SHIRIKISHO la Soka la
Ethiopia-EFF limemtimua kibarua katibu mkuu wake baada ya kukiri
kumtumia mchezaji kimakosa katika mechi za kufuzu michuano ya Kombe la
Dunia 2014 hatua ambayo inaweza kuigharimu timu nchi hiyo kukatwa alama
tatu. Kamati ya
Utendaji ya EFF ilipiga kura za kumtimua katibu huyo aitwaye Ashenafi
Ejigu lakini walipinga barua ya kujiuzulu kwa makamu wa rais wa
shirikisho hilo Berhanu Kebede ambaye ndiye alikuwa akilaumiwa kutokana
na mkanganyiko huo. Baadhi
ya wajumbe na waandishi wa habari za michezo waliokuwepo katika mkutano
huo walikuwa wakitaka uongozi mzima wa shirikisho hilo ujiuzulu kwa
kile walichokiita uzembe. Rais
wa EFF, Sahilu Gebremariam alikiri kuwa suala hilo ni la kizembe na
wanapaswa wote kujiuzulu na kudai kuwa atafanya hivyo katika mkutano
mkuu utakaofanyika Septemba mwaka huu. Akihojiwa
kuhusiana na suala la kumchezasha mchezaji aliyepewa kadi mbili za
njano kocha wa Ethiopia Sewnet Bishaw alijitetea kuwa anapokuwa uwanjani
huwa hatumii karatasi na kalamu anachofanya yeye ni kuhakikisha timu
inapata matokeo mazuri.