Mabingwa wa soka Tanzania Bara , Afrika Mashariki
na Kati, Klabu ya Dar Young Africans watacheza mechi za kirafiki dhidi
ya Rayon Sport ya Rwanda Julai 6 na 7, mwaka huu katika sehemu ya ziara
yake ya kulitembeza Kombe lake la ubingwa wa Ligi Kuu mikoa ya kanda ya
Ziwa inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake,
Kilimanjaro Premeum Lager.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka kwa kaimu katibu mkuu wa Yanga Lawrence
Mwalusako , Yanga maarufu kama Kwalalumpa Malysia itaondoka Dar es
Salaam Julai 5, siku mbili tu baada ya kuanza mazoezi Uwanja wa
sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam kuelekea Mwanza tayari kwa
mchezo wa kwanza dhidi ya mabingwa hao wa zamani wa Afrika Mashariki na
Kati, Uwanja wa CCM Kirumba, Julai 6.
Baada
ya kipute hicho, Julai 7, timu hizo ambazo zimewahi kufundishwa na
kocha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Raoul Jean Pierre
Shungu kwa wakati tofauti na kwa mafanikio, zitarudiana kwenye Uwanja wa
Kambarage mjini Shinyanga.
“Yanga
tuna mipango mingi sana, bahati mbaya tumeshindwa kwenda Sudan kutetea
ubingwa wetu wa Kagame, lakini bado tuna michuano mikubwa barani Afrika,
ikiwa ni heshima kwa mashabiki wetu na wanachama wanaotuunga mkono, ni
nafasi yao kuliona taji letu la ligi msimu uliopita, tutapita mikoani na
kushangilia pamoja”. Alisema Mwalusako.
Baada ya hapo , Yanga SC
wataelekea mjini Tabora, kucheza mechi nyingine na wenyeji, Rhino FC
waliopanda Ligi Kuu msimu huu Julai 11, mwaka huu Uwanja wa Ally Hassan
Mwinyi.
Katika
ziara hizo, Yanga watatembeza Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu,
walilolitwaa kwa mara ya 24 msimu huu kwenye mitaa mbalimbali
kushangilia na mashabiki wao.
Yanga
SC, imekuwa na mafanikio makubwa tangu ianze kudhaminiwa na TBL mnamo
2008, ikitwaa jumla ya mataji sita katika kipindi hicho, yakiwemo mawili
ya Kagame, 2011 na 2012 na manne ya Ligi Kuu Bara, 2008, 2009, 2011 na
2013.
Agosti 2, mwaka 2011, TBL ilisaini Mkataba wa udhamini na Yanga wa miaka minne sawa na kwa watani wao pia, Simba SC.
Katika
mkataba huo mpya, uliotiwa saini kwenye hoteli ya Double Tree, Masaki,
Dar es Salaam, TBL iliongeza dau la fedha za mishahara kwa wachezaji
kutoka Sh. Milioni 16 hadi Milioni 25 kwa mwezi, ikaongeza basi moja
kubwa, Yutong lenye uwezo wa kubeba abiria 54 na fedha kwa ajili ya
kugharamia mikutano ya wanachama ya kila mwaka Sh. Milioni 20 kugharamia
tamasha la mwaka la klabu na vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh.
Milioni 35 kila msimu.
Yanga pia inapewa bonasi ya Sh. Milioni 25 ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu
Bara au Milioni 15, ikishika nafasi ya pili katika Mkataba huo wenye
thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 5 tangu Agosti 8, mwaka huu hadi Julai
31, mwaka 2016.