 ambayo baadaye yalifutwa.

Baada ya kukosolewa Bi Lauten aliomba msamaha kwa kutoa matamshi hayo ya kukera.

Aliku akikosoa sketi fupi zilizovaliwa na wasichana hao wa Obama.Bi Lauteni 
pia
 aliwashtumu wasichana hao kwa kuonyesha uchovu wakati waliposimama na baba yao katika sherehe hiyo ya ikulu ya Whitehouse.