
Wadau wengi wamekuwa wakihoji kufanyika kwa Mkutano huo wakati Nchi inakabiliwa na Mechi muhimu Siku hiyo hiyo huku wengine wakidiriki kudai kuna walakini ndani yake.
Lakini Rais wa TFF, Leodegar Tenga, amefafanua kuwa vitu hivyo viwili haviwezi kuleta mgongano kwani Mechi itachezwa kwa Dakika 90 na Mkutano Mkuu umepangwa kuwa wa Siku mbili.
Tenga alisema: “Hamna njama zozote. Vitu hivyo viwili vitaendelea kama ilivyopangwa.”
Akifafanua, Tenga alisema Wajumbe wa Mkutano Mkuu wamezoea kujadili Ajenda hadi 12 katika Siku moja lakini safari hii Ajenda ni moja tu na imepangiwa Siku mbili.
Ajenda ya Mkutano Mkuu huo ni kujadili na kupitisha Mabadiliko ya Katiba ili kuruhusu Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho hilo ufanyike kama ilivyoagizwa na FIFA.
Awali Uchaguzi ulikuwa ufanyike hapo Februari 24 lakini ukatokea mgongano mkubwa baada ya baadhi ya Wagombea kufutwa na pia madai kuwa Katiba ilibadilishwa bila kufuata taratibu.
Akifafanua zaidi, Tenga alisema upo uwezekano mkubwa kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu kumaliza Kikao chao kabla hata Mechi kuchezwa.