Saturday, May 18, 2013

FERGUSON BALE WATWAA TUZO YA MSIMU WA BPL LIGI KUU UINGEREZA.

Meneja wa Manchester United,Sir Alex Ferguson na Mchezaji wa Tottenham Gareth Bale jana walipewa tuzo za msimu wa ligi kuu ya Uingereza.
Ferguson ameshinda tuzo ya kocha bora wa msimu huku Bale akitwaa tuzo ya mchezaji bora wa msimu huu unaomalizika kesho na tayari Man United imetwaa ubingwa huo.
Hii inakuwa tuzo ya 11 kwa Ferguson na akiwa ameshinda makombe 38 na United huku 13 yakiwa ya ligi kuu ya Uingereza.Pia akiwa ametangaza kustaafu baada ya kuifundisha timu hiyo kwa miaka 26 na Jumapili hii atakua anakamilisha mechi yake ya 1,500 tangu aanze kuifundisha timu hiyo.
Bale akiwa amefunga magoli 19 msimu huu huku akiwa amecheza michezo 29 amekuwa mchezaji wa kwanza wa Tottenham na raia wa Wales kutwaa tuzo hiyo.
Hii ni tuzo ya nne kwa mchezaji huyo kutoka Wales baada ya kuchukua ile ya mchezaji bora wa PFA,Mchezaji bora chipukizi na Mchezaji bora wa Chama cha Waandishi wa habari za soka nchini Uingereza.
Tottenham watakuwa na kazi kubwa ya kumbakiza Gareth Bale katika klabu hiyo kutokana na kiwango bora alichoonesha msimu huu kwani timu nyingi zimeonyesha nia ya kutaka kumnyakua.