Friday, February 14, 2014

DALADALA DAR ZATANGAZA MGOGORO NA SUMASTA.

    
Wamiliki wa daladala wametangaza mgogoro na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini nchini (Sumatra) wakipinga kile walichokiita upendeleo unaodaiwa kufanywa na Sumatra kwa mabasi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) na kuzikandamiza daladala katika utaratibu wa utoaji huduma ya usafiri jijini humo.
Wamedai upendeleo huo, mbali ya kuzikandamiza daladala, pia umekuwa ukiwanyonya wananchi kimapato, ambao wamekuwa wakijikuta wakilazimika kulipa nauli mara mbili (Sh. 800 na kuendelea) kwenye ruti, ambayo nauli yake halali ni Sh. 400.

Tamko la wamiliki hao lilitolewa kwa pamoja na Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa (Darcoboa) na Umoja wa Wasafirishaji Abiria Dar es Salaam (Uwadar), kupitia viongozi wao wakuu, jana.
Mwenyekiti wa Darcoboa, Sabri Mabrouk, alisema mabasi ya Uda hayajapangiwa ruti kama ilivyo kwa daladala, na pia kuna habari kwamba, kuanzia wiki ijayo yataruhusiwa kuweka vibao vinavyoonyesha ruti yanakokwenda na hivyo kuwa na haki ya kwenda sehemu yanakotaka.
Alisema zaidi ya hivyo juzi mabasi hayo yaliruhusiwa peke yake kuchukua abiria kutoka kituo cha Mnazi Mmoja kwenda Kivukoni, huku daladala za Kivukoni zikitakiwa kuishia Mnazi Mmoja.

Alisema kama mabasi ya Uda yataendelea kupeleka abiria Kivukoni ifikapo Jumatatu wiki ijayo, daladala nazo pia zitafanya hivyo.

“Hili ni tangazo kwa madereva wetu wa daladala zinazokwenda Kivukoni. Tunawaambia wakiona Uda wanapeleka mabasi yao Kivukoni, nao pia wapeleke magari yote Kivukoni… Katika hili tunawaambia trafiki wasiingilie ugomvi huu.

Sisi tunadai haki za wanachama wetu kwa sababu haki haiombwi ikibidi inadaiwa kwa nguvu,” alisema Mabrouk.

Mabrouk alisema kimsingi hawana ugomvi na Uda kama ambavyo hawana haki ya kuwazuia kuingiza mabasi, lakini akasema wanachokitaka ni kuwapo na uwanja sawa katika utoaji wa huduma ya usafiri Dar es Salaam.


Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simon Group inayomiliki mabasi ya Uda, Robert Kisena, alipoulizwa kuhusiana na madai hayo, alisema wameshajipanga kwa hilo.
Alisema kuanzia wiki ijayo wataanza kutoa huduma ya usafiri jijini kwa kuzingatia ruti na kwamba, hakutakuwa na kuingiliana katika ruti.

“Haya siyo masuala ya kugombana, ni masuala ya kukaa na kuangalia tufanye vipi,” alisema Kisena. 
 Na:mwamdishi wetu Dar