KATIBU Mkuu wa
Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Jerome Valcke amesema kuwa hawana
mpango wa kubadili mahali patakapochezwa michuano ya Kombe la Dunia
mwakani. Valcke
alibainisha kwamba michuano hiyo itafanyika nchini Brazil katika miji 12
kama ilivyopangwa na hakuna mpango mwingine wowote wa kuhamisha
mashindano hayo kwenda sehemu nyingine. Kauli
ya Valcke imekuja kufuatia maandamano ambayo yamekuwa yakiendelea
nchini humo wakati huu wa michuano ya Kombe la Shirikisho wakipinga
gharama kubwa za matayarisho ya Kombe la Dunia wakati wananchi wake wana
hali duni katika maisha yao ya kawaida. Valcke
pia alipinga kauli ya Waziri wa Michezo wa Brazil, Aldo Rebelo
aliyekuwa amekaa pembeni yake katika mkutano na waandishi wa habari
aliyedai kwamba kuna nchi zimeonyesha nia ya kuwa mwenyeji wa mashindano
hayo kama Brazil ikijitoa. Katibu
mkuu huyo amesema hajapokea ofa yoyote kutoka katika nchi yoyote
duniani kutaka kuandaa michuano hiyo ya 2014 na kumuondoa hofu Rebelo
ambaye alidai amesoma katika vyombo vya habari kwamba nchi za Marekani,
Uingereza, Ujerumani na Japan zinamendea nafasi hiyo.