SERIKALI ya nchini Brazil imesema baadhi ya roboti za kuimarisha usalama
zilizonunuliwa kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia 2014 zitakuwa tayari
kutumika wakati wa Kombe Shirikisho itakayoanza kutimua vumbi Juni mwaka
huu. Kampuni ya iRobot imesema roboti 30 zitawasilishwa kabla ya mwisho wa
mwaka pamoja na vipuri na vifaa vingine vya kusaidia katika
kuzitumia. Serikali ilithibitisha Alhamisi kuwa baadhi zitakuwa tayari
kutumiwa katika miji sita itakayokuwa wenyeji wa mechi za Kombe la Shirikisho. Kampuni
hiyo imesema serikali ya Brazil iliyotia saini mkataba wa $7.2 milioni, ambao
unahusisha magari madogo yasiyokuwa na dereva ambayo yanaweza kutumiwa
kupeleleza, kupekua na kuondoa mabomu pamoja na shughuli nyingine za kudumisha
utawala wa sheria. Michuano ya Kombe la Shirikisho ni ya kwanza katika
msururu wa hafla za ngazi ya juu za michezo zitakazoandaliwa na Brazil, ikiwa
ni pamoja na Kombe la Dunia na Olimpiki 2016 jijini Rio de Janeiro.