Friday, February 14, 2014

KIA WAJIPANGA KUKABILIANA NA DAWA ZA KULEVYA

                                                       Uwanja cha Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA)
Uongozi wa Uwanja cha Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), umeahidi kuongeza jitihada za kupambana na usafirishaji wa dawa za kulevya kutokana maboresho yaliyofanyika katika kitengo cha usalama cha uwanja huo.

Tamko hilo limekuja siku chache baada ya Mtanzania Mastura Makongoro, mwenye hati ya kusafiria namba AB26695, kukamatwa na dawa za kulevya zinazodhaniwa kuwa ni aina ya cocaine zenye uzito wa kilo 4.8 akielekea nchini Ghana.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Fedha na Huduma za Kibiashara wa Kampuni ya Uendelezaji Viwanja (Kadco), Bakari Murusuri, ilisema uwanja huo umejidhatiti kupambana na usafarishaji wa dawa za kulevya kupitia hapo.

Murusuri alisema maofisa usalama wa uwanja huo Jumanne usiku wa manane  wiki hii, walimkamata mwanamke huyo wakati akisubiri kupanda ndege ya Shirikia la Ethiopia kuelekea Addis Ababa.

“Mizigo yote ya abiria imekuwa ikichunguzwa kwa umakini mkubwa katika sehemu ya kuchunguza mizigo na safari hii tumefanikiwa mzigo mmoja uligundulika kuwa na shaka na vitu vilivyokuwa ndani kwa kuonyesha dalili ya kuwa ni dawa za kulevya," alisema.

Aliongeza: “Baada ya kuuchunguza mzigo huo kwa umakini, iligundulika ulikuwa na dawa za kulevya ambazo zilifungwa juu na chini kabisa ya begi lake yenye uzito wa kilo 4.8.”

Alisema wakati wa uchunguzi, mwanamke huyo alikiri kuwa aliambatana na mwenzake raia wa Nigeria aliyemtaja kwa jina la Mike Nwankwo (41), ambaye alimsindikiza mpaka uwanjani na alikuwa ni miongoni mwa mtandao wa wasafirishaji wa dawa hizo.

“Jeshi la Polisi na walinzi wa usalama hapa uwanjani waliunganisha nguvu ili kumsaka mtu huyo na baadaye alikutwa kwenye maegesho ya magari akisubiri kuhakikisha kuwa mwanamke huyo ameondoka nchini,” aliongeza.

Murusuri alisema tangu Machi, 2013 mpaka sasa, uwanja huo wa ndege umefanikiwa kukamata watu tisa wakihusishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya na kuahidi kuwa uwanja huo sasa umejipanga kikamilifu kukabiliana na suala hilo.

“Tumeongeza ulinzi wa kutosha hapa KIA ili kuondoa mianya katika taratibu za kiusalama kwa upande wa mizigo na uchunguzi kwa ujumla.
Hili litatuwezesha kuhakikisha kuwa uwanja wetu wa ndege hauwi kitovu cha usafirishaji dawa za kulevya,” aliongeza.
Chanzo: Nipashe'.